Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, January 6, 2016

Siri Ya Kupata Mafanikio Makubwa Kila Siku.

No comments :
Kuna wakati katika maisha yetu huwa ni watu wa kujihisi hatujisikii kufanya jambo fulani au hatujisikii kufanya kile tunachokifanya. Hii ni hali ambayo karibu kila mmoja wetu imeshawahi kumtokea. Mara nyingi hali hii inapotokea huwa haijalishi umakini ulionao au kiwango cha elimu ,ulichonacho inapotokea, hutokea tu bila kujali kitu.
Naamini umeshawahi kukutana na hali hii katika maisha yako. Kuna wakati ulipanga kuamka asubuhi na mapema lakini ulishindwa na kuruhusu kutawaliwa na usingizi. Kuna wakati pia ulijipa ahadi kwamba ni lazima utaweka kiasi fulani cha pesa kama akiba lakini ulishindwa pia kufanya hivyo, hili limekuwa ni  tatizo kubwa ambalo linakusumbua si wewe tu na wengine pia.
Lakini  kwa bahati mbaya sana wengi wanapokutana na hali hii ya kutokujisikia kufanya kitu hata kile ambacho kinawafikisha kwenye malengo yao hujikuta wakiahirisha na wengine kuacha kabisa mipango na malengo yao. Hili ndilo tatizo kubwa linalowafanya wengi washindwe kufikia mafanikio yao makubwa.
Kitu ambacho unatakiwa ukumbuke siku zote kila inapotokea hali ya kutokujisikia kufanya kitu fulani jaribu kujiuliza hivi, mafanikio makubwa huwa yanapatikana vipi? Ukichunguza utagundua mafanikio yote makubwa yanapatikana kwa kuchukua hatua kila siku hata kama hatua hizo ni ndogo sana lakini lilokubwa ni kuchukua hatua na kusonga mbele.

JITUME KILA SIKU.
Watu wote wenye mafanikio huwa ni watu wa kufanya kila siku bila kujali wanajisikiaje. Vinginevyo wangekuwa ni watu wa kujisikilizia kwamba wafanye au wasifanye basi wasingekuwa wamefikia hapo walipo. Hata pale walipokutana na changamoto au kuchoka na kujihisi kabisa hawajisikii kufanya walijikaza na kuchukua hatua.
Kwa hiyo inapotokea siku umeamka asubuhi na kujikuta hujisikii kufanya jambo fulani kwa siku  hiyo husika, dawa sio kuacha wala kuahirisha, dawa yake ni kufanya  hivyohivyo hata kama matokeo ya haraka huyaoni. Kwani hivyo ndivyo mafanikio makubwa yanavyopatikana. Ili ufanikiwe unahitaji kujituma kweli na kuvumilia hata pale mambo yanapokwenda vibaya.
Kama utaendelea kuwa mtu wa kujisikia kufanya mambo yako, basi elewa utakwama kwa mambo mengi sana. Kwa kifupi, hutafanikiwa. Kwa kuwa umelijua hilo hakikisha unajitoa kweli kufanikisha mipango yako, haijalishi unajisikiaje. Hivyo, Ili uweze kufaniwa na kuondokana na hali hiyo ya kutokujisikia kufanya,unaweza ukafanya mambo haya machache yatakuwa msaada mkubwa kwako:-
1. Amka asubuhi na mapema kila siku na fanya jambo moja la muhimu sana kwako kila siku litakalokusaidia kufikia mafanikio, hata kama utakuwa hujisikii kufanya lakini hakikisha unalifanya jambo hilo.
2. Tumia muda mchache kila siku kufikiria malengo na mipango yako hata kama hujisikii kufanya hivyo. Kwa kadri utakavyoendelea kujijengea tabia hii utajikuta unagundua mikakati na mbinu mpya za kuweza kukufanikisha.
3. Kuwa na nidhamu kila siku. Msingi mkubwa wa mafanikio yako upo kwenye kujijengea nidhamu. Unatakiwa uwe na nidhamu kwenye maeneo mbalimbali kama nidhamu ya muda au pesa.
4. Jiwekee akiba nyingi ya kutosha kuliko unavyojisikia kuweka. Akiba hiyo itakusaidia kuwekeza pale pesa yako itakapokuwa nyingi na imeongezeka.
5. Jiwekee mipango ya miezi kumi, mwaka mmoja au miaka mitatu. Fanya hivyo hata kama ndani yako hujisikii kufanya hivyo.
Kwa kufanya mambo hayo yatakupa nguvu na hamasa kubwa ya kufanya mambo yako bila kujali hali gani inaendelea ndani mwako. Kumbuka siku zote mafanikio ni kama mwendo.
Na kitu chochote kikiwa kwenye mwendo, kama kanuni ya mwendo inavyosema  kitaendelea kuwa kwenye mwendo vivyo hivyo. Kwa hiyo usizuiliwe na kutokujisikia. Kama tulivyotangulia kusema, kama kuna jambo unataka klifanya, lifanye hivyohivyo hata kama hujisikii. Uwe na uhakika kwa kadri utakavyokuwa unafanya ndivyo utazidi kufikia mafanikio yako makubwa.
Acha kupoteza mafanikio yako kwa kufanya mambo kwa kujisikia. Chukua hatua ya kuamua kwamba sasa wewe ni mtu wa vitendo na hutafanya tena mambo kwa kujisikia. Siri ya kupata mafanikio makubwa ni kuendelea kufanya bila kujali ni nini kinachoendelea kwenye akili yako.
Nikutakie siku njema na mafanikio mema,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nasi kwa:-
Simu; 0713 048 035,

No comments :

Post a Comment