Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, November 28, 2016

Tumia Mbinu Hizi Ili Uweze Kuishi Ndoto Yako.

No comments :
Tuanze kwa kujiuliza je hilo ambalo unalifanya ni la kwako au ni la mtu mwingine? Je kama si ndoto yako unahisi ni lini utaishi ndoto yako? hivi hupendi watu watu wajifunze kupitia kwako?.

Usinipe majibu, nimeona ni vyema tuanze na kujiuliza maswali hayo kwani ni ya msingi sana, na majibu yake yatadhihirisha kuwa umekuja duniani kwa lengo la kutimiza ndoto zako na si ndoto wengine, hata pale unaposema Mwenyezi Mungu bariki kazi mikono yangu baraka hizo zikujie moja kwa moja. 

Zifuatazo ndizo mbinu za kuzitumia ili kuishi Ndoto zako.

1. Usipoteze Muda kwa vitu visivyo vya msingi.

Mara kadhaa tumekuwa tukitumia muda mwingi kwa vitu ambavyo vimekuwa si lolote kwetu. Tumeshindwa kufanya tathimini ya kutosha juu ya ndoto zetu tulizonazo, tumekuwa tukiishi ndoto ambazo si zetu, tumekuwa tukiishi maisha ya wengine.

Mara nyingi tumekuwa tukilalama bila kutoa sauti ya kwamba maisha ni magumu, na muda mwingine tumekuwa tukidiliki hata kusema ya kwamba dunia hii haina usawa, yote hayo hutokea hasa pale tunaposhindwa kufanikiwa, huku tukisahau ya kwamba wengi wetu tunafanya vitu vya watu wengine.

Usipoteze muda kufanya vitu visivyo vya maana kwako, ishi kwenye ndoto zako.

Hivi hujawahi kuona ya kwamba mtu ndoto yake ilikuwa ni Kuwa muigizaji na leo hii ni fundi mjenzi? Unadhani nini ambacho kimesababisha hali hiyo kutokea? Usinipe majibu.

Ila nikusihi ya kwamba dunia hii inahitaji mtu ambaye anaishi ndoto zake, hivyo kila wakati unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unaishi ndoto zako kwa kuzingatia lile likusukumalo kutoka nafsini mwako, usibadili mwelekeo wa kutimiza ndoto zako eti kwa sababu maisha ni magumu, eti kwa sababu ya ndugu, jamaa na marafiki. 

Amini ya kwamba ndoto zako zinawezekana, na hivyo anza kuishi ndoto zako sasa kabla ya kuifikia ndoto hiyo, kama unataka kuwa mwalimu anza kuifundisha jamii ambayo inakuzunguka sasa,  ukifanya hivi hautautumia muda mwingi kufanya vitu visivyokuwa vya maana kwani utakuwa umeanza kuishi ndoto zako. Mafanikio hayana kesho anza leo.

2.Usikubali kukatishwa tamaa.

Kuishi ndoto zako ni moja ya kitu kikubwa ambacho naamini unakitafuta katika maisha yako. Lakini wengi wetu, hushindwa kufikia ndoto hizo hii Ni kutokana na mazingira ambayo yanamzungumka mtu huyo. Lakini ipo siri ambayo wengi hawaijui ni kwamba siku zote kuwa wewe, usiwe wao.

Inawezekana ukawa hujanielewa ni hivi wengi hukatishwa tamaa na watu wengine, na kwa kuwa wewe hupagawishwa zaidi na aina hiyo ya watu unajikuta unaliacha jambo unalolifanya na kuanza jambo jingine, lakini kabla sijaweka nukta katika muktadha huu nikwambie ya kwamba chagua fungu lililo bora acha kukatishwa tamaa na watu ambao hawana msaada wowote.

3. Uwe tayari kupokea ushauri na kuufanyia kazi.

Dunia hii imejaa watu wa aina tatu, wapo wale washauri, wapo wakatishaji tamaa, wapo wale ambao wanasubiri wewe uanze kufanya jambo fulani ili na wao waanze kujifunza kupitia kwako, wala usijali hii ndio dunia bwana, unachatakiwa kufanya ni kujifunza kutoka kwa aina hizo zote tatu.

Lakini kujifunza huko si kila jambo la kuchukua mambo mengine yaache kama yalivyo,  ila jifunze yale mambo ya muhimu kutoka kwa washauri sahihi hasa wale ambao wanafanya mambo ambayo yanafanana na ndoto zako.

Najua kila kitu katika kujifunza kina changamoto zake unachotakiwa kufanya si kukata tamaa bali ni kupambana mpaka mwisho ili ujue hatima ya maisha yako.

4. Jifunze kwa waliofanikiwa.

Maisha ni kujifunza, si kujifunza tu bali kujifunza kitu kipya, kujifunza kitu kipya pekee yake haitoshi bali unatakiwa kukiweka katika matendo, kama utaamua kujifunza pekee yake haitakusaidia kitu.

Ni vyema kila wakati ukajua thamani ya kufanyia kazi kile ulichojifunza. Mabadiliko ya kitu chochote yanatokana na wewe kujua kitu kipya, haitawezekana hata siku moja eti unataka kutimiza ndoto zako kama haupo tayari kujifunza.

Mara kwa Mara wanasema hakikisha unajifunza kwa watu ambao wamefanikiwa, watu hawa wawe ambao wana mfanano wa ndoto zako.

Mwisho afisa mipago niweke nukta kwa kusema ya kwamba kutimiza ndoto zako inawezekana kabisa endapo utaamua kuchukua maamuzi ya kuanza kuchukua hatua ndogondogo siku leo. Maana mafanikio ni Leo wala si kesho.

Ni wako rafiki katika Mafanikio;
Afisa mipango Benson Chonya

No comments :

Post a Comment