google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Dec 31, 2017

HEKIMA ZA MAISHA NA MAFANIKIO; Usijitupe Kwenye Moto Kwa Sababu Ya Kuogopa Moshi.

No comments :
Ni wakati na siku njema tena , na kukaribisha katika siku ya leo katika jukwaaa letu la hekima za maisha na mafanikio. Kama siku zote ambavyo nimekuwa nikikukumbusha, hekima za maisha na mafanikio ni sehemu ya kujifunza busara na hekima za maisha.
Hilo linakujaje au kivipi? Ni rahisi tu, ni kupitia misemo au maneno ambayo yaliweza kuzungumzwa na babu zetu enzi za kale. Kwa kujifunza huko nasi tunatoka na vitu ambavyo ni adimu lakini, vinatukomaza na kutufanya tupige hatua.
Naomba nikukaribishe jamvini, vua viatu vyako hapo ulipo, karibu kwenye mkeka wangu hapa nilipo, ili nikukaribishe kwa moyo mkunjufu na tuweze kujiunga pamoja tufunzane juu ya hekima za maisha na mafanikio za siku hii ya leo.

Hekima ya 1; Anaye elewa vibaya ni yule anayesikiliza vibaya.
Kuna watu ambao unaweza ukasema jambo na ukarudia tena na tena huku wao kazi yao ikiwa ni kuitika tu mara mbilimbili. Katika hekima yetu hii, inatuonyesha kwamba anayelewa vibaya ni yule ambaye anasikiliza vibaya pia.
Hii ikiwa na maana kama wewe ni msikilizaji mzuri, ni lazima na kwako utaweza kulewa vizuri kile ambacho kimesemwa. Ikiwa lakini utaenda kinyume, basi ni lazima kwako utakuwa unaelewa vibaya kila wakati.
Hekima yetu inatukumbusha umuhimu wa kutega masikio vizuri pale jambo linaposemwa na mtu mwingine. Ni vyema kuachana karibu na kila kitu na kujenga usikivu mkuu ili kusikiliza vizuri ili kuepuka kulewa vibaya.
Hekima ya 2; Usijitupe kwenye moto kwa sababu ya kuogopa moshi.
Hii pia ni moja ya hekima ya maisha na mafanikio iliyotolewa na wahenga wa kale ambayo inakutaka sana na kukusihi usije ukajitupa kwenye moto kisa na sababu kubwa ni kwa wewe kuogopa moshi.
Hekima hii ukiiangalia ina chekesha kidogo, lakini ujiulize ina maana gani kwetu? au inafunzo gani kwetu ambalo ni kubwa? Hapa ukichunguza tunaonywa kwamba usije ukajiingiza kwenye matatizo makubwa sana kwa sababu ya kitu kidogo tu.
Hekima hii inawaonya watu wale ambao wakipata tatizo wanakimbilia kujidhuru, ambapo madhara yake yanakuwa makubwa kuliko hata ya tatizo lenyewe, hivyo inakuwa ni sawa na kujirusha kwenye moto kwa sababu ya kukwepa moshi.
3. Imara ya jembe kaingoje shamba.
Siku zote inaeleweka hivi, iwapo jembe ni imara hujulikana pale linapolima shambani. Hiyo ikiwa na maana, udhaifu wa mtu au kitu, huthibitika sana pale mtu au kitu hicho kinapokuwa kazini na si vinginevyo.
Hapa tahadhari kubwa tunayopewa na maneno haya ya hekima ni kwamba, tusikithamini sana kitu kwa sababu ya maneno au kujidai kwake, thamamini kitu au mtu kwa sababu ya kazi, au uwezo wake.
Kuna watu kwa sababu ya tabia au huluka zao, hujikuta ni watu wa kujidai sana na kutoa kila tambo za maneno kwamba wanaweza kitu fulani, lakini kumbe kiutendaji hakuna kitu. Hapa unatakiwa kuwa makini na kuangalia uimara wao kwenye kazi na si maneno peke yake.
4. Heri kupata mkate nusu kuliko kutokupata kabisa.
Funzo kubwa tunalolipata kupitia hekima hii ya maisha ya mafanikio ni kwamba, kile kidogo ulichonacho ni bora na ni nafuu sana kuliko kukosa kabisa. Huhitaji kukiona ni duni sana wakati unacho, unatakiwa kushukuru hata kwa hicho kwani kitakusaidia.
Wapo watu ambao wao ni kunung’unika tu, wakati ukiwaangalia kuna kitu ambacho wamekipata. Hapa maneno ya busara kutokana na hekima za maisha na mafanikio yanatuonya tuachane mara moja na tabia hii, inatuaangamiza.
Kama kuna kitu kidogo umepata basi kaa chini shukuru na kisha ongeza juhudi itakayokusaidia kuweza kupata kitu kingine zaidi na zaidi. Elewa nusu ya mkate uliyoipata ni bora zaidi kuliko kuikosa kabisa.
Nikutakie siku njema na kila la kheri katika kujifunza hekima hizi, kwa leo tunaishia hapa, naomba uwe na wakati mwema zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,

No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.