Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, November 11, 2015

Mambo Matatu Muhimu Yatakayokusaidaia Kutatua Tatizo ulilonalo.

No comments :
Siku zote hata uwe na tatizo kubwa vipi, ipo njia ya kutoka pale ulipo. Kuna wakati unaweza ukahisi matatizo uliyonayo ni magumu sana na yatakushinda kuyavumulia, lakini hiyo siyo kweli kabisa. Uwezo wa kutoka hapo unao tena mkubwa kuliko unavyoweza kufikiri. Ndani yako unayo mbegu ya ushindi ambayo ukiitumia lazima ufanikiwe.
Lakini pamoja na kuwa na uwezo huo ndani yetu wa kushinda matatizo, kuna baadhi ya watu wanapokutana na matatizo, mara nyingi wanafikiri matatizo ni mabaya. Watu hawa huwa wako tofauti na ukweli kwamba matatizo siku zote siyo mabaya, bali ni chanzo cha kuondoa mabaya na kukupeleka kwenye ushindi mkuu.
Matatizo yote unayoyaona duniani yana umuhimu kama alama ya maisha yako. Pia unaweza kusema kwamba kwa kadri unavyozidi kuwa na changamoto ndivyo ambavyo unazidi kuwa na maisha magumu na mabaya. Hilo sio kweli. Njia pekee ya kuweka watu imara na kufikia mafanikio makubwa ni ya kupitia changamoto ama matatizo kama ilivyozoeleka.
Mtu anaweza kukua na kufikia kilele cha mafanikio makubwa kwa kukabiliana na changamoto, vikwazo na mahangaiko. Umuhimu wa pekee wa yale matatizo uliyonayo mara nyingi yanakuwa yanakupa mwelekeo, nguvu, dira na uwezo mkubwa wa kukujenga ikiwa utajifunza kwa matatizo hayo vizuri.
Kuna wakati fulani miaka ya nyuma mwanasayansi mmoja aliwahi kuandika katika mlango wa maabara yake kwamba “Usiniletee au kunieleza kuhusu mafanikio yako yatakayonidhoofisha, bali uniletee matatizo yako yatakayonitia nguvu na kuniinua”. Hiyo ndiyo siri iliyo kwenye matatizo, lakini ikiwa utajifunza na kuyatumia vizuri. Kinyume cha hapo ukiyawazia hasi matatizo yako utakwama sana.
Najua unaweza ukawa upo kwenye matatizo ya aina fulani yanayokusumbua sana lakini sikia, tatizo ulilonalo sio kubwa sana kama unavyolifikiria, ukubwa wa tatizo utakuja pale endapo utashindwa kulitatua. Unaweza ukatumia mambo matatu kwa ajili ya kutatua matatizo yako na kufanikiwa. Mambo haya ni kama yafuatayo:-
1. Tambua tatizo ulilonalo vizuri.
Pale ambapo utatambua chanzo kikuu cha tatizo lako, hiyo itakuwa hatua kubwa ya kwanza ya kulitatua tatizo hilo. Matatizo yote yanahitaji ujuzi na uelewa wa hali juu kabla hatujakabiliana nayo. Akili na uelewa wa binadamu ni nguvu kubwa katika kutambua na kuelewa namna ya kutatua tatizo. Tumia akili yako pale unapoona tatizo lolote na ulielewe na kulitatua.

TAFAKARI KWA MAKINI UWE MSHINDI KWA TATIZO LAKO.
2. Tafakari njia utakazotumia kulishinda.
Akili yako imejaa masuluhisho mengi, chagua moja na kisha ulitumie ili ufanikiwe. Usijaribu kutafuta suluhisho kwa hisia zako, fikiria, fikiria na uje na njia sahihi ya kutatua tatizo lako. Binadamu kwa bahati nzuri anao uwezo wa kumudu matatizo yake, japokuwa kuna magumu na maumivu mengi. Lakini yote hayo huwa yanawezekana kwa kutafakari na kuamua kuchukua njia sahihi ya kushinda tatizo hilo.
3. Amini utafanikiwa.
Hata uwe na tatizo kubwa kiasi gani amini siku zote ushindi upo ikiwa utatumia njia sahihi za kutatua tatizo hilo. Hakuna kitakachoshindikana kwako ikiwa utalitambua tatizo ulilonalo na kuamua kufuata njia salama ya kukabiliana nalo.
Acha kulia na kuhuzuninika sana, tatizo ulilonalo sio mwisho wa dunia, ipo njia ya ushindi inakusubiri. Tumia njia hizo zikusaidie kukabiliana na tatizo lolote ulilonalo kwenye maisha yako.
Endelea kujifunza kupitia mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kila siku, kumbuka TUPO PAMOJA.
Makala hii imeandikwa na Noel Ngowi wa Moshi- Tanzania. Kama una maoni au ushauri wasiliana na mwandishi wa makala hii kwa email truesuccess89@gmail.comNo comments :

Post a Comment