Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, July 7, 2016

Kilimo Cha Ufuta Na Faida Yake Kwa Mkulima.

No comments :
Ufuta (sesamum indicum) ni zao linalolimwa kwa wingi katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani, Morogoro, Dodoma, Tanga na ukanda wa chini katika mikoa ya Rukwa na Mbeya. Zao hili hulimwa kwa ajili ya chakula na biashara. Mbegu za zao hili huwa na wastani wa mafuta kiasi cha asilimia 45.
Kwa sasa soko la ufuta Tanzania ni zaidi ya mara tatu ya uzalishaji wake, kwa mantiki hiyo zao hili lina soko kubwa sana. Uzalishaji wake unafanyika kwa kiasi kidogo kwa sababu wakulima wamekuwa wakilima zao hili la ufuta kwa mazoea na kutumia mazao yake kama nafaka ya kutengeza vyakula mbalimbali kama kashata. Lakini kama utalima kibiashara ni zao ambalo linaweza kukomboa jamii yetu kutoka katika dimbwi la umasikini.
UZALISHAJI WA ZAO LA UFUTA MBEGU.
Chagua aina ya mbegu inayotoa mazao mengi na bora, inayovumilia mashambulizi ya magonjwa na wadudu, inayokomaa mapema na kutoa mafuta mengi.
Chagua mbegu inayokomaa kwa pamoja ili kurahisisha uvunaji na pia kuepuka upotevu wa zao shambani. Aina nyeupe ya mbegu ya ufuta hupendelewa zaidi kuliko aina nyeusi.
Mbegu bora ya ufuta inayopendekezwa ni LINDI 02, mbegu ambayo imefanyiwa utafiti na chuo cha utafiti NALIENDELE. Kwa wastani mbegu hii hutoa kati ya gunia 10 mpaka 15 ukifuata kanuni za kilimo bora.
Mbegu hii hukomaa ndani ya siku mia (100) mpaka mia na kumi(110). Aina hii ya ufuta ina asilimia 55 ya mafuta. Hii ni habari njema kwa wakulima kutoka kwa watafiti wetu wa Kilimo kutoka kituo cha Utafiti Naliendele, Mtwara.

Mkulima akiwa kwenye shamba lake la ufuta.
UPANDAJI.
Panda mbegu nusu inchi chini ya udongo, inchi sita umbali wa mbegu na mbegu na futi mbili nafasi ya msitari na msitari, kabla ya kupanda hakikisha ardhi imelowana vya kutosha na upande mbegu masaa mawili au matatu baadae.
MBOLEA.
Ufuta unahitaji rutuba ya kutosha ili kutoa mazao bora. Katika kudumisha rutuba ya udongo, tumia kilimo cha mzunguko wa mazao au weka mbolea za asili pale inapobidi.
PALIZI.
Dhibiti magugu kwa kupalilia ili kuruhusu ufuta kutumia vizuri unyevu na virutubishi. Magugu mengine huwa ni maficho ya wadudu waharibifu wa zao la ufuta.
MAGONJWA.
Ufuta hushambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali ambao huweza kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Hivyo kagua shamba mara kwa mara hasa kwenye maua na mapodo ili kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili zamashambulizi, chukua tahadhari mapema kabla ya uharibifu mkubwa haujatokea.
MAANDALIZI KABLA YA KUVUNA.
Kagua shamba kuona kama ufuta umekomaa. Ufuta hukomaa, kati ya miezi mitatu na minne tangu kupanda kutegemea aina. Aina ya ufuta usiokuwa na matawi hukomaa mapema kuliko ile yenye matawi. Ni muhimu kuwahi kuvuna ili kuepuka ufuta kupukutikia shambani.
DALILI ZA KUKOMAA UFUTA SHAMBANI.
Kwa kawaida majani hubadilika rangi kutoka kijani na kuwa ya manjano na hatimaye kudondoka. Mashina hubadilika rangi kutoka kijani na kuwa ya kahawia.
Mbegu za ufuta.
VIFAA VYA KUVUNIA.
Tumia kamba, siko na panga kipindi cha kuvuna.
VIFAA VYA KUKAUSHIA.
Hakikisha Sehemu ya kukaushia ni safi na yenye Sakafu ya saruji na pamefunikwa vizuri. Waweza tumia maturubai kufunika sehemu ya kukaushia.
USAFIRI.
Mikokoteni,Matela ya matrekta au Magari
KUVUNA.
Vuna ufuta mapema kabla mapodo kukomaa sana na kuanza kupasuka na kuachia punje. Mapodo ya ufuta yaliyokomaa sana yakiguswa au kutikiswa na upepo hupasuka na kuachia mbegu, hali inayosababisha upotevu mkubwa. Mbegu za ufuta ni ndogo na zikidondoka chini ni vigumu kuziokota. Vilevile mbegu zilizodondoka ni vigumu kuzitenganisha na uchafu.
Uvunaji wa ufuta huhusisha ukataji wa mimea yenye mapodo kwa kutumia vyombo vya mkono kama panga kwa kukata mashina. Kwa aina za ufuta zenye mapodo yanayopasuka, uvunaji ufanyike wakati mimea bado ni kijani ili kuepuka upotevu wa mbegu.
Aidha uvunaji ufanyike wakati hakuna upepo wala jua kali. Baada ya kukata mashina yafunge katika mizigo midogo na kuweka katika vyombo vya kusafirisha kama vile mikokoteni, matela au magari hadi sehemu ya kukaushia. Panga mizigo midogo kwa kusimamisha katika malundo madogo yasiyozidi mizigo minane kwenye sehemu safi za kukaushia.
KUKAUSHA.
Mapodo ya ufuta hukaushwa yakiwa yamefungwa katika vitita. Vitita huwekwa kwa kuegeshwa kwenye fremu ya kukaushia kwa muda wa wiki mbili hadi tatu kutegemea hali ya hewa. Fremu hii huwekwa juu ya turubai au sakafu ili kuzuia upotevu wa punje kutokana na kupasuka kwa mapodo.
KUPURA.
Upuraji hufanyika kwenye turubai, mkeka au kwenye sakafu safi.Vitita hupigwa taratibu kwa kutumia mti au hutikiswa vikiwa vimegeuzwa vichwa chini ili kuruhusu punje za ufuta kudondoka kwenye sakafu safi au turubai.
KUPEPETA NA KUPEMBUA.
Kupepeta na kupembua hufanywa ili kuondoa takataka kama vile mawe, vipande vya mapodo,vijiti na vumbi.Njia bora ya kupepeta na kupembua ni kwa kutumia mikono.
Ufuta huwekwa kwenye vyombo kama vile ungo kwa kiasi cha kilo mbili hadi tatu. Ufuta hurushwa hewani kwa kasi ndogo na takataka nyepesi huchukuliwa na upepo. 
KUFUNGASHA.
Mbegu za ufuta zilizo safi huwekwa kwenye vifungashio kama vile magunia madogo ya aina ya juti ya ujazo wa kilo 50. Fungasha mbegu za ufuta kwenye magunia yenye uzito usiozidi kilo 50. Kabla ya kufungasha hakikisha mbegu zimekauka hadi kufikia unyevu wa asilimia 10.
KUHIFADHI.
Panga magunia ya ufuta juu ya chaga. Panga kwa kupishanisha ili kuruhusu mzunguko wa hewa kati ya magunia na magunia yako tiyari kupeleka sokoni.
GHARAMA ZA UZALISHAJI NA FAIDA KWA HEKA.
Gharama za uzalishaji mara nyingi hutegemea na eneo husika.
Kwa mfano mchanganuo ufuatao unaonyesha faida ya kilimo cha ufuta kwa maeneo ya Mbeya hususani maeneo ya Chunya. Gharama hizo zinaweza kupungua au kuongezeka na kutokana na msimu husika au eneo kama nilivyotangulia kusema awali.

1. Kuandaa shamba 70,000
2.  Kulima 30,000
3.  Kupanda 20,000
4.  Mbolea 100,000
5.  Kupalilia 30,000
6.  Kuvuna 50,000
7.  Usafiri 50,000
8.  Gharama zingine 50,000
9.  Jumla 400,000
10. Mapato (Forecasts) gunia 10*50kg*3000 1,500,000
11. Faida 1,100,000
SOKO LA UFUTA.
Soko la ufuta kwa Tanzania ni mara tatu zaidi ya uzalishaji wake. Kuna makampuni mbalimbali Tanzania ya unuzi wa ufuta. Makampuni hayo hununua na kusafirisha nje ya nchi kama India na China. Makampuni hayo ni kama vile OLAM, Export Traders n.k.
Katika msimu ulopita bei ya ufuta kwa kilo ilikuwa sh 3000 ambayo ni sawa na sh 300,000 kwa gunia lenye ujazo wa kilo 100. Kwa maana hiyo uhakika wa soko upo na ni mkubwa sana.
Mchanganuo huu ni matokeo ya kiutafiti wa kibiashara, ambayo jitihada zimefanyika kuifanya iendane na hali ya kiuchumi ya sasa, hivyo haitaathiri au kuathiriwa na tamko la wazi au la kiutendaji wa mabadiliko ya kila siku ya kiuchumi duniani hasa ndani ya soko letu la Tanzania.
Matokeo yoyote utakayoyapata mtumiaji au msomaji yatakayokuathiri moja kwa moja au kimchakato, bila kikomo cha muda maalumu mpaka kuathiri faida iliyopangwa, hatutakua tayari kutupiwa lawama ya aina yoyote ile.
Endelea kujifunza zaidi kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila siku.
Kwa maswali na majibu kuhusu kilimo bora cha kisasa kitakachokutoa kwenye umaskini pamoja na huduma za ufungaji wa hema(Green House) Unaweza kuwasiliana na mtaalamu wetu wa kilimo Ndugu John Mabalaga kwa mawasiliano 0754 282 448.

No comments :

Post a Comment