Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, May 27, 2015

Huu Ndiyo Uamuzi Unaotakiwa Kuufanya, Ili Kubadilisha Maisha Yako Kabisa.

No comments :
Ni kitu ambacho huwa kinanitokea mara kwa mara  hasa pale ninapokuwa katika mazungumzo na baadhi ya jamaa zangu wakijaribu kuzungumzia jinsi hali ya maisha ilivyokuwa ngumu. Ni maelezo hayo hayo ambayo huwa ninakutana nayo nikiwa mtaani na maeneo mengine mengi, ambayo yamekuwa kama wimbo na kusababisha wengi kuamini kuwa hali zao ni ngumu na hawana uwezo wa kubadilisha maisha yao tena.

Na hivi karibuni niliweza kupokea ujumbe kwa njia ya barua pepe kutoka kwa moja ya wasomaji wetu wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO, akijaribu kunieleza kitu kama hicho ambacho wengi wanacho na kinawapa changamoto kubwa katika maisha yao kwa ujumla.

Ni maisha hayo hayo ambayo wamekuwa nayo Watanzania wenzangu wengi wakiamini hali zao ni ngumu sana  na haziwezi kubadilishwa kwa namna yeyote ile. Wengi wamekuwa wakiamini zaidi vitu vingi ambavyo viko nje ya wao kama mfumo mbaya ama uchumi mbovu ndiyo umewakwamisha na kuwafikisha hapo walipo.


Kama umekuwa ukiishi katika fikra hizo na kuamini kabisa kuwa upo katika hali ngumu sana, unachotakiwa kufanya sasa ni kubadilisha mawazo yako hayo mara moja. Kila kitu kinawezekana kwako, hakuna kisichowezekana hata iweje. Unachotakiwa kufanya wewe ni  kuamka pengine kwenye usingizi uliolala wa kutokutambua kuwa hata wewe unaweza kufanikiwa tena kwa viwango vya juu.Huna haja tena ya kuamini kuwa huwezi ama kulaumu sana. Uwezo na nguvu kubwa ya kubadilisha maisha yako unayo. Wewe ndiye mwenye uwezo wa kubadilisha matokeo ya  maisha yako kulingana na maamuzi unayofanya kila siku na kila mara katika maisha yako. Acha kujiaminisha sana vitu unavyoweza kuvibadilisha. Unao uwezo wa kugeuza matokeo ya maisha yako bila ubishi.

Hata kama imesemwa sana na ikafika mahali na wewe ukaamini kuwa wewe  ni maskini, huo sio mwisho wa mafanikio yako eti tu kwa sababu ya kauli hizo, nasema tena huo sio mwisho wa mafanikio yako. hata kama una hali ngumu sana na familia uliyotoka haijiwezi kabisa, lakini hata hivyo bado ninayo sababu ya kukwambia unaweza kutoka huko na kuwa tajiri wa kesho na unayeheshimika.

Utaweza kutoka huko, ikiwa wewe leo hii utaamua kubadili jambo moja  tu.  Kwa kubadili jambo hilo utakuwa umemudu kuweza kubadilisha maisha yote kabisa. Na jambo ambalo unatakiwa ulibadili kwa haraka sana ili kuweza kuishi maisha ya mafanikio ni namna wewe unavyowaza juu ya umaskini ulionao. Huu ndiyo uamuzi unaotakiwa kuufanya ili kubadilisha maisha yako kabisa.

Mabadiliko makubwa ya maisha yako yanategemea jinsi unavyowaza. Kama utaendelea kuwaza kuwa huwezi na ni maskini wa kutupwa ndivyo itakavyokuwa. Leo hii upo hapo ulivyo kutokana na matokeo ya mawazo uliyokuwa nayo hapo awali. Kwa kufanya uuamuzi wa kubadilisha fikra zako utakuwa umefanya uamuzi ambao utabadilisha maisha yako kwa sehemu kubwa sana.


Kumbuka kuwa, fikra ulizonazo  zinakuwa zinakupa mtazamo wa aina fulani iwe hasi ama chanya. Kama mtazamo ulionao unakuwa ni hasi na ukabaki nao kwa muda mrefu, hatimaye hujitokeza katika maneno na matendo. Kwa mtu mwenye mtazamo chanya na anayewaza mafanikio katika maisha yake, ni kawaida kumkuta akizungumzia mafanikio na hata matendo yake yatadhihirisha hilo pia.

Kwa hiyo, mawazo aliyonayo mtu juu ya maisha yake huweza kudhihirika kwa urahisi katika maneno yake. Unapoona mtu amekata tamaa juu ya maisha yake na kuamua kuishi maisha ya kimaskini, chanzo au asili yake ni mawazo yake. Msaada mkubwa anaotakiwa kupata mtu huyu ni kuweza kufanya uamuzi wa kubadili mawazo yake jinsi anavyo uwazia huo umaskini.  

Hivyo ninaweza kusema kuwa, umaskini na utajiri ni suala linalohusisha mawazo zaidi kuliko kuwa au kutokuwa nacho. Kama ukitaka kubadilisha hali ngumu ya maisha uliyonayo, kitu cha kwanza unachotakiwa kushughulika nacho ni mawazo uliyonayo. Na utakuwa na mawazo chanya ikiwa utachukua jukumu la kujifunza kila siku na kukaa na watu wenye mtazamo chanya juu ya maisha. Huu ndio uamuzi utakaoweza kubadilisha maisha yako kabisa.

Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi kila siku.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,  

No comments :

Post a Comment