Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, June 27, 2016

Mambo Muhimu Ya Kukumbuka Kama Unataka Kuwa Mjasiriamali Mwenye Mafanikio.

No comments :
Kila kitu katika maisha ya binadamu kinaanza kama wazo. Haijalishi kitu hicho kimeleta mafanikio au la, lakini mwanzo wake huwa unaanzia kwenye wazo analokuwa nalo mtu.
Kumbuka  siku zote, mawazo yako ndiyo yanayokufanya uwe na maamuzi ya aina fulani. Maamuzi hayo pia ndiyo yanakufanya uwe na matendo ya aina fulani. Na matendo hayo ndiyo yanayotoa matokeo ya kile ukifanyacho.
Kwa hiyo, ikiwa unataka kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio, kitu cha kwanza unachotakiwa kuwa nacho ni mawazo sahihi. Unapokuwa na mawazo sahihi yatakusaidia kufanya maamuzi na matendo sahihi.
Hivyo, mafanikio utayaona kwa sababu maamuzi na matendo yako yatakuwa sawa kukusaidia kufanikiwa. Kwa sababu hiyo, ni lazima kukumbuka mambo ya msingi kama unataka kuwa mjasiramali mwenye mafanikio. Kwa vipi?
Yafuatayo  Ndiyo Mambo Muhimu Ya Kukumbuka Kama Unataka Kuwa Mjasiriamali Mwenye Mafanikio.
1. Jifunze kuwajibika.
Mjasiriamali mwenye mafanikio ni yule ambaye anawajibika na kuweka mambo sawa kila wakati na sio kusubiri hali fulani ndizo zimletee mafanikio. Mjasiriamali huyu anakuwa tayari kukabiliana na kila changamoto na kutatua.
Hili ni jambo muhimu sana la kukumbuka na kuweka kwenye akili ikiwa unataka kuwa mjasirimali mwenye mafanikio. Wakati wote usisubiri matokeo ya aina fulani bali pambana mpaka kieleweke.

Jifunze kuwajibika.
2. Jifunze kuwa mbunifu.
Ubunifu ni njia pekee itakayokufanya uwe mjasiriamali wa mafanikio. Hakuna mafanikio kwenye ujasiriamli kama wewe si mbunifu. Karibia kila kitu kinaweza kufa kwako usipochukua hatua za kuwa mbunifu.
Jifunze kufikiri tofauti na wajasiriamali wengine. Kwa mfano kila wakati unaweza ukawa unajiuliza ufanye nini cha ziada ili uongeze idadi ya wateja kwenye biashara yako? hapo ndipo unatakiwa kubuni mambo ya ziada ambayo wengine hawana.
3. Jiamini.
Vipo vikwazo vingi katika safari ya mafanikio. Lakini yote hayo yanapotokea ni wakati wa kujifunza kujiamini wewe mwenyewe na kuamini ndoto zako kuwa unaweza kuzifikia. Hakuna mtu mwingine anayeweza kufanya hivyo zaidi yako. Ni lazima ujue kujiamini kwako ndio msingi mkubwa wa mafanikio.
Wajasiriamali wenye mafanikio wana hulka au tabia ya kujiamini sana. Hicho ndicho kinachowasaidia waweze kufikia viwango vya juu vya mafanikio. Hata wewe kama usipochukua jukumu la kuweza kujiamini hakuna utakachoweza kufanikisha sanasana  utazidi kushindwa.
4. Usikate tamaa mapema.
Hakuna kitu kibaya kama kukata tamaa mapema. Unapokuwa unakata tamaa unakuwa unaitangazia dunia kwamba wewe huwezi tena. Na kimsingi hakuna faida hata moja ambayo mtu anaweza kuipata eti kwa sababu ya kukata tamaa.
Wajasiriamali wakubwa wenye mafanikio ni ving’ang’anizi wakubwa wa malengo na ndoto zao. Wanajua bila kufanya hivyo hakuna kitakachofanikiwa. Siku zote mafanikio yanakutaka usikate tamaa mapema la sivyo, utayasikia mafanikio kwa wengine.
5. Jitoe mhanga.
Je, wewe ni miongoni mwa watu wanaojitoa mhanga kuhakikisha ndoto zao zinatimia? Kama jibu ni ndiyo basi wewe ni miongoni mwa wajasiriamali wenye mafanikio makubwa.
Sifa kubwa ya wajasiriamali wenye mafanikio ni kujitoa. Mara nyingi huwa hawaangalii hasara watakazozipata zaidi sana huangalia kile watakachokipata. Hili ni jambo muhimu sana la kulielewa na kuliweka kwenye akili yako ikiwa wewe unataka kuwa mjasiriamali wa mafanikio.
6. Nenda hatua ya ziada.
Jifunze kujiongeza na kuongeza vitu vya ziada ambavyo ni tofauti na wajasiriamali wengine. Ikiwa huwezi kujitofautisha wewe na wajasiriamali wegine, basi moja kwa moja upo kwenye hatari pengine ya kushindwa kwa baadae.
Hapa unatakiwa kujitoa na kufanya kazi zako kwa uhakika na muda mrefu. Hiyo haitoshi unatakiwa kujifunza kila wakati yale ambayo wenzio wanayafanya. Kwa kwenda hatua za ziada ni silaha muhimu ya kukufanya ukawa mjasiriamali wa mafanikio.
Naamini umejifunza kitu cha kukusidia kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio. Lakini usiishie hapa endelea kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kupata maarifa yatakayoboresha maisha yako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048 035,

No comments :

Post a Comment