Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Sunday, April 2, 2017

Usipoteze Uwezo Na Mafanikio Yako Kwa Kuamini Hivi…

No comments :
Fikiria kuhusu sheria ulizojiwekea na kile unachokiamini katika maisha yako. Sheria au kile unachokiamini msingi wake unatokana na nini? Je, msingi wake umetokana sana na wewe au unaiga tu maisha ya wengine?
Kwa mfano, unaamini sana ukiwa na pesa basi tena utakuwa na matatizo kidogo au changamoto umeziondoa kabisa. Kitu cha kujiuliza huo ndio ukweli au unajidanganya bado?
Unaamini pia ili furaha yako iwe timilifu ni lazima ufanye mapenzi au uwe na wapenzi wengi ambao wanakufariji. Kwa sababu hiyo unajisahau kwamba kumbe upo uwezekano mkubwa pia wa kupoteza afya yako.
Pia unaamini sana huna mafanikio ya aina fulani au huna kazi ya aina fulani kwa sababu hukusoma na unajiona hufai. Hivyo, umekuwa mnyonge sana na kujilaumu kwa nini hukusoma.
Hata hivyo unaendelea kuamini sana kwamba wewe hauko bora kabisa na kuwapa ubora huo watu wengine na matokeo unasahau kutumia hata uwezo mdogo ulionao ili ukusaidie kufanikiwa. 

Hata wewe unao uwezo mkubwa wa kufanikiwa, acha kujilinganisha sana.
Kwa kuamini hivyo umekuwa ukijipoteza kwa sababu umekuwa ukifuata sheria za wengine za mafanikio walizojiwekea bila hata wewe kujua na kushindwa kabisa kufuata sheria zako za mafanikio.
Unaamini sana kuna ubora wanao ambao wewe huna au kuna njia pengine hata za mkato wanapitia ambazo zimewapa wao mafanikio. Kwa hali kama hiyo umekuwa hufanyi kitu na kujiruhusu kushindwa.
Kitendo cha kufikiria hivyo tu umekuwa ni mtu wa kupoteza muda wako bure. Tambua kila mtu ana kitu bora cha kujivunia ndani yake ambacho kwa mwingine kitu hicho hakipo.
Sasa kama iko hivyo kwa nini umekuwa ukijiweka kwenye hali ya unyonge sana kujibebesha lawana kwa kuamini wengine ni bora kuliko wewe. Fikra hizi zinakuangusha, unatakiwa kuzifuta mara moja.
Kwa kuamini fikra hizo, umekuwa ukijipunguzia nguvu na mafanikio yako na kujikuta unawapa wengine mamlaka na nguvu ya kufanikiwa na kujisahau wewe mwenyewe.
Ni wakati wa wewe kutambua kwamba unao uwezo ambao unatakiwa kuutumia hadi kufanikiwa. Uwezo huo unao ila utakuja kwa kuundeleza na sio kukaa tu na kutegemea muujiza.
Ondokana na fikira za kwamba wengine ni bora kuliko wewe. Hata wewe una kitu ambacho wengine wanaweza kukitamani na kukifanyia kazi. Sasa kama iko hivyo kwa nini ujidharau?
Kazi kubwa unayotakiwa kuifanya kama nilivyosema ni kuendeleza kitu hicho ambacho unacho na kikupe mafanikio. Acha kutulia, tambua uwezo au kipaji ulichonacho na kukiendeleza.
Kama ni kipaji kidogo ulichonacho, kitumie kikusaidie kufanikiwa. Kagua uwezo ulionao hiyo ni njia sahihi ya kukusaidia kufanikiwa. Usiruhusu uwezo huo uwape watu wengine.
Ukweli usiojua ni kwamba watu unaowaona wako bora kuliko wewe, kwa ndani wako kama wewe tu, hakuna tofauti kubwa sana iliyopitiliza, zaidi yako wewe unajidharau tu.
Watu hao hawana kanuni ya ajabu ambayo wanaitumia ambayo wewe huna, kikubwa unachotakiwa ujue wanauendeleza uwezo wao sana karibu kila siku hadi kufikia mafanikio yao.
Ukiamua leo kukiendeleza chochote ulichonacho uwe una uhakika utafika mbali sana kimafanikio na kufanikiwa vikubwa. Hakuna kitachokuzuia ni lazima utafika kwenye mafanikio yako.
Acha kupoteza uwezo wako na mafanikio yako kwa kuamini kwamba wengine ndio wanaweza, utapotea.
Ansante kwa kutufatilia, washirikishe wengine waweze kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,

Blog, dirayamafanikio.blogspot.com
Mawasiliano; +255 628 929 816, +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com

No comments :

Post a Comment