Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, September 17, 2015

Mambo 7 Yakukusaidia Kutunza Muda Wako Vizuri.

No comments :
Matumizi mazuri ya muda ni moja kati ya changamoto kubwa sana inayotukabili wengi wetu. Mara nyingi imekuwa ikitokea kwa wengi wetu karibu kila siku, kujikuta tuna mambo mengi ya kufanya ukilinganisha na muda tulionao. Kutokana na mambo hayo kuwa mengi, mipango yetu mingi pia hujikuta imekwama na kushindwa kuendelea kutokana na ukosefu wa muda.
Lakini hata hivyo, pamoja na changamoto zote hizo za ukosefu wa muda, kwa wengine bado hubaki kuwa ni watu wa kupoteza muda katika maisha yao. Nikiwa na maana kuwa, wanakuwa ni watu ambao hawajali sana kupoteza muda wao na pia hata wanakuwa wanawapotezea wengine muda hivyohivyo. Najua umeshawahi kuwaona watu wa namna hii katika maisha yako wasiojali thamani ya muda.
Hawa ni watu ambao huishi maisha yasiyo na mafanikio sana kutokana na kupoteza muda mwingi sana katika maisha yao. Kitu cha muhimu hapa kujua ni kuwa muda ni kitu cha  thamani sana kuliko kitu chochote duniani. Mafanikio yote yanategemea muda. Unapopoteza muda wako ni sawa na kupoteza mafanikio yako. Sasa jiulize kama wewe unapoteza muda unategemea nini katika maisha yako?
Ili uweze kufanikiwa na kuwa tajiri ni lazima kujifunza kutumia muda wako vizuri tena sana. Watu wote wenye mafanikio makubwa ni watumiaji wazuri wa muda wao kuliko unavyofikiri. Kinachowatofautisha wao na wewe ni matumizi ya muda tu na sio kitu kingine. Hiyo yote inaonyesha siri kubwa ya mafanikio ipo kwenye muda. Kitu kingine cha kujiuliza tena  je, unataka kutunza muda wako na kujijengea mafanikio ya kudumu? Kama jibu ni NDIYO.
Yafuatayo Ni Mambo 7 Yakukusaidia Kutunza Muda Wako Vizuri.
1. Weka vipaumbele vya kila siku.
Ili uweze kuepuka muingiliano wa mambo ni lazima kujifunza kuweka vipaumbele vya kila siku. Andika mambo ya lazima ambayo unatakiwa uyafanye kwa siku hiyo husika bila kuacha kitu. Hilo litakusaidia kutopoteza hovyo muda wako ulionao kwa sababu kila kitu kitakuwa kwenye ratiba yake na muda wa kukifanya.

2. Jiwekee malengo.
Kama utakuwa unajiwekea malengo hiyo itakuwa ni silaha ya kukuwezesha kutumia muda wako vizuri pia. Kwa sababu utakuwa unajua kabisa baada ya muda fulani unatakiwa uwe umetekeleza kitu hiki ama kile. Wengi wanaopoteza muda mara nyingi ni watu ambao hawana malengo hata yale ya siku moja tu. Na kwa sababu hiyo kwao muda kupotea ni kitu ambacho hakikwepeki.
3. Fanya mambo machache kwa uhakika.
Ni rahisi sana kwako kupoteza muda kama utajikuta unataka kafanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Hii ni kwa sababu utashika hiki mara kile na kujikuta hakuna ulichokifanya zaidi ya kurukaruka. Ili kufanikiwa jifunze kufanya mambo machache kwanza ikiwezekana jambo moja tu. Hiyo itakupa ufanisi wa kutunza muda wako vizuri sana.
4. Weka kumbukumbu ya muda wako.
Ili uweze kujua muda wako unautumiaje, ni vizuri kujiwekea kumbukumbu ya muda wako jinsi unavyoutumia. Unaweza ukaona ni kitu kama cha kijinga lakini ikifika siku kitakusaidia kujua tathmini ya wapi hasa unapopoteza muda wako mwingi ili kama ikiwezekana ujirekebishe. Kwa kujiwekea kumbukumbu ya muda wako uwe na uhakika utaweza kumiliki na kuutawala muda wako vizuri sana kwa mafanikio.
5. Kuwa makini na mambo yanayokupotezea muda.
Kuna mambo ambayo wengi wetu huwa yanatupotezea muda bila sababu. Jiulize ni kitu gani ambacho kinakupotezea muda sana. Je, ni mitandao ya kijamii, simu, mpira au ni kitu gani? Ukishajua kitu kinachokupotezea muda sana, tafuta njia nzuri namna ya kupunguza matumizi hayo. Acha kupoteza muda wako hovyo kwa kitu ambacho hakikupi faida ya moja kwa moja, badala yake linda na tunza sana muda wako kwani hapo ndipo mafanikio yako yalipo.
6. Jifunze kusema HAPANA.
Wengi huwa wanajikuta ni watu wa kupoteza muda wao pengine kutokana na kukubali vitu vingi bila kujiuliza kwa nini walikubali. Kabla hujasema ndiyo kwa jambo lolote la makubaliano jiulize linawezekana? Kama hutajifunza kusemaHAPANA hii itakufanya uzidi kupoteza muda wako mwingi wa thamani siku hadi siku bila ya wewe kujua. Kama huelewi kitu ni bora ukasema HAPANA kuliko ukafanya na ukaacha, hiyo itakuwa ni kupoteza muda.
7. Wape wengine majukumu.
Kama pengine kuna jambo ambalo unataka kulifanya wewe, lakini ukagundua wapo watu ambao wanaweza wa kakusaidia katika jambo hilo ni vizuri ukawapa wakafanya. Hiyo itakusaidia kufanya majukumu mengine zaidi na isitoshe utakuwa umeokoa muda wako mwingi. Acha kung’ang’ania kufanya mambo yote wewe, wape na wengine wakusaidie majukumu hayo ili kuokoa muda wako. 
Kumbuka, muda ni kitu cha thamani sana ambapo ukijenga tabia ya kuutumia vizuri utakuwezesha kufikia mafanikio makubwa yanajitokeza katika maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika matumizi bora ya muda wako na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
 Imani Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.  


 


No comments :

Post a Comment