Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, November 17, 2016

Unahitaji Mambo Haya Manne Basi, Ili Kutimiza Malengo Yako.

No comments :
Siku zote hakuna uchawi au miujiza mkubwa sana unaotakiwa uwe nao ili uweze kutimiza ndoto zako. Suala la kutimiza ndoto zako ambazo umejiwekea mara nyingi linakuwa lipo mikononi mwako.
Ki vipi hili linawezekana? Na hapo inakuwaje kuwaje? Sikiliza, utaweza kutimiza ndoto zako ikiwa unajua misingi au mambo ya muhimu yatakayokusaidia kutimiza ndoto hizo. Hapo ndipo ilipo siri ya kutimiza ndoto zako.
Najua una hamu na shauku kubwa sana ya kutaka kuona ndoto zako zinatimia na kuwa kweli. Kama hiyo iko hivyo usiwaze sana na wala hilo lisikupe shida. Je, unajua ni mambo gani unahitaji ili kutumiza ndoto zako?
Unahitaji mambo haya manne basi, ili kutimiza malengo yako.
1. Kukijua vizuri kile unachokitaka.
Kuna wakati wengi wanaanza kutafuta safari ya mafanikio pasipo kujua vizuri hasa, kile wanachokitaka. Huwezi kufanikiwa kama hukijui vizuri kile kitu unachokitaka.
Kwa mfano nikiulize, wewe binafsi hapo unakijua vizuri kile unachokitaka katika maisha yako? Je, unajua baada ya miaka miwili au miaka mitano unatakiwa uwe wapi kimafanikio? Ni lazima ukijue unachokitaka.
Inapotokea hata wewe mwenyewe binafsi hukijui vizuri kile unachokitaka, si rahisi sana kufanikiwa. Siri kubwa ya kufikia ndoto zako na kufanikiwa ipo kwenye kukijua vizuri kile unachokitaka.

Tekeleza ndoto zako kila siku.
2. Kuwa na sababu.
Kukijua tu kile unachokitaka, hiyo pekee haitoshi, ni lazima uwe na sababu. Lazima ujue kwanini umejiwekea hayo malengo? Kwanini unataka kufanya hicho unachotaka kufanya?
Unapokuwa na sababu za kujua kwa nini unafanya hicho unachotaka kufanya hiyo inakuwa ni motisha na nguvu ya kuweza kukusaidia kuweza kusonga mbele. Kila unapokumbuka sababu za kufanya hicho unachofanya, hata kama umechoka ni lazima utaamka na kwenda kupiga kazi.
Wewe tafuta sababu kwa nini unafanya hicho unachokifanya sasa? Kama huna sababu, elewa tu ni lazima kwa sehemu utakuwa ni mzembe sana na hutaweza kufikia malengo yako. Nguvu kubwa ya kufanya zaidi, utaipata ukishakuwa na sababu ya kufanya hicho unachokifanya.
3. Fanya kila siku.
Ndoto zako huwezi kuzifikia ikiwa hutaweka juhudi ya kufanya kila siku. Ni lazima kuweka juhudi na kufanya kila siku hata kama kipo kipindi ambacho unakuwa umechoka.
Kwa jinsi unavyofanya kila siku, juhudi zako zitakwenda kuweka matunda. Watu waliofanikiwa, kila siku wanajitahidi kuweka juhudi zao kila siku hadi kutumiza ndoto zao.
Kitu unachotakiwa kujiuliza, je, upo tayari kupiga kazi kila siku hata kama kuna wakati unakuwa umechoka? Ikiwa utafanya hivyo, anza kujijengea uhakika mkubwa wa kufikia ndoto zako.
4. Tafuta msaada.
Si vyema sana ukakomaa na ndoto zako peke yako, wakati upo uwezekano wa kutafuta msaada kwa wale waliofanikiwa kwa hicho unachokifanya. Jifunze kutoka kwao na waulize nini siri ya mafanikio yao.
Acha kuwa mbinafsi na kukubali kufa na tai shingoni kama mjerumani. Watu wenye mafanikio wana hulka na tabia ya kuuliza kwa wale waliowazidi kwa yale wanayoyafanya bila shida yoyote.
Ukianza leo kuuliza na kutafuta msaada juu ya ndoto zako, utafika mbali sana kimafanikio , tofauti na ambavyo ungebaki kimya kimya. Anza kubadili fikra zako na kuwa na mtazamo wa tofauti ili uweze kutimiza ndoto zako.
Kila wakati zingatia hivi, kukijua vizuri kile unachokitaka, kuwa na sababu juu ya ndoto yako, kutekeleza ndoto zako kila siku na kutafuta msada kwa wale waliofanikiwa, ni nguzo kubwa sana ya kukusaidia kufanikiwa kwa ndoto na malengo yako.
Nakutakia ushindi katika kufikia mafanikio yako makubwa.
Endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
0713 04 80 35,

 
No comments :

Post a Comment