Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, June 6, 2016

Jambo La Msingi Unalotakiwa Kulijua, Ili Kutimiza Ndoto Na Malengo Yako.

No comments :
Naomba nianze makala hii kwa kukuuliza hivi je, umeshawahi kujiuliza ni sifa gani walizonazo matajiri hadi kuwapelekea wao kuwa matajiri? Je, pia ulishawahi kujiuliza ni mambo yepi ya ziada wanayowafanya watu mtajiri kuzidi kuwa matajiri? Au je, pia na wewe binafsi ulishawahi kujiuliza ni aina gani ya tabia, sifa, au imani unayotakiwa uwe nayo ili uwe tajiri?
Nimeanza maswali hayo kukufikirisha kidogo kwa sababu naamini na wewe ni kati ya watu ambao wapo kwenye safari ya kuelekea kwenye utajiri kama ilivyo kwangu. Na ni vyema ukawa unajua majibu ya maswali haya ili wakati upo kwenye safari yako ya kutafuta mafanikio makubwa ya utajiri yawe msaada kwako.
Naamini sana hakuna mtu asiyependa mafanikio makubwa. Kila mtu anapenda mafanikio makubwa ila tatizo la walio wengi hufikia mahali wanashindwa kujua waanzie wapi ili kufika kwenye kilele cha mafanikio makubwa. Nasema hivyo nikiwa na maana, ukisema hutaki utajiri basi utakuwa ni sawa na kuniletea hadithi ya sungura ‘sizitaki mbivu hizi’.
Sasa kama nia na lengo ni kufikia mafanikio makubwa tena ya utajiri, huwezi kukwepa kujua sifa, tabia na hata mambo wanayofanya matajiri ili kufikia pale walipo. Bila kujua vitu hivyo ambavyo wanavifanya matajiri na hadi kufanikiwa itakuwa ni kazi bure kwako kuweza kufanikiwa. Juhudi zako nyingi ambazo utakuwa unaziweka zitakuwa hazina msaada sana.

Kwa chochote unachokifanya, kifanye kwa ujasiri.
Kwa kujua umuhimu wa hilo, leo nimeaamua kukushirikisha jambo moja la msingi ambalo watu wenye mafanikio wanalo sana. Kutokana na jambo hilo hupelekea wao kuweza kutimiza ndoto na malengo yao, ikiwemo malengo ya kufikia kwenye utajiri. Jambo hilo ambalo watu wenye mafanikio wanalo sana ni ile kubeba sifa ya kutenda kwa ujasiri.
Watu wenye mafanikio siku zote mambo yao na mipango yao wanaifanya kwa ujasiri na kujiamini sana. Na mara nyingi huwa haijalishi wana uzoefu katika jambo hilo au hawana, kikubwa wanachokizingatia ni kufanya kwa ujasiri hadi kufanikiwa, hata kama hawana uhakika na matokeo. Ni ujasiri huohuo ambao kwa namna moja au nyingine hupelekea wao kuwa washindi.
Ili uweze kunielewa zaidi katika hili hebu twende kwa mifano. Mark Zuckerberg mwazilishi wa mtandao maarufu wa facebook, asingeweza kuanzisha mtandao huo ikiwa ndani yake asingekuwa na sifa ya kutenda kwa ujasiri. Kilichokuwa kikimpa jeuri kwamba ni lazima atafanikiwa ni kule kuamua kutenda kwa ujasiri. Na hiyo kweli ilimsaidia kufanikiwa. 
Mwangalie Evander Holyifield mpiganaji wa ngumi enzi hizo pia naye asingeweza kumpiga Mike Iron Tyson kama tu asingeamua kubeba sifa ya kutenda kwa ujasiri. Ilikuwa sio rahisi kwa mtu yoyote kuamini eti Tyson anaweza kupigwa na Evander hasa kutokana na Tyson alivyokuwa na uwezo mkubwa wa kupigana ikiwa pamoja na kushinda karibu kila shindano.

Ukitenda kwa ujasiri unaweza.
Hiyo haitoshi hebu tutazame maisha ya Nick Vujicic. Kwa kumtazama ni rahisi sana kumuonea huruma kwa sababu ya ulemavu wa miguu alionao. Lakini ukiona maisha ya mafanikio aliyonayo unaweza ukalia kwa kujionea huruma wewe kwa kuwa kamili lakini huna kitu.
Nick Vujicic pamoja na ulemavu wake huo amefanikiwa kuwa mhamasishaji wa mafanikio na kutenda mambo mengi sana ikiwemo hata kucheza piano, kuandika kwenye kompyuta lakini akiwa hana mikono wala miguu. Kitu kikubwa kilichomfikisha hapo ni kule kuamua kutumia sifa ya kutenda bila kuogopa kitu chochote.  
Ukiangalia historia ya dunia utakuja kuona ina watu wengi ambao waliitwa hawawezi kutokana na walivyochukuliwa lakini wao walijiaminisha na kuweza. Ipo nguvu kubwa sana ya kufanikiwa kama utatumia sifa ya kutenda kwa ujasiri. Tunaposoma maandiko matakatifu yanatuonesha, hata Goliathi alipigwa na Daudi hiyo yote kwa sababu Daudi aliamini nguvu kubwa ya kuweza kutenda kwa ujasiri.
Kuna wakati katika maisha unaweza kupambana na changamoto nyingi sana, kiasi kwamba ukajiona huwezi kitu tena. Lakini inapotokea hivyo, simama tena na jiambie unaweza kupambana na chochote na hakika utakuwa mshindi. Kwa chochote unachofanya, hata kama unakiona ni kigumu sana kifanye kwa kumaanisha huku ukitenda kwa ujasiri, utafanikiwa.
Watu waliofanikiwa si kwamba wao wana akili sana au uwezo mkubwa wa tofauti. Wanafanikiwa kwa sababu wanaamua kutenda kwa ujasiri. Kila wanapokutana na changagamoto hukabiliana nazo hivyo hivyo kwa ujasiri mkubwa. Siku zote acha kujiruhusu kushindwa kwa urahisi, utapotea sana na hutafanikiwa. Lilokubwa kwako tenda kwa ujasiri hadi kufanikiwa.
Je, jiulize tena katika maisha yako unatenda mambo yako kwa ujasiri? Kama uko kinyume na hapo anza sasa kutenda mambo yako kwa ujasiri ili kufanikiwa.
Kama makala hii imekuasidia kwa namna moja au nyingine mshirikishe na mtu mwingine aweze kujifunza kupitia mtandao wako wa DIRA YA MAFANIKIO kila siku.
Nakutakia siku njema na mafanikio mema.
Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713048035,
No comments :

Post a Comment