Jun 19, 2015
Haya Ndiyo Mabadiliko Ya Lazima Unayotakiwa Kuyafanya Sasa Ili Kufanikiwa.
Hakuna mtu ambaye anapenda
kuona maisha yake yakienda hovyo ama akiwa hana kipato cha kutosha. Kila mtu
mpenda mafanikio huwa ana nia ya kutaka kufanikiwa na kuona mambo yake yakienda
sawa kama anavyotaka iwe kwake. Lakini maisha hayo ya mafanikio huwa hayawezi kuja
hivihivi tu, ni lazima kuwe na mabadiliko ambayo yanatakiwa kufanyika.
Kwa kufanya madiliko hayo
muhimu ni lazima kwa vyovyote vile maisha yako yatabalika. Acha ile tabia ya kukaa
na kuanza kulalamika, unachotakiwa kufanya wewe ni kuleta mabadiliko
yatakayokutoa sehemu moja na kukupeleka nyingine na siyo kulalamika. Haya ndiyo
mabadiliko unayotakiwa kuyafanya katika maisha yako. Je, ni mabadiliko gani
kwako ya lazima ambayo unatakiwa kuyafanya ili kufanikiwa zaidi?
1.
Kuwa mtu wa vitendo.
Kitu kitakachoweza
kukufanikisha na kukutoa hapo ulipo ni kwa wewe kuwa mtu wa vitendo. Watu wengi
ambao hawana mafanikio huwa ni watu ambao ni waongeaji sana juu ya ndoto zao
lakini si watendaji. Mabadiliko unayotakiwa kuyafanya wewe ni kuwa mtendaji, hata
kama ni kwa kidogo wewe tenda na acha kuahirisha mipango yako mara kwa mara. Kwa kuwa mtu wa vitendo ni lazima
uone mabadiliko.
2.
Kuwa king’ang’anizi.
Katika safari ya kutafuta
mafanikio mara nyingi huwa tunakutana na vikwazo vingi ambavyo vingine
hutukatisha tamaa sana. Lakini lilokubwa kwako ni kuwa king’ang’azi kwa
kushikilia ndoto zako mpaka kuona zinaleta majibu. Kama umefika mahali umekwama
acha kukataa tamaa mapema jipe moyo kisha zidi kusonga mbele, safari bado
inaendelea na fanya mabadiliko haya ya kuwa king’ang’azi utaona mabadiliko.
3.
Kuwa na mipango inayoeleweka.
Katika hili ili uweze
kufanikiwa hakikisha uwe unajua unatoka wapi na unakwenda wapi na kwa muda
gani. Hakikisha uwe unajua ni nini unachotakiwa ufanye kwa siku, wiki, mwezi na
hata mwaka ili kutimiza malengo uliyojiwekea. Haya yote yatawezekana kwa
kupangilia vizuri. Haya ni mabadiliko ya lazima unayoyahitaji kwani bila
utaratibu huu utakuwa unaishi hovyo na itakuwa ngumu sana kwako kufikia malengo
yako.
4.
Kuwa makini na afya yako.
Wengi huwa ni watu ambao
hawaelewi sana juu ya hili. Kitu cha pekee ambacho kinaweza kukusaidia kufikia
ndoto zako ni afya yako. Kama utakuwa na afya mbovu, hata uwe na ndoto nzuri
vipi huwezi kuzifikia. Kwa hiyo kitu cha kuangalia hapa ni kutunza afya zetu
ili ziweze kutusaidia kufikia malengo tuliyojiwekea. Hakikisha unajikinga na
magonjwa kwa jinsi unavyoweza na kula chakula kizuri chenye afya.
5.
Kuwa na mitizamo chanya.
Hii ndiyo siri kubwa ya
mafanikio kwa wajasiriamali wengi. Bila kuwa na mtazamo chanya katika maisha
yako halafu ukawa tu unazidi kukomaa kuwa unataka mafanikio hiyo takuwa ni sawa
na kujidanganya wewe mwenyewe. Unapojenga mtazamo chanya hakuna kitachokuzuia
kuelekea kwenye njia ya mafanikio. Ili kufanikiwa unalazimika kuwa mtu chanya
kwanza, ambaye utaona mabadiliko kwako yanawezekana.
6.
Kuwa na mahusiano na watu sahihi.
Watu wanaokuzunguka ni
muhimu sana katika mafanikio yako. Kama umezungukwa na watu wengi matajiri ni kiwa
na maana wenye mafanikio ni rahisi sana kwako kufanikiwa. Hii yote ni kwa sababu utakuwa unajifunza kwao
mambo mengi ambayo yatakufanya na wewe ufanikiwe hivyo hivyo. Ni muhimu sana
kukagua marafiki ulionao kama wanakusaidia kukufikisha kwenye ndoto zako au
wanakurudisha nyuma?
Hitimisho.
Kwa kufanya mabadiliko hayo
utakuwa umejiweka katika nafasi nzuri ya kuweza kufanikiwa zaidi kattika maisha
yako. Na ni mabadiliko ambayo yataweza kukutoa kutoka sehemu moja kwenda sehemu
nyingine.
Ansante kwa kutembelea
mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO na endelea kuwashirikisha wengine kuweza
kujifunza zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA
MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI
NGWANGWALU,
0713
048035,
dirayamafanikio@gmail.com.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.