Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, May 9, 2016

Kama Unafanyia Kazi Mambo Haya Kila Wakati, Hakuna Wa Kukuzuia Kufanikiwa.

No comments :
Ili kupata mafanikio siku zote unahitaji kuwa makini sana na kuzingatia mambo yanayoleta mafanikio. Bila kuwa makini na mambo hayo, suala la kupata mafanikio kwako linaweza likawa ni ndoto au hadithi kabisa, tena hadithi isiyo na mwisho. Wengi kwa kutokujua wanashindwa kupata mafanikio kwa sababu ya kuupuza au kushindwa kufanyia kazi mambo yanayosababisha mafanikio kutokea kwao.
Naamini kama wewe ni msomaji wa dira ya mafanikio umekuwa ukijifunza mbinu nyingi kila wakati za kukusaidia kufanikiwa. Katika makala yetu ya leo, tutakwenda kukumbushana mbinu au mambo muhimu ambayo unatakiwa kuyafanyia kazi kila wakati ili kufanikiwa. Ni mambo ambayo wengi wanayajua, lakini wamekuwa wakiyapuuza pengine kwa kutokujua. Bila kukupotezea muda, fuatana nami katika makala haya tujifunze pamoja.
 1. Kujiwekea vipaumbele.
Haijalishi una malengo na mipango mizuri vipi. Kitu cha msingi ili uweze kutimiza malengo yako ni kwa wewe kuwa na vipaumbele ambavyo umejiwekea ili kutumiza malengo uliyojiwekea. Ni lazima na muhimu sana kujua mambo ambayo unatakiwa kuyapa vipaumbele. Si kila jambo una uwezo wa kulifanya kwa uzito ule ule. Usipoweka  vipaumbele ni rahisi kushindwa ama naweza kusema hutaweza kufanikiwa kabisa.
Ikiwa hujanielewa vizuri hapa kwenye kujiwekea vipaumbele ngoja nikupe mfano. Tuchukulie una malengo ya aina tatu yaani unataka kufungua duka, kufuga kuku na wakati huohuo unataka kulima vitunguu kwa sababu umesikia kuna sehemu vinalipa sana. Sasa kwa malengo yako hayo yote matatu ili yaweze kutimia na kutekelezeka kwa uhakika ni lazima uchague lengo moja tu utakalo toa nguvu zako zote hadi kulifanikisha.
Tatizo la baadhi ya watu iwe kwa kujua au kijifanya wajuaji huwa wanataka kukamilisha mambo mengi sana kwa pamoja, kitu  ambacho baadae huwashinda tena. Jiulize una vipaumbele vipi ambavyo unataka kuvitimiza. Usipoweka vipaumbele na ukajifanya una tamaa, Ooooh! utaishia kugusa gusa mambo na hakuna makubwa utakayofanikisha. Kama unataka kufanikiwa tambua unatakiwa kuweka vipaumbele na si vinginevyo.

Jiwekee vipaumbele kila wakati.
2. Kufanya maboresho.
Kila kitu katika hii dunia kina badilika tena kwa kasi sana. Hata wewe hapo ulipo kuna mabadiliko yanayotokea ndani yako ya kimwili na akili uwe unataka au hutaki. Kwa kuwa dunia ina badilika  hivyo unalazimika na wewe kubadilika vivyo hivyo. Kama upo kwenye dunia hii ya mabadiliko na hutaki kubadilika kitu kimojawapo kitakachokukuta ni lazima utaachwa nyuma sana. Kwa kifupi utashangaa hufanikiwi na kushuhudia wengine wakifanikiwa tena kwa kasi.
Sasa kitu unachotakiwa kufanya ili uendane na madiliko kasi ya dunia ili usije ukadumaa na kuachwa kimafanikio ni lazima kila wakati kufanya maboresho kwenye maisha yako. Ni lazima kuboresha kila eneo lililo la muhimu sana kwako katika maisha yako. Yapo maeneo mengi ambayo ni lazima kuyafanyia maboresho kama kuwa na mahusiano bora na wengine, afya, kujisomea mambo ya mafanikio na mengineyo mengi ambayo yana msaada kwetu mkubwa.
Kumbuka bila kuwa na lengo la kuwa bora kila siku kufanikiwa itakuwa ni ngumu sana. Je, unataka kujua hiyo yote inatokana na nini? Ni kwa sababu utakuwa unaishi kimazoesa sana na kusahau kwamba mabadiliko na kuboresha maisha yako kila siku kuna hitajika. Kama unataka kuboresha eneo la afya fanya hivyo kila siku kwa kufuata kanuni za afya. Kama unataka kuwa na mafanikio jifunze kila siku mafanikio kupitia vitabu au semina. Ukifanya mabadiliko au ‘improvement’ kila siku, mafanikio utayapata.
3. Kuweka kumbukumbu.
Kwa chohote unachokifanya kiwekee kumbukumbu. Kama kuna jambo unataka kulifanya kesho au wiki lijalo weka kumbukumbu. Unapoweka kumbukumbu inakusaidia sana kuiamsha akili yako kulazimisha utekelezaji kuliko ungeacha hivi hivi. Hili ni moja kati ya jambo rahisi ambalo wengi hawalifanyi lakini katika maisha ya malengo ni muhimu sana. Najua kwa wale wanaofanya hivi wananielewa kitu ambacho ninakisema hapa kwa vizuri sana.
Siku zote malengo au kitu ambacho hakipo kwenye maandishi huwa hakina maana sana. kwa hiyo, ili uweze kufanikiwa na kujihakikishia ushindi wa malengo yako. Anza kujiwekea kumbukumbu kila siku kwa unachokifanya au unataka kukifanya. Na kila inapofika jioni jikumbushie kwa kupitia kijitabu chako cha kumbukumbu. Kwa jinsi utakavyoendelea hivyo, utajikuta ukibadilisha maisha yako kwa sehemu kubwa sana, hiyo nikiwa na maana utaishi kitaalamu na kisomi zaidi.
Kama utazingatia mambo hayo matatu na kuyafanyia kazi kama nilivyotangulia kusema hapo awali uwe na uhakika utafanikiwa na hakutakuwa na mtu wa kukuzia.
Tunakutakia siku njema na ansante sana kwa kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa ajili ya kujifunza.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.
Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713048035,

No comments :

Post a Comment