Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, June 19, 2015

Mambo 6 Yakukusaidia Kusonga Mbele Wakati Unapoona Mipango Yako Haiendi sawa.

No comments :
Habari za leo mpenzi msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO tunaamini ya kuwa umzima na unendelea vyema na harakati zako za kuboresha maisha yako. Karibu tena mahali ambapo unapata tena nafasi nyingine ya kuweza kujifunza mambo muhimu yanayoboresha maisha yako kwa ujumla.

Katika makala yetu ya leo tutaangalia mambo muhimu yatakayoweza kukusaidia kuweza kusonga mbele pale ambapo unaweza ukaanza kuhisi umekwama au huendi mbele sana kama ambavyo unataka ikutokee katika maisha yako. Kuna wakati katika maisha yetu huwa tunajikuta yale mambo ambayo tunayafanya yanakuwa kama hayasogei ama kuna kuzuiliwa fulani hivi.

Hali hii inapotokea kwa wengi huwa wanahisi kukata tamaa na kushindwa kujua nini cha kufanya. Kiuhalisia, unauwezo wa kusonga mbele zaidi katika maisha yako haijalishi ni nini kinachokutokea katika maisha yako. Uwezo wa kuishi maisha ya ndoto yako unayoyataka unao na hilo linawezekana kikubwa kwako ni kuchukua hatua ya kuamua kuwa hilo linawezekana.

Kama nguvu ya maamuzi na uwezo wa kusonga mbele unao ni kipi kinachokukatisha tamaa na kuona kuwa huwezi kusonga mbele tena? Ni vizuri kwako ukaweza kukumbuka mambo muhimu yanayoweza kukusaidia katika kipindi kigumu ambacho unahisi mipango yako haiendi sawa. Huu ni uamuzi wako ambao unaweza kuufanya sasa ili kuweza kubadilisha maisha yako. Mambo yapi ya kukusaidia Kusonga mbele?

Haya Ndiyo Mambo 6 Yakukusaidia Kusonga Mbele Wakati Unapoona Mipango Yako Haiendi sawa.

1. Tambua Ni wakati wa kufanya mabadiliko.
Hili ni jambo mojawapo muhimu sana la kukumbuka ambalo litakusaidia kusonga mbele ikiwa utaelewa kuwa unahitaji kufanya mabadiliko tena ya haraka. Mambo yako kutokwenda vizuri hiyo ni ishara tosha kwako kuwa ipo sehemu kuna tatizo. Inawezekana ukawa unatumia muda vibaya ama unafanya matumizi ya pesa vibaya ambayo yanakukwamisha kila mara.

Kwa kujiangalia na kujichunguza kidogo unaweza ukagundua hilo. Ukishapata majibu hutakiwi kuchelewa ni kuanza kufanya mabadiliko mara moja. Kwa kufanya mabadiliko hayo utakuwa umejiweka kwenye nafasi nzuri ya kuweza kuzidi kusonga mbele. Kinyume cha hapo utakuwa unajikwamisha wewe mwenyewe. 2. Unahitaji kuwajibika zaidi.
Kama mambo yako unaona kabisa hayasogei ama yanataka kwenda hovyo, unahitaji kujituma zaidi. Huu ndiyo ukweli ulio wazi ambao naweza nikakwambia kuwa ni lazima  uukumbuke mapema na uufuate vinginevyo utakuwa unajidanganya mwenyewe. Huhitaji kulaumu mtu, hali ama serikali ndiyo iliyokufikisha hapo, zaidi kama unataka kufanya hivyo jilaumu wewe.

Maisha yako ni yako mwenyewe. Hakuna mtu wa kumtwisha mzigo wa lawama zaidi yako mwenyewe. Inatakiwa uifikie mahali pengine ukubaliane na ukweli kuwa unahitaji kutumia nguvu nyingi sana katika kuwajibika na siyo kulaumu. Kama wewe utabaki tu unalaumu nakupa uhakika hautaweza kufanikiwa hata ufanye nini.

3. Unahitaji kusahau yote yaliyopita.
Inawezakana ukawa unakwama katika maisha yako kutoka pengine na kukumbuka sana matukio yaliyotokea nyuma. Kama ndivyo hivyo ilivyo kwako achana na hali hiyo na ujifunze kusahau kila kitu ili kuweza kusonga mbele na kufanikiwa zaidi. Hautafanya kitu kama utakuwa ni mtu wa kukumbuka tu yale ya nyuma zaidi.

Watu wengi ambao huwa wanakwama wengi wao huwa wanatabia hii ya kushikilia sana vitu vya nyuma kitu ambacho ni hatari sana kwa maisha yao. Kumbuka kuwa tunafanikiwa kwa kufanyia kazi mipango tuliyonayo sasa na siyo iliyopita. Kwa maana hiyo acha kujenga kumbukumbu hasa zile mbaya ambazo zilipita, sahau kisha songa mbele.


4. Kuwa mvumilivu.
Kwa mabadiliko yoyote ambayo huwa tunayataka yawe katika maisha yetu huwa ni lazima yanahitaji uvumilivu tena wa hali juu. Unaweza ukawa unaona kama mambo yako yametulia lakini kumbuka ni vyema ukajipa uvumilivu fulani hivi ambao utaweza kukusaidia kusonga mbele.

Wakati unavumilia huko kwa kujipa muda, lakini hata hivyo kumbuka kutafuta hasa kujua nini hasa sababu ambayo inaweza ikawa imepelekea mambo yako yasiende kwa kasi kama ulivyotarajia. Ukiweza kuigundua hiyo sababu fanya mabadiliko muhimu yanayotakiwa na kisha songa mbele.

5. Kuwa mtu wa vitendo.
Badala ya kukaaa chini na kuanza kuwa na visingizio kuwa umekwama pengine kutokana na hili hiyo tabia achana nayo, badala yake kuwa mtu wa vitendo. Visingizio vyako havitaweza kukusaidia chochote zaidi utashangaa vinakukuwamisha hata wewe mwenyewe bila kujielewa.

Kama unataka kufanya kitu kitakachokupa mafanikio katika maisha jifunze kutafuta njia na siyo visingizio kama unavyofanya. Ni wakati umefika wa kufanya madiliko katika maisha yako na siyi tu visingizio kila mara. Mtu anayekurudisha nyuma sana katika maisha yako ni wewe mwenyewe. Ukiwa mtu wa vitendo na kuachana na visingizio utafanikiwa.


6. Simamia maisha yako mwenyewe.
Acha kuwa na tabia ya kuruhusu sana watu wengine waingilie maisha yako. Ni vizuri kuwa na mpaka katika maisha yako. Siyo na maanisha usiwe mtu wa kutokushaurika, hapana. Sikiliza maoni kama umuhimu upo kisha fanyia kazi yale unayoona yanakufaa.

Lakini usije ukaruhusu ama ukajiona mkosefu ikitokea wamekukosoa eti ulikosea sana hili na lile ndiyo maana husongi mbele. Jifunze kusimamia maisha yako wewe kama wewe, pia kuwa na msimamo wako ambao unaweza kukusaidia kusonga mbele na siyo kubeba kila kitu ili kuwaridhisha wengine hiyo itakwa siyo nzuri na haifai kabisa.

Kumbuka kuwa, kwa vyovyote vile iwavyo wewe ndiyo mtu wa mwisho wa kutengeneza maisha yako kwa jinsi unavyotaka iwe. Kwa pale unapohisi mambo ama mipango yako haikuendei sawia kama ulivyokuwa ukitaka unaweza ukarejea katika mambo hayo muhimu kwako.

Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa maarifa bora, lakini usikose kuwashirikisha wengine kwa ajili ya kujifunza zaidi.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,

No comments :

Post a Comment