Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, March 13, 2017

Jenga Tabia Ya Kujiuliza Maswali Uishi Maisha Unayotaka.

No comments :
Ili kubadilisha maisha yako na kuwa bora, unahitaji kujenga tabia ya kujiuliza maswali yatakayokusaidia kubadili maisha yako. Kila wakati jiulize ni njia au kwa namna gani ambavyo utaweza kuboresha maisha yako na kuwa ya mafanikio.
Acha kujiuliza kwa nini ‘mimi sina hiki au kile,’ badala yake jiulize nitawezeje kupata kile ninachokihitaji. Ukiwa unajiuliza hivi kila siku unapata msukumo wa kukusaidia kupata kile unachokihitaji maishani mwako.
Jiulize kila wakati, je, usipobadilisha hali ya maisha yako sasa na ikaendelea hivyo, maisha yako yatakawaje baada ya miaka mitano au kumi. Na pia jiulize maisha yako kifamilia, kiuchumi na kimahusianao yatakuwaje baada ya miaka mitano.
Njia rahisi ya uhakika na yenye nguvu kubwa ya kubadilisha maisha yako ni kujiuliza maswali. Unaweza ukawa upo kwenye hali ngumu sana ya kimaisha lakini kama unajiuliza maswali ya nitatoka vipi hapa nilipo, ni lazima utafanikiwa.
Kwa kawaida unapojiuliza maswali juu ya jinsi ya kubadilisha maisha yako na kuyafanya bora, vipo vitu viwili ambavyo vitakutokea;-
1. Utabadili mtazamo wako na kile kitu unachokitaka.
Kwa mfano, kama unajiuliza kila wakati, nitafanyaje ili nifanikiwe katika jambo hili? Hapo ni lazima mawazo yote na akili zote zitakuwa kwenye kutafuta njia itakayokusaidia kupata jibu hilo.

Hoji na ujiulize kila kitu kwenye maisha yako.
2. Itakuwa rahisi kwako kupata rasilimali za kukusaidia kufanikiwa.
Kwa jinsi unavyoendelea kujiuliza jinsi ya kuboresha maisha yako, utashangaa ukipata watu wa kukusaidia kutimiza ndoto zako. Watu wengi wanashindwa kujiuliza maswali kwa sababu ya kuona haiwezekani tena.
Kujiuliza maswali ni utaratibu mzuri sana ambao utakufanya ufikiri tofauti na kubadili maisha yako kwa sehemu kubwa.
Unapoinza siku yako kila siku anza kujiuliza maswali kama hivi;-
 a) Kitu gani ambacho nimejitoa kukifanya kwa moyo wote katika maisha yangu yote, bila kujali nalipwa au si lipwi na mtu. Sababu ipi inayonifanya nikifanye kitu hicho?
 b) Kitu gani ninachojivunia katika maisha yangu mpaka sasa? Kama kipo vizuri, kama hakipo nachukua hatua gani na mimi kuwa na vitu vichache vya kujivunia?
 c) Kitu gani ninachokifurahia sana, katika maisha yangu? Kwa nini nakifurahia kitu hicho?
Unapoimaliza siku yako yaani jioni, jiulize pia hivi:-
 a)   Kitu gani ambacho nimekitoa katika siku ya leo, ambacho kimekuwa msaada kwa wengine. Kipi nilichokitoa ili kuboresha maisha ya wengine?
 b)   Kitu gani ambacho nilichojifunza leo na kinamsaada mkubwa sana  kwa maisha yangu yote?
 c)   Na kwa jinsi gani siku ya leo imeongeza thamani ya maisha yangu? Je, imekuwa ni siku ya faida kubwa kwako na kubadili kwa sehemu, maisha yako?
Endelea kujiuliza maswali mengi tena na tena kwa kadri unavyoweza tena na tena, utashangaa maisha yakibadilika. Mafanikio sio ajali, ni kujifunza mbinu mbalimbali za mafanikio kama hivi.
Tunakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa,
Endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
DAIMA TUPO PAMOJA NAWE MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 04 80 35,

No comments :

Post a Comment