Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, June 22, 2016

Kijana Wa Umri Wa Chini Miaka 30 Anayemiliki Kampuni Yake Binafsi.

No comments :
"Endapo utafika miaka 25 hujui unapoelekea ujue fika umekwisha potea"

Hayo ni maneno ambayo aliwahi kuniambia mama yangu mpendwa, hivyo kila nikikaa huwa yanajirudia sana  kichwani mwangu. Maneno hayo ndiyo ambayo yananipa hamasa kwa kila jambo ambalo nalitenda siku zote, pia hunifanya niongeze juhudi na maarifa zaidi kwa kila jambo ambalo nalifanya.
Kwani juhudi nilizonazo hunifanya niwe mbunifu kila jua lichomazapo. Ubunifu huu huwa unanijenga hasa pale ninapoyakumbuka maneno ya mwalimu wangu wa somo la brand Tanzania Mr. Nduku Jr kwani mara kadhaa alikiwa ananiambia ya kwamba kwa kuwa zama zimebadilika hauhitaji kupeleka hirizi kwenye biashara bali unahitaji ubunifu utakao kutofautisha na watu wengine.

Hivyo katika kuthibisha juu ya kauli hizo ambazo nimezieleza, mara namuona kijana kwa mbali ambaye amevalaa tisheti nyeupe ambaye yupo ofisini kwake ila kadri nivyozidi kusogea nagundua ya kwamba wapo na vijana wenzake, huku kijana huyo aliyevalia tisheti ya nyeupe akiwa anazungumza.
Loooh! Kadri ninavyozidi kusogea na gundua ya kwamba tisheti hilo limeandikwa Tim success ltd. Mmh kama ilivyokuwa kawaida yangu nikiona neno success (Mafanikio) huwa mishipa ya aldenalini huwa inashutuka kama nimepita sehemu yenye giza huku nikiwa na hofu fulani.

Hivyo kwa kuwa nimeona fulana imeandikwa success (Mafanikio) nikataka kujua mawili matatu kutoka kwao na kuwaomba nifanye mazungumzo japo ya dakika chache na kijana huyo.

Baada ya kujitambulisha mimi, kisha kijana huyo akaanza kujitambulisha kwa kusema; "Kwa jina naitwa Tamimu ni kijana ambaye mnamo mwaka 2008 niliweza kuhitimu chuo kilichopo mkoani morogoro, pia pale morogoro niliweza kusomea masomo masuala ya tekinolojia ya habari ya mawasiliano(IT).
Baada ya kumaliza niliungana na wanafunzi wengine mbalimbali katika kuandika barua kwa ajili ya kuomba ajira kama wafanyavyo vijana wengi baada ya kumaliza vyuo.

Muda mwingi ulipita bila kuona mafanikio ya kupata ajira, kila tangazo ambalo lililotoka kuhusiana na ajira ambalo lilikuwa linahusu ilikuwa ni lazima niweze kutuma barua ya maombi. Mara kadhaa nilikuwa nachaguliwa mpaka kufanya usaili lakini matokea yake nilikuwa ninaishia kufanya usali tu, licha yakuwa nilihitimu na kuwa nawastani mkubwa wa alama. Ilifika mahali mpaka nikaanza kulaumu ni kwanini nilikwenda kusoma?

Miaka mitatu ilikatika bila mafanikio yeyote ya kupata ajira, mnamo mwaka 2012 nilikutana na kaka mmoja huko maeneo ya kwetu songea, ambaye alikuwa ni rafiki wa kaka yangu ambaye alikuwa anaishi huko jijini Dar-es-salaam.
Hivyo kwa kuwa nilikuwa naamini ya kwamba Dar-es-salaam ni  njia panda ya kuelelekea ulaya hivyo niliamini ya kuwa huko kila kitu kipo, hii ni kutokana jinsi ambavyo huwa nasikia na kuona habari mbalimbali juu ya jiji hilo hivyo niliamini kupitia huyo rafiki yake kaka, nitakwenda kupata jawabu tosha juu ya tatizo langu la ajira.

Hivyo nilimueleza changamoto kubwa ambayo ilikuwa inanisibu, baadae kaka huyo(jina limehifadhiwa) alinimbia ya kwamba kutoka na kitu ambacho nimesomea nina uwezo kufanya kitu kikubwa na kutengeneza kipato changu ambacho  kitasaidia kutatua changamoto zangu binafsi pasipo kutegemea suala la ajira ambalo ni changamoto sana kwa wengi.

Baada ya siku chache tangu siku ambayo tulizungumza maneno yale, tuliweza kusafiri kwenda Dar, huko niliweza kujifunza masuala ya kutengeneza mabango ya kutangaza biashara mbalimbali, bussiness card yaani kwa ufupi naweza sema nilijifunza masuala yote yanayohusiana na designing kwa ujumla.
Pia nilijikita zaidi zaidi katika kuweka alarm za magari, muziki kwenye magari pamoja na stika za magari na ufundi mwingine. Kufanya hivi kukanifanya niweze kupata kipato ambacho nilijitahidi kuweka akiba, akiba ambayo ilinifanya nije nimiliki kampuni yangu  ambayo inaitwaTim success Ltd kama unavyoona kwenye tishiti hii.

Kijana Tamimu katikati,
akiwa na mwandishi wa makala haya Benson Chonya,
 Kushoto kabisa.
Pamoja na misukosuko mingi ambayo nilikuwa naipata wakati wa kusajili kampuni hii nilijipa moyo pasipo kuwa na hata chembe ya kukata tamaa. Ilifika kipindi hata pesa ya kuendesha maisha yangu ilikuwa ngumu kwa kuwa pesa nyingi zilitumika katika nauli pamoja na usajili wa kampuni.

KUHUSU KAMPUNI
Kwa kifupi ni kwamba mimi kama ndiye mwazilishi wa kampuni niliwaza ya kwamba katika nchi yetu lina jopo kubwa ni vijana. Na kwa kuwa asilimia kubwa ya vijana hao ni wale wasomi na wasio wasomi, lakini changamoto kubwa ambayo inatukabili ni suala la ajira, nikaona ni vyema kwangu niifanye kama fursa ili niweze kuwasaidia vijana wenzangu, hivyo nikawakusanya vijana wenye ujuzi na wasio na ujuzi tukajifunza pamoja kuweza kufanya mambo mbalimbali.
Mambo hayo ni kama vile umeme , mapambo ya nyumba, kufunga kamera za ulinzi majumbani, kufanya designing, kupima viwanja(land survey),kuandika miradi mbalimbali na kuwashauri vijana wengine ambao wamekata tamaa na Maisha haya.

Kama timu ya mafanikio mnaleta suluhisho na changamoto gani ambayo inaihusu jamii kwa ujumla? Kama timu tumeamua kuja na suluhisho la changamoto ya maji. Kwa kuwa tunasema kwa kuwa maji ni uhai, hivyo tukaona ni vyema tuweze kuja na majibu kwani changamoto ya maji ni kubwa.
Unajua ndugu mwandishi licha ya kuendelea kusema ile sera ya kilimo kilimo kwanza lakini tunashidwa kufikia sera hiyo kwa kiwango cha juu, hii ni kutokana hatuna kilimo cha umwagiliaji, hivyo tunajikuta tunafanya kilimo kilekile miaka nenda miaka rudi. Pia ukijaribu kufanya uchunguzi mdogo utagundua ya kwamba majimbo mengi yana changamoto ya maji.
Hivyo sisi kama vijana wachapa kazi tumeamua kuja na suluhisho ambapo tunatengeneza visima ambavyo maji mengi yatavunwa kwa kutumia nguvu ya upepo, hapa ndugu mwandishi haitaji uwepo wa Umeme, au kupungua kwa maji kwenye chanzo bali mashine hii itatoa maji muda wote, nafikiri hii itasaidia sana hasa maeneo ya mjini na vijini ambayo kiuhalisia yana changamoto ya maji, wito wetu kwa viongozi Wa serikali na watu wengine hii ni fursa ambayo itabadili Tanzania kwa asilimia kubwa sana, kwani tutakwenda kuwa wakulima bora ambao hatutegemei misimu kufanya kilimo chetu tu.

Neno langu la mwisho ni kwamba kupata maendeleo kwa kiwango kikubwa inawezekana lakini jambo la msingi la kuzingatia ni kwamba inahitajika ushilikishwaji wa wananchi katika kutoa maamuzi yao kwani ni muhimu sana, mwisho kabisa nawashauri sana vijana ambao hawana ajira ni kwamba wazipe nafasi bongo zao kuweza kufikiri kwa umakini ni jinsi gani wataweza kuondokana na adhaa hii ya ajira kama tulivyofanya sisi

Kama una swali lolote kwa Mr tamimu piga au sms kwenda
0714-800922.
Kama una hadithi kama hizi zenye ukweli na ubunifu wasiliana na afisa mipango Benson chonya (0757-909942
).

No comments :

Post a Comment