Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, June 13, 2016

Sifa Nne Zitakazokusaidia Kuziona Fursa Zinazokuzunguka.

No comments :
Pata taarifa sahihi za kukuwezesha kuziona fursa.
FURSA ni habari yeyote nzuri au mbaya inayoweza kumpelekea mtu kuona njia sahihi ya kumpatia mafanikio ayatakayo katika maisha yake. Tunasema ni habari nzuri au mbaya kwa sababu si taarifa zote mbaya ni kweli 100% ni mbaya na hizo nzuri pia zinachangamoto na mitihani yake.

Fursa Mara nyingi huonekana kwa watu wenye jicho la tatu japokuwa huwapitia wengi machoni mwao na wengine huzishika na kuziachia. Watu wengi katika hii dunia kwa tafiti za kisaikolojia ni matajiri na wana uwezo MKUBWA sana ndani yao. Ila hawajijui. Uwezo wa binadamu kwa wastani imegundulika kuwa binadamu wengi hutumia 1/3 ya ubongo wao katika kufikiri na kutenda mambo yake. 

Imebainika kuwa kuna kundi dogo sana la watu ambao hutumia robo ya ubongo wao katika kufikiri na kutenda majambo yao na hao ndio pekee tunaowaita matajiri na wakati mwingine tunawaona ni watu fulani wenye akili na uwezo mkubwa wa kufanya mambo. Hawa ndio watu wenye jicho la tatu la kuweza kuona fursa.

Fursa zipo kila sehemu tatizo ni namna gani ujue kuwa hii ni fursa. Hata hapo ulipo kuna fursa nyingi za mafanikio. Utaniuliza Kisuda mbona mimi sizioni?  Huna jicho la tatu utazionaje fursa? Umevaa miwani ya mbao huku unataka kuangalia mwezi utauona?  Mpaka uwe na jicho la tatu ndipo utaziona fursa. Vinginevyo mafanikio utayasikia kwa jirani tu. Utaishia kushika pesa lakini unaishi maisha ya dhiki,utapata biashara nzuri au kazi nzuri kisha utaingia tamaa na  kutamani biashara au kazi nyingine.

Zinapatikana wapi na zibaonekanaje fursa za mafanikio na kuelewa wazi hii ndio fursa ya mafanikio katika maisha yangu? Kisaikolojia kila kitu unacho kitaka katika maisha yako kinaanzia ndani mwako kwanza. Ukitaka mafanikio lazima uanze kuifundisha akili yako,mwili wako na nafsi yako kubeba viashiria vya kile unachokitaka au kukitamani katika maisha yako.

Kwa maana hiyo ili mtu yeyote aweze kufanikiwa na kuziona fursa za mafanikio lazima awe na sifa kuu nne.
 
Sifa ya kwanza kwa watu wenye kuziona fursa ni uaminifu. Kamwe huwezi kuiona fursa ya mafanikio kama wewe si mwaminifu. Uaminifu huvutia fursa na watu wengi kuja kwako na kuanzisha miradi au biashara kubwa hata bila ya wewe kuwa na mtaji( msingi) Uaminifu ndio siri ya kuziona fursa za mafanikio kwa macho yako.

Sifa ya pili ya watu wenye kuiona fursa ni kuwa na marafiki bora.Ukitaka kuziona fursa za mafanikio badili marafiki zako tafuta marafiki wapya lakini kwa kuchagua walio bora kwa maana ya kuwa na fikra chanya,wenye uchu na maendeleo na wanaojitambua katika safari ya mafanikio. Marafiki wakatisha tamaa na wenye wivu wa maendeleo weka pembeni. 

Utaniambia baada ya miezi sita tu kweli Kisuda ulisema nimebadili marafiki nikapata kuona fursa za mafanikio katika maisha yangu na leo masha Allah namiliki mradi wangu wa kuku wa nyama na mbogamboga. Marafiki wanamchango mkubwa katika maisha yako.

Uchaguzi ni wako kubaki na marafiki walewale wenye mawazo hasi kila siku kukaa kijiweni kujadili maisha ya watu au kulaumu bajeti ya serikali. Ama ubaki na rafiki yako kila siku kiguu na njia kukuletea umbea kibarazani. Shoga nikuambieeeee! ? Mhhhh wajua Jana usiku nimemwona yule mkaka ametoka na yule mdada wanaelekea mjini. Hayo mambo ya kuchunga watu washapitwa na wakati chunga maisha yako usijechekwa na wajukuu zako shauri yako, Kisuda mie simo.

Sifa ya tatu ya watu wenye jicho la tatu la kuona fursa wana hofu ya Mungu. Hili huwa napenda sana kulisema kama huna hofu ya Mungu ndani yako mafanikio ni magumu kupatikana. Kwa sababu huta kuwa na Imani thabiti katika mitihani na changamoto utakazo kutana nazo utakata tamaa na kuvunjika moyo.

Sio hivyo tu hata utaweza kutenda haki na kuwahurumia wengine. Hutadhulumu cha mwenzio na utaheshimu utu wako. Ukikosa hofu ya Mungu ni rahisi kudhulumu na ndio mwanzo wa kukosa fursa nyingine nzuri ambazo zingekuja kupitia Njia hiyo ya kuwa na Hofu ya Mungu.

Sifa ya nne ni  kuwa wana vyombo sahihi vya kupata taarifa sahihi na kwa wakati sahihi. Katika hali ya kawaida ili mtu afanikiwe ni lazima upate taarifa sahihi kutoka vyombo sahihi na kwa wakati sahihi . Hili haliepukiki kwa namna yeyote ile. Mafanikio ya kupata fursa za mafanikio lazima kuwepo na usahihi katika taarifa, vyombo na muda au wakati.

Kinyume chake ni kukosa fursa ya mafanikio. Vyombo sahihi ni kama vile vitabu,marafiki waaminifu na makini,wakufunzi, wajasiriamali waaminifu na washauri wenye ujuzi. Je wewe unazo sifa ngapi katika kuziona fursa za mafanikio?

CHUKUA HATUA ZINDUKA AMKA KUTOKA USINGIZINI MAFANIKIO NI HAKI YAKO.

Imeandikwa na mtaalamu wa saikolojia na mbinu za mafanikio katika maisha.

Shariff H. Kisuda alimaarufu Mzee wa nyundo 0715079993


No comments :

Post a Comment