Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, February 1, 2016

Hasara Kubwa Za HOFU Katika Maisha Na Mafanikio Yako.

No comments :
Hofu ni nini? Kisaikolojia hofu ni hali yeyote inayomfanya mtu kuwa na wasiwasi, kutokujiamini na kuwa na mashaka juu ya kile anachofanya au anachofikiria kufanya.

Kimsingi na kimaumbile binadamu ameumbwa na hofu kuu mbili tu.
Hofu ya kushindwa katika maisha na hofu ya kukataliwa katika ndoa au mapenzi. Na ile hofu ya mtu kufanikiwa tumezitengeneza sisi binadamu.

Lakini hata hivyo, kila binadamu  anapozaliwa, anazaliwa na hofu kuu mbili ambazo ni hofu ya sauti kali na hofu ya kuanguka. Mchunguze kwa makini mtoto mchanga utabaini kwanza ukimrusha juu lazima ashituke na kulia. Pia ukipiga chini kitu kinachotoa sauti kali au  kelele lazima ashtuke.

Sasa naomba tuangalie faida na hasara za hofu katika maisha na mafanikio.
Kwa kifupi hofu ina hasara kubwa na inaathiri maisha ya watu kuliko faida yake. Hofu inamfanya mtu yeyote;

1. Kutokujiamini kufanya mambo yake katika maisha yake.

2. Hofu inamfanya mtu kushindwa kuthubutu kufanya hata mambo madogo yaliyoko ndani ya uwezo wake, sijui nitaweza, sijui ndo inafanywa hivi, mbona wengine walishindwa mi nitaweza? Sina elimu sana nikishindwa watu watanicheka, jamii na marafiki watanionaje wakinukuta nalima?

HOFU HUKUFANYA USHINDWE KUJIAMINI.
3. Hofu humuua mtu kisaikolojia kwa sehemu kubwa na athari za kisaikolojia kuhusu kufanikiwa kwake mfano mwanamke aliyeolewa na kuachika huwa na hofu hata akiambiwa nataka kukuoa huwa na imani ya kutendwa akilini mwake. Pia mwanafunzi aliyefeli mtihani hua ana athari za kisaikolojia kuwa naweza kufeli tena nikifanya mtihani. Hizo ni athari za kisaikolojia zinazosababishwa na hofu.


4. Hofu humfanya mtu kujiona mpweke kujitenga na watu na kujiona si wa hadhi fulani katika kundi la watu.

5. Hofu hufamfanya mtu kufanya kazi au kuzalisha vitu visivyo na ubora.

6. Hofu humnyima mtu nafasi ya kutumia kipaji chake alichopewa na Mungu.

7. Hofu imemfanya kila binadamu awe alivyo. Hivyo ulivyo ni kwa sababu ya hofu usimlaumu mtu yeyote. Kama yupo anaebisha anyooshe mkono juu. Fani uliyosomea sio kipaji chako kama unabisha we jeuri na hutaki kujifunza. Umesomea ualimu  wakati unapenda udakitari.


Sababu ya hofu uliogopa kusoma masomo ya sayansi eti magumu mwone. Hofu tu hiyo ndugu yangu. Umesomea masomo ya uandishi wa habari wakati kipaji chako kilimo acha kujidai uliogopa jamii itanionaje msomi mzima na degree nikalime? 

8. Hofu ndio iliyokufanya uogope kufanya vitu vya maendeleo kijijini kwenu au mtaa unaoishi unaogopa kujenga nyumba nzuri eti wataniloga! Unaogopa kuvaa vizuri eti watasema najidai nawaringishia. Unaogopa kufungua biashara eti nitafilisika au sina elimu ya biashara au sina mtaji Hiyo ni hofu ya kushindwa inakusumbua.

9. Hofu  inakufanya leo uwe maskini ukitegemea wazazi, ‘boom’ chuoni na ukitegemea ajira kuendesha maisha yako kisa hofu imekutawala huamini kuhusu kujisimamia mwenyewe unaamini hakuna maisha bila ajira. Wapi wewe mbona matajiri wengi hawajaajiriwa na mtu?

Ondoa hofu kuanzia leo acha hofu tena jiapize kwa Mungu kuanzia leo hofu basi. Nitapambana na hofu na Mwenyezi Mungu nisaidie. Ameen inatosha, kwa leo tafakari haya machache na chukua hatua.

Kumbuka endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza kila wakati.

Tupo pamoja,

Shariff H. Kisuda (Mzee wa Nyundo)
Simu; 0715 079 993,
Blog; dirayamafanikio.blogspot.com

No comments :

Post a Comment