Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, January 14, 2016

Mambo Ya Msingi Ambayo Ni lazima Uyajue Katika Biashara Yako.

No comments :
Habari za siku mpenzi msomaji wangu wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO. Bila shaka naamini umzima wa afya na unaendelea kuchota maarifa bora kabisa ya kukusaidia kufikia mafanikio uliyojiwekea. Kumbuka siku zote kujifunza ni msingi mkubwa sana wa mafaniko yako.
Leo katika makala yetu tutajifunza jinsi ambavyo unavyoweza kuifanya biashara yako kuwa ya mafanikio kwa kuangalia mambo ya msingi kabisa ambayo ni lazima uyajue. Kwa kutambua mambo haya itakuwa chachu kubwa kwako ya kukuwezesha kuendelea mbele.
Bila kukupotezea muda naomba nikutajie mambo ya msingi ambayo ni lazima uyajue katika biashara yako.
1. Kusukuma mambo ambayo hayaendi sawa.
Siku zote katika maisha mambo huwa hayendi sawa kwa asilimia mia moja kama tulivyokuwa tukitegemea. Inapotokea mipango au malengo yako hayajaenda sawa, kitu kinachofuata kwako ni kutumia mbinu zote na kuhakikisha mipango hiyo inaenda sawa kama ilivyopangwa na siyo tena kuacha.
Kwa hiyo unapoona mipango yako haiendi sawa, jukumu la kwanza hakikisha unatafuta njia nyingine mpaka kila kitu kikae vizuri. Kwa mfano inapotokea wateja unaona wamepungua jukumu ambalo unatakiwa uwe nalo siyo kuacha hivyo bali ni kutafuta wateja popote walipo mpaka kufanya kila kitu kiwe sawa ikiwa ni pamoja na kutoa matangazo.

KUWA KING'ANG'ANIZI WA MALENGO YAKO.
2. Kuwa king’ang’anizi wa malengo yako.
Najua kuna malengo ambayo ni lazima utakuwa umejiwekea kwenye biashara uliyonayo. Labda unaweza ukawa umejiwekea malengo ya baada ya muda fulani biashara yako itakuwa imefikisha ukubwa huu au itakuwa ina mtaji wa kiasi fulani. Haya ni malengo mazuri sana ambayo kila mtu anatakiwa awe nayo ili biashara yake iweze kukua.
Lakini kwa bahati mbaya kama niliyotangulia kusema hapo awali mambo siku zote huwa hayaendi sawa kama tunavyotaka. Kuna wakati ni lazima tukutane na changamoto. Inapotokea changamoto yoyote kwenye biashara yako, jaribu sana kuwa king’ang’anizi wa malengo yako mpaka ndoto zako zitimie. Acha kuyumbishwa na changamoto hizo na mwisho wa siku ukaacha malengo yako muhimu.
3. Penda kile unachokifanya.
Itakuwa ni ngumu sana kufanikiwa ikiwa ndani yako huna mapenzi sana na kile unachokifanya. Uzoefu unaonyesha hivi mara nyingi wengi wanaofanikiwa wanapenda yale wanayoyafanya. Unapokuwa unapenda kile unachokifanya inakuwa ni rahisi sana kwako kusonga mbele hata pale unapokutana na vizuizi vya hapa na pale.
4. Jiandae vizuri.
Silaha mojawapo ya kukufanya ufanikiwe katika biashara yako ni kufanya maandalizi mazuri. Unapojiwekea maandalizi muhimu ikiwa pamoja na kujua mapema changamoto unazokutana nazo katika biashara au washindani wako itakusaidia kufanikiwa kwa kiwango cha juu katika biashara yako. Kumbuka siku zote mafanikio yanatokea hasa pale maandalizi mazuri yanapokutana na fursa.
Kwa mambo hayo manne ukiyajua, yatakujengea msingi mzuri wa kufikia mafanikio makubwa katika biashara yako.
Nakutakia siku njema na mafanikio makubwa yawe kwako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nasi kwa:-
Simu; 0713 048 035,


No comments :

Post a Comment