Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, June 11, 2015

Kama Hujui, Akina Misifa Wote Hutafuta Kile Walichokosa Utotoni.

No comments :
Na Deogratius Gunju, Mbeya.
Kuna wakati nilipouwa nikisomea ualimu siku za nyuma, nilikwenda kwenye shule moja ya sekondari wakati wa kile tulichokiita field, yaani mazoezi kwa vitendo. Nilipangiwa darasa ambalo kwa pale shule, mkondo huo huwa darasa ni kwa wale wasio na uwezo kimasomo. Ilikuwa ni darasa la C.

Kwa kweli ile siku ya awali tangu kuanza mafunzo ya ualimu wa diploma, ilitaka kunifanya nichukie Ualimu.  Na chanzo ilikuwa ni mwanafunzi mmoja ambaye kwa kweli aliniendesha.

Mwanafunzi huyu alikuwa ‘mjuaji’ sana, kwani kila nikifundisha, yeye alikuwa akizungumza au kujigeuza mara huku mara kule . Awali nilijifanya sioni, lakini baadaye ilibidi nimuulize sababu ya kufanya vile. Badala ya kujibu kwa adabu alibetua mdomo na kusema, ‘basi yameisha, endelea.’

Hadi kumaliza kipindi cha dakika 40 nilikuwa nimechoka, nilipotoka hapo darasani, nilikwenda kusoma kuhusu saikolojia ya watoto zaidi. Nilikuja kugundua kuwa, mwanafunzi Yule alikuwa akitafuta au kutafuta wengine wamjali, akitaka kukubaliwa na wengine, akitafutwa kuonwa na wengine na uwepo wake kuthibitika.


Niliposoma pia sababu za mwanafunzi kama yule kutafuta wengine kuweza kumjali sana kwa kiwango kiasi kile. Nilijitahidi kusoma ili niweze kujua namna ya kuweza kumsaidia au kwenda naye vizuri bila kukwaruzana.


Ukweli ni kwamba, kila mmoja wetu anapenda kuona wengine wakimjali au kumkubali, lakini tunaweza kusema wengine kumwona. Kutaka wengine watujali ni jambo muhimu sana kwa karibu kila binadamu. Kuna wataalamu wanaodai kwamba, hitaji hili ni muhimu, sawa kabisa na chakula au hewa maishani.

Kila mmoja wetu, hujitahidi sana kutafuta wengine wamjali au kumwoa kwa njia mbalimbali , bila kujali kama anaita jambo hilo kutafuta wengine kumjali au anaita vingine. Lakini, pale haja ya wengine kutujali au kutuona, kutambua uwepo wetu mahali inapopindukia mipaka, hapo tunasema kuna tatizo.

Siyo tu yule mwanafunzi aliyenichefua siku ile ya kwanza kwangu kuingia darasani, bali kuna watu wengi ambao hutafuta sana kuonwa na wengine, hutaka wengine kuwajali na kutambua uwepo wao.

Kuna watu ambao hukera sana kwa sababu ya kile kitu ambacho tunakiita kutaka au kutafuta sifa. Hawa ni watu ambao wanapenda kuonwa wao ni wa kwanza kwenye kundi la watu na wanataka watu wengine wawatambue au kuwajali wao zaidi.


Unaweza kukuta watu wote kwenye kundi wamekubaliana na mawazo ya mtu Fulani. Lakini mtu mmoja tu ndiye atakayebisha, tena kwa nguvu sana. Siyo kwamba anabisha kwa sababu mawazo yake yana mantiki, hapana, hayana kitu chochote, bali anachotaka yeye ni sifa, ili watu wamtambue kwamba yupo.

Kuna watu ambao hawajahusishwa kwenye mazungumzo ya watu wengine, lakini hujiiingiza kwenye mazungumzo hayo na kuyanunua, hasa kama ni mazungumzo ambayo yatawafanya watu wengi kuwasikiliza. Hebu jaribu kuchunguza abiria kwenye mabasi ya daladala mijini, kuna watu ambao huwa wako tayari kununua ugomvi usiowahusu ili watu wengine wawaone kuwa wapo.

Kuna watu wengi ambao hubisha chochote, mahali popote, siyo kwa sababu wanajua zaidi au wanaleta  mawazo mapya, hapana. Hubisha kwa sababu, wengine wajue kwamba wapo.

Watu hawa, ni matokeo ya malezi mabovu au ya wazazi ambao hawakuwa wakijali kuhusu watoto wao. Watoto wanapokuwa kwenye umri fulani na hasa kuanzia miaka miwili (Kwa wenye uwezo mkubwa kiakili) huanza udadisi na pia kutafuta kufanyiwa tathimini kwa kile wanachokifanya katika maisha yao hayo ya utotoni.

Mtoto anaweza kupanga maboksi na kumwita mama au baba kutazama alivyofanya. Wakati mwingine mzazi ana shughuli zake na hivyo kumpuzia mtoto. Hii inapotokea sana, mtoto hukua akiwa anatafuta mtu wa kumjali, mtu atakayeonesha kwamba, anajua kuwa amefanya jambo fulani.


Kwa hiyo, mwalimu anapofundisha darasani, kijana husukumwa na kutaka kufanya jambo ili usikivu kwa wengine uweze kwenda kwake. Anajaribu kwa nguvu zote kutafuta kile ambacho baba au mama yake hakumpa utotoni, yaani kujali alipohitaji mtu wa kumjali kwa kile anachokifanya.

Tukikutana na mtu wa aina hii tusikasirike sana kwa sababu, hata yeye yuko kwenye moto, anaumia, anatafuta ahueni, ndiyo maana anahangaika kwa kiasi chote hicho. Tunaweza kuzungumza naye kwa upendo kumwelimisha kwamba, hapaswi kuwa hivyo na kumwelezea sababu za yeye kuwa hivyo.

Wazazi, kwa hali hiyo wanashauriwa kuwa makini zaidi katika namna wanavyowatendea watoto wao. Mtoto akimwambia mzazi, ‘baba, ona nimjenga nyumba,’ inabidi mzazi aangalie na kusema jambo, hasa kumpa moyo. Anapompuuzia, ndipo ambapo kasoro kama hizi huweza kuzaliwa.

Tunakutakia kila la kheri katika safari ya mafanikio, ansante kwa kuwa msomaji mzuri wa DIRA YAMAFANIKIO, endelea kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza zaidi.

UNAWEZA KUWASILIANA NA MWANDISHI WA MAKALA HII DEOGRATIUS GUNJU KWA 0718 610 022


No comments :

Post a Comment