Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, January 20, 2016

Mambo Ambayo Wengi Hujutia Katika Dakika Za Mwisho Za Maisha.

No comments :
Kwa waliofanya au wanaofanya kazi katika hospitali kwenye vitengo ambavyo wanaweza kuongea na kuonana na wagonjwa ambao wapo katika hali ya kukaribia kifo au walizidiwa na kushindikana kupona hivyo wanangojea kifo, wamejifunza mengi. Au kama umewahi kuwa karibu na mzee anayesubiri siku zake za mwisho kufika au mgonjwa ambaye anaumwa ugonjwa usiopona. Katika mahospitali au kwenye watu wazee wanaosubiria siku zipite, kuna mengi sana wanaweza kutufundisha kuhusiana na maisha. 
Leo tutaangalia mambo matano ambayo wengi hujutia katika dakika za mwisho kabla ya kifo. 
1. Natamani ningeishi maisha yangu kwa jinsi ninavyopenda mimi mwenyewe na sio kama watu wanavyonilazimisha niishi.
Hii ni mojawapo kati ya kauli ambayo wengi wanaokaribia kufa huzungumza. Ni kauli inayotamkwa na wengi. Katika maisha ya ujana kuelekea utu uzima wengi huishi maisha ambayo wanakuwa wamelazimishwa na marafiki, ndugu au wazazi. Wengine huishi maisha kuwafurahisha watu bila wao kupenda maisha hayo. Wengine huona raha kudanganya maisha wanayoyaishi na ikifika safari ya mwisho wa maisha hujutia sana kwa walipoteza muda wao kuishi maisha kwa jinsi watu wanavyotaka na sio kama wao wanavyotaka.

Kama unapenda kuwa daktrari kuwa daktari na sio uwe mtu wa aina nyingine wakati ndoto zako hazipo huko. Ishi katika ndoto zako na malengo yako. 

FURAHIA MAISHA NA FAMILIA YAKO.

2. Natamani nisingefanya majukumu na kazi nyingi kwa kujitesa sana na kukosa muda.
 Wengine hutumia muda mwingi katika maisha yao kufanya kazi na kuwa busy sana muda wote. Wengine husahau familia, marafiki na ndugu. Mwisho wa maisha ukifika unajutia kutumia maisha yako kuwa busy kila saa na kusahau kuyafurahia maisha kwa wakati mwingine na sio kujitesa katika majukumu tu.
Maisha yanahitaji usawa (balance). Kila kitu kina nafasi yake na umuhimu wake. Kimoja kuzidi sana huleta madhara. Ni vyema kuwa mtu wa kupangilia muda wako vyema katika kila jambo. 
3. Natamani ningekuwa na nafasi ya kuonyesha hisia zangu. 
Kuna watu wanajisahau kuonyesha au kuelezea hisia zao kwa ndugu, watu, familia na marafiki. Na inapofika dakika za mwisho za maisha mtu anaumia sana na anajuta ni kwanini hakutumia muda wake vyema kujali watu, kuonyesha upendo kwa maneno na vitendo.

Wakati ni kitu cha umuhimu sana katika maisha, hivyo inatufundisha ni vyema kujitahidi kutumia muda tulio nao kuonyesha hisia zetu kwa tunaowapenda na wanaotupenda. Kama kuna matatizo omba msamaha au toa maamuzi mazuri yatakayo saidia kusuluhisha matatizo na mwisho uweze kuishi kwa amani. 
4. Natamani ningekuwa karibu na familia na marafiki zangu. 
Wengi huonyesha kujali mtu pale akifariki. Marafiki wa zamani watakuja kukuaga, ndugu na watu wanaokufahamu. Lakini hivi sasa hakuna anayefanya hivyo. Kila mmoja ana shughuli zake, lakini katika dakika za mwisho au baada ya maisha kuisha wengi watajitokeza kuwa wanakujua na kukupendi, hivyo ndivyo wanadamu tulivyo. Wajali marafiki na ndugu zako. Tumia wakati huu vyema.

5. Natamani ningekuwa nimeipata furaha yangu ya Kweli. 
Wengi wanajisahau sana. Wengine wanaitafuta furaha kwa tamaa, mali, raha n.k. Mwisho ukifika wanajuta na kutamani wangeweza kuipata furaha ya daima. Furaha isiyoshikiliwa na mali, raha, thamani na anasa. Mpaka mwisho wa maisha ukifika unaanza kutambua kuwa kumbe furaha sio mali, raha, anasa, na tamaa. Bali furaha inatoka ndani mwako ukiweza kuishi kiusahihi na kuridhika na maisha na kushukuru kwa kila jambo.
Maisha ni YAKO. Hakuna mwingine anayeweza kukuchagulia maisha ya kuishi. Maamuzi unayoweka katika maisha yana adhari kwako na kwa watu wanaokuzunguka kwa kiasi fulani. Fanya maamuzi sahihi ya kimaisha, kuwa mkweli na nafsi yako. Amua kuwa na furaha hivi sasa.
 Makala hii imeandikwa na Apolinary Protas wa JITAMBUE SASA.No comments :

Post a Comment