Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, July 4, 2016

Mambo Manne (4) Yanayofanya Maisha Yako Kuwa Bora Wakati Wote.

No comments :
Wengi wetu katika maisha, tunapenda sana kuwa na maisha bora. Hakuna hata mmoja ambaye anapenda maisha yake yawe hovyo. Kila mmoja wetu hujitahidi kwa kadri anavyoweza ili kufanya maisha yawe bora na thamani kubwa.
Lakini hata hivyo wengi bado huwa hawajui mambo ambayo wanatakiwa kuyafanya ili kufanya maisha yao kuwa bora. Kwa sababu hiyo wengi hujikuta wakifanya hata mambo yasiyowasaidia kufanya maisha yawe bora, zaidi ya kuwarudisha nyuma.
Ni kusudio la makala haya likusaidie kutambua mambo unayotakiwa kuyazingatia ili kufanya maisha yako kuwa bora kila siku. Kwa kujifunza mambo hayo itakusaidia kubadilika wewe na hata wale wanaokuzunguka siku hadi siku.
Yafuatayo Ni Mambo Manne (4) Yanayofanya Maisha Yako Kuwa Bora Wakati Wote.
1. Thamani.
Unaweza kuwa ni ukweli unaouma lakini huo ndio uhalisia kwamba, huwezi kufanikiwa katika maisha yako kama hutoi thamani inayostahili. Ni lazima utoe thamani ili kupata hicho unachokihitaji. Unaposhindwa kufanya hivyo lazima maisha yako yatakwama tu.
Mara nyingi tumekuwa tukiambiwa tunavuna tulichopanda. Ndiyo, huo ndio ukweli. Huwezi kuvuna mafanikio makubwa kama thamani unayotoa ni kidogo au haiendani na mafanikio hayo unayoyataka. Kama hutoi thamani inayostahili tambua kabisa mafanikio yako yatakuwa kidogo sana.

Hivyo, ni jukumu lako wewe kuongeza thamani katika maisha yako katika kila eneo ambalo unaona haupo vizuri. Kwa mfano kama unaona huna maarifa ya kutosha katika jambo fulani, ongeza maarifa hayo na kujiboresha kila siku kwa kujisomea vitabu. Hapo utafanikiwa na kujenga maisha bora unayoyataka.
2. Marafiki wazuri.
Kujijengea marafiki wazuri ambao wanakupa nguvu na hamasa katika safari ya mafanikio, ni jambo ambalo lipo wazi lazima lifanye maisha yako kuwa bora na thamani. Marafiki ni chachu kubwa sana ya mafanikio ikiwa utawatumia vizuri.
Ogopa sana kuwa na marafiki hasi, wakatisha tamaa na ambao watakufanya kila wakati ujisikie vibaya. Jifunze kutafuta ‘timu’ nzuri ya marafiki itakayokufikisha juu kwenye kilele cha mafanikio. Marafiki hao watakusaidia kushirikiana katika mipango mizuri na kufanya maisha yako kuwa bora.
3. Familia bora.
Maisha bora lazima yahusishe familia bora. Familia hii bora unatakiwa kujijenga wewe. Huwezi kujidai ukasema eti maisha yako ni bora wakati familia yako iinateseka. Ni lazima uhakikishe familia yako iko salama na inapata mahitaji yote muhimu kwanza.
Ukiwa kama baba wa familia ni muhimu kulijua hili na kulifanyia kazi. Migogoro ya hapa na pale ni lazima kuachana nayo ili kujenga familia bora. Furahia maisha na watoto wako, furahia maisha na mke wako hapo utakuwa unajijengea maisha bora ambayo kila mtu atayatamani.
4. Maisha ya kiroho.
Ni muhimu sana kuishi maisha ya kiroho ili kufanikiwa. Ni lazima utambue uwepo na HOFU ya Mungu ili kufanikiwa. Huu utakuwa ni msingi bora na muhimu sana kwako na kizazi chako kijacho katika kutengeneza maisha bora ya kila siku.
Kwa kuzingatia thamani unayotoa, marafiki wazuri wanaokuzunguka, kujenga familia bora na kuishi maisha ya kiroho ni lazima utaishi maisha bora na utaiona dunia ni moja ya sehemu safi na salama sana kwako.
Nikutakie siku njema na endelea kuwaalika wengine waweze kujifunza kupitia mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kila siku.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki, Imani Ngwangwalu.
MUHIMU; Tunatambua umuhimu wako mpenzi msomaji wa makala haya, hivyo tunaomba maoni/ushauri wako kwani tunahitaji kufanya marekebisho ya mtandao wetu wa Dira ya Mafanikio ili uwe bora zaidi. Tuambie ni nini unataka tuongeze au tupunguze. 
Tuma maoni yako kwenda namba 0757909942/0713048035 au dirayamafanikio@gmail.comNo comments :

Post a Comment