google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Apr 11, 2017

KITABU; Mambo 15 Ya Kujifunza Kutoka Kwenye Kitabu Cha THE POWER OF NOW.

No comments :
Hiki ni kitabu kilichoandikwa na ECKHART TOLLE ambacho kinalenga kukutoa kwenye utumwa wa kufikiri na utumwa wa kuendelea kuteseka kwenye maisha yako, kwa sababu ya kutokujua au kukosa maarifa sahihi ya kuyatumia sasa.
Watu wanashindwa sana katika maisha kwa sababu tu hawako makini na yale wanayoyafanya sasa, wanajikuta ni watu ambao wapo wapo tu, hawafanyi jitihada yoyote kubwa ya kujifikirisha kufanya mipango yao sasa.
Hebu tuangalie mambo ya msingi  tunayoweza kujifunza kupitia kitabu hiki;-  
1. Matatizo mengi ya binadamu chanzo kikubwa yanaanzia kwenye ufahamu na sio sehemu nyingine yoyote. Ukichunguza utagundua matatizo mengi sana yamesababishwa na matokeo ya kutokutumia ufahamu kwa usahihi.
2. Hakuna kitu ambacho kinaweza kukutokea katika maisha yako bila ya wewe kuamua kuanza sasa. Nguvu kubwa  ya mafanikio inaanzia hapo ulipo kwa kukubali kuchukua hatua mara moja. Huwezi kuwa na maisha mazuri kesho, kama kwa sasa hufanyi kitu cha maana, msingi mkubwa wa mafanikio yako unajengwa sana leo. Hivyo wekeza sana leo, upate mafanikio makubwa kesho.
3. Uhalisia wa maisha yako unatengenezwa sasa, unapofikiria kwamba kesho utakuwa na maisha mazuri, maisha hayo hayawezi kuja kama sasa unafanya upuuzi mwingi, lazima ujue nguvu ya mafanikio yako inatengenezwa sasa. Hata hayo maisha bora unayoyataka yatakuja kwa kutenda vilivyo bora kwanza sasa.
4. Kila wakati unatakiwa ujiulize kama hautaweza kufanya mambo yako sasa, utayafanya lini? Je, unafikiria kwamba utakuwa na muda wa kutosha hapo baadae? Maisha yako yanatengenezwa sasa na sio kesho, kesho unayoisubiri sana inaweza isifike kwako na ukashindwa kutenda, chukua hatua mapema.
5. Kama kuna kitu unakifanya, acha kuweka nguvu zako nyingi kwenye matokeo, badala yake weka nguvu zako nyingi kwenye hatua unazochukua. Ukiweka nguvu zako nyingi kwenye matokeo na ukashindwa kuyapata matokeo mapema, itakufanya ushindwe kufurahia hata kile unachokifanya.
6. Njia rahisi ya kumjua mtu vizuri ni kutazama ile thamani anayoitoa. Kama unaona mtu huyo anatoa mawazo mabovu au thamani anayoitoa ipo duni, basi elewa kinachoingia ndani yake ni kibovu pia.
Mara nyingi vile vitu tunavyovitoa nje, ni ishara ya sisi jinsi tulivyo ndani yetu. Sasa jiulize mwenyewe kila siku unatumia jitihada gani, kuwekeza ndani yako na kuwa bora kila iitwapo leo?
7. Popote ulipo weka mawazo yako hapo. Chochote unachokifanya pia weka mawazo yako hapo. Weka nguvu yako ya mawazo kwa kile unachokifanya. Epuka mara moja tabia ya kufanya kitu hiki halafu mawazo mengine yapo kule. Hutaweza kufanya kwa usanifu kama mawazo yako yamegawanyika sana, zaidi utajipotezea muda wako bure.
8. Kuna malengo makubwa ya aina mbili katika maisha yako. kwanza, kuna lengo la nje na pili kuna lengo la ndani. Haya ni malengo makubwa yanayoongoza maisha karibu ya watu wote duniani.
Malengo ya nje ni yale malengo yanayotokana na kuchukua hatua zitakazokuwezesha kufikia malengo yako uliyojiwekea. Hatua hizi ni rahisi kuziona sana.
Malengo ya ndani ni yale malengo yanakufanya uchukue hatua ndogo ndogo na za sasa kuweza kutimiza malengo yako. Kama hutaweza kufanikiwa katika malengo haya ni ngumu kufanikiwa.
Kwa hiyo ni lazima ufanikiwe kwanza katika malengo ya ndani, malengo ambayo unafanya kila siku au sasa, ili ujenge msingi mkubwa wa kufanikiwa kwa kesho au kwa malengo yako uliyojiwekea.
Watu wengi wanajisahau katika hili na kujikuta ni watu wa kuwaza malengo makubwa na kusahau malengo madogo madogo ambayo yangeweza kuwasaidia. Fanikisha malengo madogo kwanza ya ndani na utafanikiwa.
9. Kuwaza tu kile unachokifanya peke yake bila kupeleka mawazo sehemu nyingine inakufanya kufanya jambo hilo kwa usahihi, lakini pia inakutengenezea nguvu nyingi zaidi za kufanikisha jambo hilo. Hiyo iko hivyo kwa sababu, mawazo yote ya nje yanayoweza kukukwamisha yanakuwa yanapungua sana, hivyo nguvu zako unajikuta zinaelekea sana kwa kile unachokifanya na kuleta matokeo sahihi. Hii ndiyo faida ya NGUVU ZA UZINGATIVU.
10. Huwezi kuona uzuri au thamani ya kile ulichonacho mpaka mawazo yako kwa muda mwingi uyaweke kwenye hicho kitu ulichonacho. Kwa mfano, huwezi kuona uzuri wa kazi yako mpaka mawazo yako yawe kwenye hiyo kazi yako. Pia huwezi kuona uzuri wa mume au mke wako kama kila siku unakazana tu kuwaangalia watu wengine.
Mara nyingi ni rahisi tu kuona uzuri kwa mambo yasiyo ya kwetu kwa sababu akili zetu tunakuwa tumezielekeza huko sana na kusahau kabisa ya kwetu. Siri kubwa ya kuona thamani ya kile ulichonacho ni kuweka mawazo kwenye kitu hicho ulichonacho. Kama kuna kitu unataka kuona thamani yake ni rahisi tu, weka juhudi na mawazo yako hapo.
11. Kila wakati jifunze kuwa msikilizaji mzuri. Kama kuna kitu mtu anazungumza hebu msikilize vizuri. Acha kufikiri vitu vingine kama kuna mazungumzo yanaendelea ya mtu mwingine. Hutaweza kujua mtu huyo anayezungumza ana maanisha nini? zaidi utaanza tena kuuliza kwa sababu ya kutokusikiliza kwako.
12. Unatakiwa uwe na utulivu mkubwa sana ndani yako wa kifikira ndio uwe na utulivu wa nje. Kama ndani yako hauna utulivu mkubwa hata kwa nje utaonekana haujatulia. Jitahidi sana kutuliza fikra zako ili kupata utulivu pia wa nje utakaokusaidia kufanikiwa.
13. Upendo wa kweli katika maisha hauchagui. Kama lilivyojua ambavyo halina ubaguzi wowote pia upendo wa kweli katika maisha hauchagui. Upendo huu wa kweli una mulika popote bila kuchagua. Hili ndilo pendo ambalo analo Mungu wetu. Ni upendo ambao hauna ubaguzi wowote.
14. Mbinu mojawapo bora ya kuondokana na mawazo hasi ni kuweka mawazo yako katika eneo moja. Ikiwa utakuwa una uwezo wa kuweka mawazo yako eneo moja na kwa muda mrefu basi utafanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kuweza kuondokana na mawazo mengi sana hasi ambayo yangekuzuia kwa namna fulani kufanikiwa.
15. Kama hali yako ya nje ni mbovu na huipendi, anza kubadilisha hali ya ndani yako sasa. Mabadiliko yote, yanaanzia ndani mwako kwanza na sio sehemu nyingine yoyote ile. Anza kubadilisha hali hiyo sasa.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Blog, dirayamafanikio.blogspot.com
Mawasiliano; +255 628 929 816, +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com

No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.