Oct 27, 2016
Namna Ya Kutambua Shughuli Iliyokuleta Duniani.
Watu wengi huwa ni watu wa kujiuliza na kutaka kujua hasa ni
shughuli ipi iliyowaleta duniani. Mara nyingi wengi huwaza ‘ Sasa
nitajuaje kwamba, kazi hii ndiyo ambayo imenileta au nimekuja kuifanya hapa
duniani’? Ni kweli kila mtu duniani ameletwa au amekuja kwa ajili ya shughuli
ama kazi maalumu kwake ambayo ni lazima aitimize ili kuweza kufanikiwa kwa
viwango vya juu zaidi.
Tatizo kubwa linalooonekana kwa wengi wetu ni kutokujua hasa
shughuli iliyotuleta hapa duniani. Kwa kutokujua huko hupelekea wengi kuvamia
kazi ambazo sio zao na matokeo yake kushusha kiwango cha ufanisi. Kama unataka
kufikia kiwango kikubwa cha mafanikio ni muhimu kujua shughuli iliyokuleta
duniani. Swali la kujiuliza hapa utajuaje hasa shughuli iliyokuleta hapa
duniani?
1.Tambua ni kipi kimeikalia akili yako sana.
Hatua ya awali itakayokuwezesha kujua shughuli au kazi uifanyayo
ndiyo hasa unayotakiwa kuifanya, ambayo ndiyo itakayokupa ridhiko la moyo na
mafanikio, ni kuangalia kiwango chako cha kuipenda na kuridhika nayo. Lakini
pengine pia ni kupima au kujiuliza juu ya shughuli au kazi ambayo inaingia
akilini mwako mara kwa mara.
Siyo kuingia akilini kwa kufikiria kipato, hapana, bali kuingia
akilini ukitamani kuifanya. Wakati mwingine hata kuona kama vile wale
wanoifanya shughuli hiyo inayoitawala sana akili yako wamependelewa au kupata
bahati. Shughuli hii inayotawala akili yako kwa muda mrefu, mara nyingi huwa ndiyo shughuli iliyokuleta duniani.
Watu wanaofanya shughuli zilizowaleta duniani huwa wana mafanikio
mkubwa sana, hata kama shughuli hizo zinaonekana ni za watu duni, wasio na
kipato wala heshima katika jamii, lakini huweza kustawi kimapato na kuweza
kuishi kwa utulivu wa nafsi. Mtu anapofanya kile ambacho ndicho kilichomleta
duniani, kufanikiwa kwake ni lazima.
2. Tambua ‘hobi’ yako ni ipi.
Kuna wakati shughuli zilizotuleta hapa duniani ni yale mambo
ambayo sisi huwa tuyachukulia kirahisi na kuyafanya kwa urahisi kwa sababu ya
kujifurahisha. Utafiti mwingi kuhusiana na malengo yetu maishani, unaonyesha
kuwa, yale mambo tunayoyaita ‘hobi’ zinaweza zisiwe ‘hobi’ bali ndiyo shughuli
zetu za kutupa mafanikio ya kweli maishani.
Kwa mfano unaweza ukaona mtu ana kipaji kikubwa sana cha kuchora
na akawa anakitumia katika kujifurahisha tu, mwenyewe anaita ‘hobi’ wakati
ukweli ni kwamba, angeamua kuingia kwenye uchoraji kama shughuli kamili,
angefanikiwa sana. Wakati mwingine hata zile tunazoziona kama ‘hobi’ zisizo na
maana sana, wengine ni shughuli maalumu kwao na kubwa.
Kama unayo shughuli au jambo ambalo unalipenda sana na unalifanya
kama ‘hobi’, jaribu kulikagua. Inawezekana kabisa isiwe ‘hobi’ kama
unavyofikiri bali ndilo limefanya ukaletwa hapa duniani. Kumbuka hakuna
shughuli ndogo, ya kijinga au haina faida, bali inategemea wewe unayeifanya
unaifanya kwa sababu gani?
3. Kama haina umuhimu wa nje.
Kama mtu anaipenda shughuli ambayo ni wazi haijulikani wala
kufahamika kwa nje nap engine hata iikfahamika ni kwa kudharauliwa sana nab ado
mtu huyo akajivunia kuifanya shughuli hiyo, hii ni dalili nzuri ya mtu kuwa
kwenye shughuli iliyomleta hapa duniani.
Kuna watu ambao huficha shughuli zao, hawataki wengine wakajua
wanafanya shughuli gani. Huficha kwa sababu wanahisi aibu kwa kuamini kwamba
hizo shughuli zao ni zenye pengine kudhalilisha. Hawaoni kama wanastahili
kuzifanya, kwani kwao hizo ni shughuli za watu wa aina Fulani wa kiwango cha
chini.
Mtu anapogundua kuwa, anahisi aibu kutaja shughuli yake kwa sababu
anadhani ni shughuli duni, ni vizuri akaacha kufanya shughuli hiyo, kwani
anapoteza muda wake wa bure. Kudhani shughuli mtu aifanyayo ni dhalilisho, ni
dalili kubwa ya kwamba mtu huyoanafanya shughuli ambayo hakutakiwa kuigusa
maishani mwake.
4. Kutambua matatizo siyo hoja.
Kama kweli shughuli ambayo unaifanya ndiyo imekuleta hapa
duniani,ndiyo shughuli ambayo unatakiwa kuifanya, haeiwezi kuwa na matatizo.
Siyo kwamba ukifanya shughuli hiyo, huwezi au shughuli yenyewe haiwezi kukumbwa
na vikwazo, hapana. Bali yanapotokea matatizo hutakata tamaa na kusema ‘basi’.
Badala yake matatizo hayo yatakusukuma kusonga mbele na kukusaidia kujikita
zaidi kwenye shughuli hiyo.
Bila shaka umeshawahi kuona au kusikia juu ya watu ambao shughuli
fulani wazifanyazo zinakumbwa na matatizo, wengine wote wakajitoa, lakini wao
wakabaki peke yao na kuendelea nazo, kama kwamba hayo matatizo ndiyo waliokuwa
wanayasubiri. Biashara inakumbwa na matatizo ya aina fulani ambapo kuendelea
kwake ni kwa kubahatisha sana na wengi wazifunga biashara zao, lakini mwingine
anaendelea kama vile hakijatokea kitu. Kazini na mahali pengine hali kama hiyo
huweza kujitokeza pia.
Kama kweli shughuli unayoifanya ni yako kabisa haiwezi kutokea
hata mara moja ukaiacha kwa sababu ya matatizo. Hata kama utaiacha ni kwa muda
tu, kwani utajikuta unatafuta njia au mbinu ya kupata ufumbuzi wa matatizo
hayo. Matatizo hayawezi kukukatisha tamaa kama ambavyo yanaweza kumkatisha
tamaa mtu ambaye anaifanya shughuli hiyo kwa sababu za nje, ikiwemo kipato.
Huyu anayeifanya kwa sababu ya kipato, umaarufu au madaraka na sababu nyingine,
ndiye ambaye tatizo likitokea ni mwepesi kughairi na kubadili shughuli.
5. Kuwa na ridhiko la ubunifu au ugunduzi.
Kama kweli shughuli unayoifanya ndiyo ambayo ‘umeandikiwa’
kuifanya, utajikuta mara nyingi unakuwa mtundu nayo na kuvumbua au kugundua
mambo mapya. Hata kama mambo hayo mapya hayakupi faida inayogusika au ya moja
kwa moja kama ya kipato, bado uvumbuzi au ugunduzi huo utakufanya kuridhika zaidi
kuliko yule ambaye angepata pesa na kufurahia kuridhika tu kwa sababu ya pesa.
Wengi wanapobuni au kuvumbua vitu kwenye shughuli zao hukata
tamaa, kuvunjwa moyo, kuvunjwa nguvu na pengine kubadilisha shughuli zao hasa
wanapoona kwamba hakuna mtu aliyeonyesha kutambua ugunduzi wao na pengine
kuwapa zawadi au fedha. Ukiwa hivyo jua kabisa unafanya shughuli ambayo siyo
yako na ambayo haijakuleta duniani.
Kugundua na kuvumbua kinachozungumzwa hapa kunaweza kuonekana
kuwahusu watu wachache, wasomi au wenye taaluma maalumu, hapana. Mtu yoyote,
katika shughuli yoyote anaweza kugundua au kuvumbua jambo jipya na la manufaa
kwa shughuli yake, kwake mwenyewe na kwa wengine pia.
6. Nguvu ya wito.
Kuna wakati huwa tunajiuliza ni kwa nini baadhi ya watu ambao
wanauwezo mkubwa wa kubadili shughuli, bado wanang’ang’ania
shughuli ambazo zinaonekana kuwa hazina hata matumaini kidogo ya baadaye? Kwa
hapa ilifika mahali Fulani ambapo ualimu ulionekana kama vile kuufanya ni
kujitafutia umaskini na balaa kubwa kimaisha.
Lakini ni jambo linaloweza kuonekana kama la kushangaa kugundua
kuwa, kuna baadhi ya watu ambao wangeweza kufanya shughuli nyingine na
kufanikiwa sana kimapato, lakini wameamua kuwa walimu kwa furaha kubwa, wewe
mwenyewe ni shahidi umeshawahi kukutana na watu wa namna hiyo.
Hapa ndipo ambapo tunasema, mtu anafanya shughuli fulani kwa
sababu ya wito, siyo kwa sababu ya kitu kingine. Mtu anajua wazi kwamba,
shughuli aifanyayo inadharauliwa nap engine haina maslahi ya fedha, lakini yeye
anajisikia vizuri, anaona fahari na anafurahia kuifanya. Wito maana yake ni mtu
kufanya kile ambacho ndicho alichotakiwa kuja kukifanya hapa duniani, ambacho
kwa hali hiyo kimemkaa moyoni na akilini.
Kumbuka, hakuna aliyekuja hapa duniani kufanya tu shughuli ambayo
haimhusu, kila mtu ameletwa na shughuli yake. Kaa chini tafakari na utafute
shughuli iliyokuleta hapa duniani itakupa mafanikio makubwa sana.
Ni wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.