Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, October 26, 2016

Kipindi Muhimu Sana Cha Mafanikio Yako.

No comments :
Njia mojawapo kubwa ya uhakika ambayo ukiitumia ni lazima itakupa mafanikio ni kusubiri. Hakuna kitu au mafanikio ambayo utashindwa kuyapata katika maisha yako ,ikiwa utakuwa ni mtu wa kufanya kazi na kusubiri.
Wataalamu mbalimbali wa mafanikio, akiwemo mwandishi wa vitabu wa kimarekani ndugu J.G Holland amewahi kuthibitisha hili pia kwa kusema“Hakuna mafanikio makubwa duniani ambayo utayapata bila kufanya kazi kwa bidii na kusubiri”.
Hiyo ikiwa inaonyesha kuwa upo uhusiano mkubwa sana kati ya kile unachokitaka na swala zima la uvumilivu wakati unasubiri kufanikisha jambo lako. Ni lazima ufanye kazi na usubiri mchakato wa kufanikisha jambo lako hilo.
Hakuna mafanikio  ambayo unaweza kuyapata ‘chapuchapu’ na kuamua kukwepa njia hii. Mchakato wa kusubiri na kuwa mvumulivu kwa kile unachokitaka, upo palepale. Watu wote wenye mafanikio wanapitia njia hii kufanikiwa na sio kinyume cha hapo.

Vumilia mpaka utimize ndoto zako.
Kwa kawaida ile tu kujua kusubiri kitu ambacho una mhemko nacho au mchecheto mkubwa kukipata ni siri au hatua kubwa sana ya kuweza kukusaidia kufanikiwa. Utulivu utakao utengeneza wakati unasubiri, ndio utakusaidia ukae sana na kitu hicho tofauti na ungekipata kwa upesi.
Elewa zipo namna nyingi za kusubiri kile unachokitaka kwenye maisha yako ili ukipate. Kwa mfano, kipo kipindi cha kusubiri wateja kuongezeka pale unapoanza biashara yako. Kipo kipindi cha kusubiri miezi tisa mtoto, pale mama anapopata ujauzito.  Kipo kipindi cha kusubiri kujibiwa majibu yako pale unapoomba kazi.
Kuwa na subira, ni kipindi muhimu sana cha mafanikio yako  na pia ni kanuni ya asili. Kanuni hii inaweza ikajitokeza katika yai. Kwa kawaida yai haliwezi kutoa kifaranga mpaka zifike siku 21.
Si hivyo pia tunaona kanuni hii inajitokeza pale unapoumia na kupata kidonda. Kwa mfano tunaona, ukipata kidonda huwa hakiponi mara moja, upo muda wa kusubiri hadi kidonda chako kipone. Na ndivyo kanuni hii inafanya kazi kwa misingi kama hiyo kwa mambo mbalimbali.
Kwa hiyo inapotokea umejiwekea malengo yako na kuanza kuyafanyia kazi, jifunze kuwa na subira. Acha kuwa na haraka zisizo na msingi kuharakisha matokeo. Kama kila wakati wewe ni mtu wa haraka haraka hutafika popote. Maisha yanakutaka sana uwe mvumilivu na mtulivu ili kufanikisha makubwa.
Kipo kipindi ambacho kinakulazimisha uwe na subira ili mambo yako yatimie. Hiki ni kipindi au muda ambao unakujenga na kukufanya uweze kufanikiwa. Hichi ndicho kipindi au wakati muhimu sana wa mafanikio yako. Ukishindwa kuvumilia hapa basi utaharibu kila kitu.
Hebu jaribu kufikiria ni wangapi ambao huwa hawana uvumilivu wa kusubiri mafanikio yao, bila shaka ni wengi tu. Huwa kuna ugumu kwa watu wengi kuvumila kile wanachokitaka, zaidi ya wengi hutafuta njia za mkato sana ambazo pia huwaangusha.
Kutokana na kukosa subira, wengi hutaka mipango yao iende upesi sana. kwa mfano, vijana wa miaka 22 wao hutamani kwa umri huo wawe wana gari, nyumba nzuri, mke mzuri, miradi ya kutosha na watoto. Haa! Haa! Haa! kama hizo ni ndoto zako umepotea.
Huwezi kufanikisha maisha yako kwa kwenda kinyume na kanuni za asili au kanuni za mafanikio. Maisha yanakutaka ufuate kanuni ndogo ndogo ambazo zitakusaida kupiga hatua kila siku. Mojawapo ya kanuni hizo ni kuwa na subira.
Kama huna subira ya kutosha unataka mambo kwa upesi sana huwezi kufanikiwa. Anza leo kwa kujenga msingi wa maisha yako kidogo kidogo. Anza leo kwa kuchapa kazi huku ukiwa na subira na ndoto zako. Kumbuka ile kusubiria ndoto yako itimie, ni kipindi muhimu sana cha mafanikio yako.
Endelea kuwashirikisha wengine waweze kujifunza kupitia mtandao wako wa DIRA YA MAFANIKIO kila siku.
Pia napenda kuchukua fursa hii kukaribisha wewe rafiki yangu, kwenye kundi la Whats App ili uweze kujifunza pamoja nami kwa ukaribu zaidi. Kujiunga tuma neno MAFANIKIO YANGU, kisha ikifuatia na namba yako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,


No comments :

Post a Comment