google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Sep 22, 2015

Jinsi Unavyoweza Kuwavuta Watu Unaokutana Nao.

No comments :
Kwa nguvu zake Mungu naamini umzima wa afya na unaendelea kujifunza kupitia DIRA YAMAFANIKIO ili kuboresha maisha yako. Leo napenda nianze makala hii kwa kukuuliza swali hili, ni kwa nini baadhi ya watu, wakikutana na mtu kwa mara ya kwanza tu, mtu huyo waliyekutana naye ‘anaboreka’ haraka? Na ni kwa nini wengine, wanapokelewa kirahisi na watu wapya wanaokutana nao maishani?
Najua, unajua kuna sababu nyingi. Lakini ningependa nikutajie moja tu, ili iweze kukusaidia kukabiliana na ‘kuwaboa’ watu wengine. Na tumia neno ‘kuboa’ kwa sababu ni neno ambalo limezoeleka kimatumizi kwa sasa, likiwa na maana ya kumfanya mtu asiwe na haja ya kukusikiliza au kuwepo kwako hukera, wewe ukiwa ndiyo chanzo.
Kama umekutana na mtu kwa mara ya kwanza, usizungumze sana kuhusu wewe, usijizungumzie kwa kujisifu na kujipandisha sana. Ingawa haina maana kwamba usijishushe. Usitake kuonesha kwamba wewe ndiye wewe.
Watu wasiojitosha, huwa wanakawaida ya kujisifu sana, wanataka kuwavuta wanaozungumza nao wawaone wa maana sana, huzungumza kwa muda mwingi wao tu, hujisifu na kujikweza. Ni mara chache sana huwaacha wengine waseme.
Hebe fikiria, hujamjua mtu, unasema kama kinanda kuhusu mambo yako, unadhani atakuchukulia vipi? Ni lazima utamkera tu, badala ya kumfurahisha, kama unavyofikiria. Ni lazima utaanza kuwa na wasiwasi nawe.

Jambo la awali unalotakiwa kulifanya unapokutana na mtu mgeni, ambaye hujawahi kukutana naye, iwe kibiashara, kimapenzi au kwa nasibu tu, inabidi uwe msikilizaji tu kuliko kuwa msemaji.
Kuna watu ambao wanatatizo la kutaka kusikilizwa wao tu, amablo chimbuko lake ni kushindwa kwao kupata watu waliowajali walipokuwa wadogo.
Kama nawe ni mmojawapo, inabidi uwe mwepesi kujikumbusha kwamba, una tatizo la kutaka kusikilizwa wewe tu. Kujikumbusha au kukumbuka, kutakusaidia kuamua kumsikiliza mwingine badala ya wewe kusema.
Siku zote wanaopenda kusikiliza badala ya kusema, hao ndiyo mara nyingi huwa wanawavutia watu, siyo wale wanaopenda kusema sana. Wengi hawalijui sana jambo hili.
Ni vizuri unapokutana na mtu mgeni, ukasema kidogo uhusu wewe, yaani yale mambo ya msingi tu yanayokuhusu. Sema tu yale ambayo ni ya lazima au muhimu. Usiwe kasuku kwanza.
Halafu, soma kama huyo mtu ambaye humjui, ndiyo kwanza mnakutana, anavutwa na mazungumzo gani? Unaweza ukaanza kubwata siasa wakati hataki kusikia kabisa mambo yanayohusiana na siasa zako hizo. Unaweza ukaanza kubwata kuhusu vifo, wakati pengine wiki iliyopita tu kapoteza mkewe au mumewe ama mtu wake wa karibu kabisa.
Ukijua mtu au watu wa fulani ambao ndiyo kwanza unakutana nao wanafurahia kuungumzia mambo gani, hutawakera. Kwako itakuwa rahisi pia kuwasikiliza, kwani huenda watakuwa na mengi, kwani wanazungumza yale wanayoyapenda na pengine wanajua zaidi.
Unapokutana na mtu mgeni popote na mazingira yakakulazimisha muwasiliane, siyo vibaya ukaanza kwa kujitambuisha kwa kujitaja jina.
Hii humjengea mtu huyo mwingine kukuamini na kuhisi ukaribu na urafiki.  Onesha kwamba, mtu huyo mgeni anapozungumza unafurahia mazungumzo yake. Unaweza kutabasamu, kumtazama bila kukodolea macho na kutikisa kichwa mara kwa mara.
Hata kama ikitokea mtu huyo anaongea upuuzi, ni vema kujenga uhusiano wa karibu na mtu huyo. Wacha mgeni aseme zaidi ili umjue zaidi kuliko wewe anavyokujua.
Kumjua kwako zaidi kutakusaidia kujua uzungumze vipi naye na kwa sababu zipi. Lakini, usijaribu kuwa mtu ambaye siyo wewe. Kuwa wewe kwa kujikubali, bila kujipandisha wala kujishusha.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya mafanikio yako na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
 Imani Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka. 

No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.