Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, April 7, 2017

Dalili Zinazoonyesha Kwamba Hutaweza Kutimiza Ndoto Zako.

No comments :
Najua kuna wakati unakuwa unajiwekea malengo yako vizuri tu, lakini unakuwa unashangaa kwa nini pamoja na kujiwekea malengo hayo bado tu ndoto zako fulani hazitimii?
Naamini umeshawahi kukutana na kitu kama hiki na kimekuwa kikikusumbua sana na kushindwa kujua ni nini ambacho huwa kinatokea hadi kuna ndoto zako nyingine hazitimii.
Kupitia makala haya nataka nikupe jibu litakalokusaidia kujua dalili zinazoonyesha kwamba hutaweza kutimiza ndoto zako.  Kama una dalili hizo ujue kabisa ndoto zako haziwezi kufanikiwa hata ufanyaje.
Hebu sasa twende pamoja kwenye somo letu tujifunze dalili zinazoonyesha kwamba hutaweza kutimiza ndoto zako.
1. Kusubiri wengine wakubali ndoto yako.
Kati ya kosa kubwa ambalo hutakiwi kulifanya wakati unajiwekea ndoto zako ni kule wewe kuendelea kusubiri wengine wakusifie au wakubali kwamba eti ndoto yako ni nzuri na itatimia. Huhitaji kitu cha namna hiyo hata mara moja.
Unachotakiwa kufanya ni kwa wewe kufanya tu. Acha kusubiri mtu fulani akwambie ndoto yako inawezekana. Taarifa ya kujimbia kwamba utafakisha hili au lile unatakiwa ujiambie wewe kwanza.
Kwa hiyo dalili ya kwanza na ya wazi kabisa ambayo itasaidia kutuonyesha kwamba ndoto yako haiwezi kutimia ni kule wewe kusubiria wengine wakwambie ndoto yako inawezekana. Kama unasubiria uambiwe hivyo, unajichelewesha hutaweza kufanikisha kitu.

Acha kusubiri sana, tekeleza ndoto yako mara moja.
2. Kutoipa ndoto yako vipaumbele.
Ni rahisi sana kusema kwamba nina ndoto ya kufanya kitu fulani au nataka kufanikisha jambo hili mwaka huu. Hata hivyo ukiwaangalia watu wengi wanaosema hivyo, ndoto zao hizo hawazipi sana vipaumbele.
Utakuta ni watu wa kusema tu, lakini hawachukui hata zile hatua ndogo ndogo za kufikia ndoto zao. Kiuhalisa, kama ndoto yako hauipi vipaumbele, yaani huchukui hatua hata ndogo ndogo, hutaweza kufanikisha ndoto yako hiyo, zaidi utajidanganya.
3. Kutoipa ndoto yako hali ya uzingativu.
Kama unataka kujua ndoto yako itafanikiwa au haitafanikiwa angalia jinsi unavyoipa nguvu ya uzingativu. Je, unaizingatia ndoto yako kila wakati? Ndoto hiyo inakunyima usingizi? Kama hakuna uzingativu hauwezi kuifanikisha.
Wale wanaoshindwa katika ndoto zao, wengi wanashindwa kuzizingatia ndoto zao, yaani wanashindwa kuwa na ile tunasema ‘focus’, kuweka mawazo ya aina moja kuelekea kwenye ndoto zao.
4. Kutokuwa na mahusiano na watu sahihi.
Ndoto yako haiwezi kutumia kama upo kwenye mazingira mengi na watu ambao sio sahihi kwako. Inatakiwa ujue watu wanaokuzunguka ni akina nani? Je, watu hao wana msaada katika kutimiza ndoto zangu au hapana.
Watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwa sababu ya jambo kama hili la kutokuwa na mahusiano sahihi. Wengi ni watu ambao wana mahusiano mabovu sana, hali ambayo huweza kupelekea mipango yao hiyo isiweze hata kutimia.
Hizo ndizo dalili muhimu ambazo zinaweza kuonyesha kwamba hutaweza kutimiza ndoto zako. Kama una dalili hizo na unataka ndoto zako zitimie, hakikisha;-
Kwanza, unafanya kile unachokiamini kuelekea kwenye ndoto zako bila kusubiri mtu mwingine akwambie jambo hili linawezekana. Jiamini kwamba unaweza kutimiza ndoto zako na uiamini pia ndoto yako.
Pili, hakikisha unaipa ndoto yako vipaumbele. Jua kitu cha kufanya kila siku kitakachokusogeza kwenye ndoto yako. Usiache siku ikapita bila kufanya kitu cha kukupeleka kwenye ndoto zako.
Tatu, hakikisha unajenga tabia ya uzingativu kwenye ndoto yako. Mawazo na akili zako kila wakati unatakiwa uzielekeze kwenye ndoto zako na kila kitu kitatimia kwako.   
Mwisho, Jenga mahusiano sahihi na watu watakaokusaidia kutimiza ndoto zako. Hapa kwa kifupi tengeneza ‘timu’ itakayokusaidia kufanikiwa.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku na washirikishe wengine pia waweze kujifunza kupitia mtandao huu.
Kila la kheri katika kufikia mafanikio  makubwa.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 628 929 816, +255 713 048 035,

Email; dirayamafanikio@gmail.com

No comments :

Post a Comment