Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, June 26, 2015

Hizi Ndizo Athari Za Kuwa Na Maumivu Makali Kihisia.

No comments :
Nakumbuka ni hivi karibuni ambapo  ilikuwa ni majira ya jioni na nilirudi nyumbani tofauti na kawaida yangu. Siku hiyo niliamua kupitia jikoni kama kituo change cha kwanza. Nilipoingia jikoni nilimwona binti ambaye huwa tunakaa naye  akiwa  ameinamia kwenye beseni la kuoshea vyombo hapo jikoni.

Nilimsemesha na aligeuka kuniangalia bila kunijibu chochote. Mikono yake alikuwa ameiweka ndani ya beseni kama kuficha kitu lakini hata nilipomwangalia nilihisi kama alikuwa analia hivi. Nilipomsogelea na kutazama mikono yake, nilipatwa na mshtuko sana. Alikuwa ameshika kisu na mkono wake wa kushoto ulikuwa ukitoka damu. Ilionesha alikuwa amejikata.

Nilipomuuliza ni kwa nini anafanya vile huku nikiwa nimetundikiwa, alinitazama tu huku machozi yakimtoka. Siyo siri niliogopa sana. Baada ya tukio lile niliamua kumuulizia daktari kwa ufafanuzi zaidi alionipa  ndipo nilipojua hasa kuhusu jambo lile ambalo lilipelekea binti yule kuweza kujiumiza.


Ilinibidi kwa kweli, nimpeleke hospitali na tatizo nililokuja kuambiwa na daktri ni tatizizo  linalotokana hasa na mtu kukata tamaa, kuchangiwa na kuamua kujiadhibu kwa kujiumiza. Bila shaka tunajua kwamba, kukata tamaa kunapozidi na mtu anapohisi kuwa maisha hayana maana, anaweza kujiuwa.

Nilijifunza yote  hayo kutokana na tatizo alilokuwa nalo binti yangu huyu. Kujiumiza huku kunaweza kuwa ni kwa kujikata mikono, miguu au sehemu nyingine ya mwili. Wakati mwingine inaweza kuwa kwa kuvuta nywele , ung’ata kucha kwa nguvu, kujipiga au kujichubua au kukwaruza hata kidond ambacho hata kilikuwa karibu kupona.


 Ingawa siyo tatizo kubwa , kwani inakadiriwa  ni mtu mmoja tu kila mia moja anakabiliwa nalo, bado hii ni idadi kubwa ya kutosha. Ina maana kwaba kwa hapa nchini kiasi cha watu 440,000 wanakabiliwa na tatizo hilo.

Pamoja na ukubwa wa tatizo hilo kwa bahati mbaya hakuna mtaalamu ambaye hadi sasa amewahi kusema  kwa hakika tatizo hilo linatokana na nini hasa. Lakini angalau inafahamika kwamba ni juhudi ya anayejiadhibu kutaka kujihisi ahueni ya kimaisha angalau kwa muda fulani.

Bila shaka tumewahi kushuhudia au kusikia kuhusu watu wanaojikwangua, wanaojiumiza, wanaojibamiza ukutani, wanaopanda mitini na kujiangusha ili wavunjike kwa kuamini kuwa wanapata ahueni kwa kufanya hivyo. Kama tumewahi kushudia au kusikia, hii yote ni sehemu ya tatizo hili.

Mara nyingi kujiadhibu huku hufanywa kwa siri sana na wahusika. Kwa hiyo wakati mwingine inakuwa vigumu kuona kuwa anajiadhibu,  bali tunaweza kuona matokeo yake. Mtu anaweza kuona kidonda kipya kwenye mwili wa mtu au kuona nywele zimevurugwavurugwa ghafla tu ama dalili nyinginezo.

Kwa bahati mbaya, hawa watu wanaojiumiza wenyewe, ni mara nyingi huwa hawajui ni kwanini wanajiumiza, hujiumiza kwa sababu huhisi wakifanya hivyo watapata nafuu. Lakini nafuu ya nini, huwa ni swali gumu kupatiwa majibu.

Bado hata hivyo, ukweli unabaki kwamba, wanafanya hivyo kwa sababu wana maumivi kihisia. Kwa hali hiyo, kama inatokea mtu anagundua kwamba, jamaa yake ameingia mahali ambapo anajiumiza mwenyewe kwa njia yoyote, inabidi ajaribu kumsaidia akijua ni tatizo la kihisia.

Nimeshawahi kusikia kuhusu watu amao wamepelekwa kwa waganga wa asili kwa sababu ya tatizo hili. Kufika huko wakaambiwa wana wana jini anatafuta damu na kuanza kutibiwa kwa kutaka kumtoa jini huyo, hali ambayo iliwazidishia maumivu kihisia hadi wakaamua kujiua. Kumbe ambacho hawakujua  kujiumiza huko siyo majini wala nini bali hizo ndizo athari za kuwa na maumivu makali ya kihisia.

Tatizo la mtu kujiumiza mwenyewe kwa lengo la kupata nafuu, halihusiani na kulongwa au nguvu nyingine za giza. Ni tatizo ambalo kisaikolojia linaelezeka kabisa. Ingekuwa halijanipata, ningeweza kusema, huenda lina nguvu za giza ndani yake kama wengi wanavyofikiri. Lakini nimelishuhudia moja kwa moja na nalijua vizuri.

Tunakutakia kila la kheri, endelea kujifunza kila siku bila kuchoka kwa kupitia mtandao huu wa DIRA YAMAFANIKIO lakini hakikisha unawashirikisha wengine ili kuweza kujifunza zaidi.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,No comments :

Post a Comment