Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, June 24, 2016

Aina Tatu Za Mawazo Zinazokufanya Ushindwe Au Ufanikiwe.

No comments :
Kiasili binadamu tumepewa uwezo mkubwa wa kufikiri ukitofautisha na wanyama wengine. Uwezo huu tulionao huwa unakuja hasa kutokana na matumizi ya mawazo au kufikiri kwetu. Kufikiri huko ambapo tunafanya kila siku na kila wakati ndipo kunapotufanya tuwe na maisha ya aina fulani, haijalishi yawe ya mafanikio au kushindwa.
Lakini hata hivyo wengi wetu huwa tunafikiri au tuna mawazo ya kimazoea na kushindwa kutambua kwamba hayo mawazo yetu pia yamegawanyika. Kwa mawazo yoyote uliyonayo mara huwa yamegawanyika katika sehemu. Kwa mfano unapowaza wazo fulani, wazo hilo linakuwa lipo moja kwa moja kwenye sehemu ya kwanza, au ya pili au ya tatu ya mawazo yako.
Kivipi hili linatokea? Fuatana nami katika makala haya kujua aina tatu za mawazo zinazokufanya ushindwe au ufafanikiwe katika maisha yako.
1. Mawazo elekezi.
Haya ni mawazo yanayoleta mafanikio. Kwa lugha nyingine haya ni mawazo chanya. Mawazo yenye uwezo wa kutubalisha na kutufanya tuwe na mawazo bora. Haya ni mawazo yanakufanya uamini unaweza kufanya biashara, unaweza kuwa tajiri au unaweza kuacha chochote.
Kwa kifupi, haya ni mawazo yanayokupa mwongozo wa kufanikiwa. Unapokuwa na mawazo haya kila wakati, elewa kabisa upo kwenye njia sahihi ya kuelekea kwenye mafanikio. Ni mawazo yanayotoa hatma ya kesho yetu itakuwaje.

2. Mawazo ya kuharibu.
Kama huna mawazo chanya au mawazo elekezi ya kukusaidia basi elewa utakuwa na mawazo ya kuharibu. Mawazo haya wakati mwingine yanafahamika kama mawazo hasi. Haya ni mawazo ambayo  kila wakati yanakwambia huwezi kufanikiwa au huwezi kufanya hili.
Haya ni mawazo yanayoua na kuharibu maisha ya wengi. Jaribu kujiuliza utakuwa ni mtu wa aina gani ikiwa kila unalolifanya unaona kama haliwezi kufanikiwa? Ukiwa na mawazo haya, tambua una mawazo ya kuharibu ambayo hayawezi kukusaidia kwa chochote.
3. Mawazo ya hovyo.
Unapokuwa na mawazo haya mara nyingi yanakuungoza katika vitu kama kupoteza muda au kufanya mambo yasiyo na faida. Utakuta badala ya kukaa chini na kufanya mambo ambayo yanaweza yakakusaidia kufanikiwa, badala yake unajikuta unafanya mambo ambayo hayana msaada kama kupiga soga na marafiki.
Kumbuka, aina hizi za mawazo ndizo zinazokufanya ufanikiwe au ushindwe katika jambo unalolifanya. Jambo kubwa kwako la kujiuliza je, ni aina gani ya mawazo uliyonayo ambayo inakutawala sana? Kwa aina hiyo ya mawazo uliyonayo ndiyo itakayoamua maisha yako yaweje.
Nikutakie siku njema na endelea kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila siku. Hakikisha pia usikose kuwashirikisha wengine waendelee kujifunza kupitia mtandao wako huu. 
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com

No comments :

Post a Comment