Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, May 18, 2016

Kweli Nne (4) Kuhusu Mafanikio, Ambazo Hutakiwi Kuzisahau.

No comments :
Ili uweze kufanikiwa ni lazima uzijue kweli zenye uwezo wa kukupa mafanikio. Haijalishi unafanya nini, ukizijua kweli, kanuni au mbinu zinazotoa mafanikio ni lazima ufanikiwe. Hivyo haitajalisha una historia gani au unatoka katika taifa ama familia gani kufanikiwa kwako kutakuwa ni lazima ukielewa kweli au kanuni hizo. Mara nyingi watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwa sababu ya kushindwa kuzijua kweli hizo.
Sipendi uwe miongoni mwao ukashindwa kufanikiwa kwa sababu ya kutokujua mafanikio yanataka nini. Kwa kusoma makala haya, nitakushirikisha kweli ambazo unatakiwa kuzijua ili uweze kufanikiwa. Ni kweli ambazo zinatumiwa na wengi ikiwemo mpaka na watu wenye mafanikio makubwa. Hakuna ubishi ukijua kweli hizi na kuzifanyia kazi, nafasi ya kufanikiwa kwako itakuwa ni kubwa. Je, kweli hizo ni zipi?
1. Maisha yako yanakutegemea kwa asilimia zote.
Ukitaka kufanikiwa kwa viwango vikubwa, elewa kabisa kwamba maisha yako yanakutegemea wewe kwa asilimia zote. Acha kutegemea kitu au chochote kilicho nje ya maisha yako, wewe ndiye unayewajibika katika maisha yako kwa asilimia zote. Hata inapotokea pengine umekosea acha kusukumia makosa hayo kwa wengine, jifunze kutambua wewe ndiye chanzo.
Kwa kuwa umeshajua maisha yako yanakutegemea wewe, acha kubeba visingizio vinavyokuzuia kufanikiwa. Sahau juu ya habari ya wazazi wako eti kwamba ooh hawakuweza kukusomesha, sahau kila kitu. Wajibu wa maisha yako, unao wewe. Tenda kazi zako kwa nguvu zote huku ukiamini mtu pekee wa kubadilisha maisha yako ni wewe. Huu ni ukweli ambao kamwe hupaswi kuusahau kwenye maisha ya mafanikio.

Wewe ni mshindi.
2. Mawazo yako ni kila kitu.
Mawazo uliyonayo ndiyo yanayaoamua maisha yako yawe vipi. Upo hapo kimaisha ni kwa sababu ya mawazo ambayo ulikuwa nayo siku za nyuma. Kwa hiyo, sisi ni matokeo ya fikra au mawazo tuliyonayo. Mawazo yetu ndiyo yaliyotufikisha hapa na sio kitu kingine. Hivyo kwa kujua hili ni muhimu sana kuwa makini na kile unachokiwaza kwa sababu utakivuna, haijalishi kiwe kibaya au kizuri.
Kila siku jifunze kufikiri mawazo chanya. Fikiria yale mambo ambayo unataka yakutokee. Acha kufikiria yale usiyataka utayapata. Mawazo yako hayatakudanganya, utavuna kile unachofikiria. Kumbuka kama nilivyoanza kwa kusema, upo hivyo kwa sababu ya mawazo uliyonayo. Kwa kulijua hili, itakusaidia kuwa makini na kile unachokiwaza.
3. Una uwezo mkubwa wa kupata chochote, ukiamua.
Kweli nyingine ambayo hutakiwi kuisahau katika maisha yako ni kwamba, una uwezo wa kupata chochote ikiwa utaamua. Kama utaamua kuwa na mafanikio makubwa, utayapata. Kama utaamua kuwa mwanamziki, mwandishi au kitu kingine chochote, unauwezo wa kukipata pia. Kitu cha msingi ili kukipata hicho unachokitaka ni lazima ujitoe kwanza.
Hakuna ajali kwenye mafanikio. Upo hivyo pia kwa sababu ya maamuzi yako uliyoyafanya. Kama kuna kitu chochote unachokitaka, fanya maamuzi  na kisha chukua hatua. Uwezo wa kufanikisha chochote katika maisha yako, unao.
4. Una nguvu kubwa zilizo ndani yako.
Fanya kazi kwa ubora na juhudi zako zote huku ukiamini nguvu kubwa ambazo unazo ndani yako. Unao uwezo mkubwa wa kufanikisha jambo lolote ulio ndani yako. Lakini kwa bahati wengi wetu ni watu wa kutumia nguvu zilizo chini ya viwango vyetu. Ukijua uwezo ulionao na ukaamua kuutumia, utafanikiwa sana. Huu ni moja ya ukweli unaotakiwa kuujua kuhusu mafanikio na kukubali kutumia.
Utafika kwenye mafanikio makubwa ikiwa utaamua kuzitumia kweli hizo, kukusaidia kufanikiwa.
Tunakutakia siku njema na endelea kujifunza kupitia mtandao wako wa DIRA YA MAFANIKIO kila siku.
Ni wako rafiki,

Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713048035,No comments :

Post a Comment