Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, May 19, 2016

Kupinduana Kwenye Ndoa Hutokea Sana.

No comments :
Unapoishi nyumbani na ndugu yako, jamaa yako na hata mtumishi wa kike, ni vizuri ukajitahidi kulinda ndoa yako. Kumbuka kwamba, wanaume hawajali sana hisia, bali hujali zaidi mwili. Kama ukimwachia jamaa yako, ndugu yako au rafiki yako kumzoea sana mumeo, jua tu kwamba, inawezekana unajitengenezea maumivu makubwa sana hapo baadae.
Tafiti zinathibitisha sasa kwamba, mwanamume anapohisi kuwa mwanamke fulani anamwonesha kwamba, yeye ni mwanaume kwelikweli, anapoonesha kwamba, anatambua uwepo wake na mchango wake katika familia, mwanaume huanza kumpenda, bila kujali sura au hadhi.
Kama ndugu yako ni mjuaji wa mambo haya, anaweza kumwonyesha mumeo kwamba, anaamini kuwa ni mwanamume kwelikweli. Hii hufanyika kwa kumsifu, kutokupingana naye, kumpongeza mara kwa mara na kumwosha kwamba, anaamini katika yeye.
Hata wale watumishi wa ndani, wanaochukuliwa na wanaume za watu hawafanyi hivyo kwa sababu, ati hao watumishi ni wazuri sana wa sura au wanajua sana mapenzi, hapana.

Kuwa makini na ndoa yako.
Wanaume huwachukua kwa sababu, wake au wapenzi wa wanaume hao, wameshindwa wajibu wao, wameshindwa kujua kwamba, wanaume hutazama uhusiano kwa jicho tofauti.
Lakini, iwe ndugu zetu au jamaa zetu na hata watumishi majumbani mwetu, bado na wao ni binadamu, wana udhaifu. Kwa udhaifu wao, pamoja na udhaifu wa wanaume au wapenzi wetu, wanaweza kutusaliti. Kwa hiyo ni juu yetu kulinda ndoa zetu, ili udhaifu huo usiwe chanzo cha kuvunjika kwa matumaini na matarajio yetu ya kujenga familia.
Kuna mambo mawili makubwa hapa. Kwanza, inawezekana tumejiachia sana kama wanawake na kusahau kuwa wanaume huvutiwa na mambo gani. Kwa hali hiyo, tunawaacha wale waliokaribu nao kuwafanyia yale wanayohitaji na kuchukua nafasi zetu..
Lakini pili, ni udhaifu wa kibinadamu na zaidi kwa wanaume, linapokuja suala la mwili. Kwa udhaifu huo, inabidi tuwasaidie kuwalinda ili wasishawishiwe kiurahisi. Lakini, ndugu zetu wa kike au watumishi tunaoishi nao, inabidi tuwakague vizuri na kuacha kuwaamini kupita kiasi kwa wanaume au wapenzi wetu.
Ni hatari sana kwa mwanamke kwa mfano, kumwambia au kumruhusu mumewe aende sehemu za starehe na rafiki yake wa kike au na ndugu yake wa kike, ati kwa sababu anamwamini rafiki huyo au mumewe. Kumbuka, suala hapa siyo kuaminika, bali ukweli wa kiimaumbile pia. Chunga ndoa yako, ilinde sana, kwani siyo dhambi kufanya hivyo.
Nakutakia siku njema na Baraka katika ndoa yako.
Makala hii imeandaliwa na Devotha Kauki. Unaweza kuwasiliana na mwandishi kwa dvkauki@gmail.com
No comments :

Post a Comment