google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Jul 11, 2016

Huna Haja Ya Kukata Tamaa, Mafanikio Yako Yanaanza Na Kitu Hiki.

No comments :
Kila safari yoyote unayoijua wewe, siku zote huanza na hatua moja. Hatua hiyo hutengeneza hatua ya pili na mwisho wa siku  safari nzima hata iwe ya kilometa nyingi kiasi gani huweza kukamilika.
Kila mradi wowote unaouona upo duniani mwanzo wake ulianza tu na wazo wala si mradi kama hivyo unavyouona. Lakini wazo hilo liliweza kuendelezwa kidogo kidogo na mwisho mradi ule ukaanza.
Kila jengo unaloliona limesimama popote pale, pia mwanzo wake lilianza kwa tofali moja tu. Tofali hilo liliweza kuendelezwa na matofali mengine juu yake mpaka likaja kutokea jengo kubwa kabisa, pengine kufikia ghorofa.
Pia kila kitabu kiliachoandikwa hata kiwe na kurasa nyingi vipi siku zote kilianza kwa neno moja na hatimaye maneno hayo yakaunda sura, mwisho wa siku sura hizo zikaunda kitabu chote kikakamilika.
Kila siku mpya mara nyingi inaanza na nuru ya jua. Hainzi siku tu na mara tukaona mchana. Huwa unaanza mwanga mdogo ambao unaashiria siku mpya nyingine imeanza.

Hiyo haitoshi hata mimi na wewe tulianza kama ‘vimjusi’. Lakini siku hadi siku ‘vimjusi’ vile viliweza kubadilika hatimaye ikatungwa mimba, ambapo baada ya miezi tisa mimi na wewe tukatokea kwenye uso huu wa dunia.
Hivyo ndivyo kila kitu ambavyo huwa kinaanza duniani. Hakuna kitu ambacho kilitokea tu na kuwa hivyo kama kilivyo. Ni lazima kilianzia mwanzo fulani, mwanzo huo na siku zote huwa ni mdogo. Na hii ndiyo kanuni ambayo haiwezi kuvunjwa na kitu chochote.
Inawezekana unasoma makala hii upo kwenye maisha magumu na umekata tamaa kabisa na huoni tumaini la mafanikio. Lakini ninachotaka kukwambia huna haja ya kukata tamaa, kwani kila mafanikio unayoyatafuta huwa yanaanza hatua kwa hatua, tena wakati mwingine hatua ndogo kabisa.
Kama kuna kitu ulitaka kukifanya, kifanye na kukifanikisha acha kujidharau kuwa hakiwezi kuleta mabadiliko kwako hiyo si kweli. Kama umeamua kufanya biashara fulani fanya na siyo lazima uanze na mtaji mkubwa kama unavyofikiri, anza kidogo na hicho ulichonacho, mwisho wa siku kitakuwa kikubwa na utafanikiwa.
Mabadiliko yote unayoyataka huwa yanaanza hatua kwa hatua. Na ukumbuke kwamba huwezi kufanikisha kitu katika maisha yako kama usipoanza hatua moja kwanza. Hiki ni kitu cha msingi sana katika mafanikio yoyote na ni lazima ukipitie. Vinginevyo kama utajidanganya ipo njia ya mkato hutofanikiwa.
Hilo unaweza ukaliona vizuri kwenye hatua za ukuaji wa mtoto. Bila shaka kila mtoto unajua ni lazima atambae ndipo atembee na mwisho kukimbia. Hakuna mtoto aliyezaliwa na kuanza kutembea. Huwa zipo hatua za lazima ambazo kwake ni lazima azipitie ili kukamilisha ukuaji wake.
Hivyo ndivyo ilivyo kwenye mafanikio, siku zote hakuna mafanikio ya mkato wala ya haraka. Mafanikio ni mchakato unaenda hatua kwa hatua. Ndiyo maana watu wengi ambao huwa wakitafuta mafanikio ya mkato hujikuta mara nyingi wakiishia pabaya sana kuliko walivyokuwa mwanzo.
Hiyo yote inatuonyesha huwezi kuvunja kanuni za  mafanikio hata iweje. Ni lazima hatua zifuatwe. Kwa hiyo hata hali yako iwe mbaya vipi kiuchumi uwezo wa kubadilisha maisha yako unao. Kikubwa jipe muda wa kubadilisha maisha yako hatua kwa hatua na kila kitu kitabadilika mpaka utashangaa.
Kumbuka hakuna lisilowezekana. Amua kuwa utachukua hatua hata kama ni ndogo vipi lakini zinakupeleka kule kwenye lengo lako. Kama nilivyoanza makala hii kila kitu huwa kinaanza kidogo kidogo, hata maisha yako yanakwenda kubadilika ikiwa utachukua hatua hizo ndogo na kuacha kusubiri tena. Ni bora ukasonga mbele ukiwa unatambaa kuliko ukawa umekaa unasubri.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kuboresha maisha yako na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.







No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.