Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, November 18, 2016

Ili Ufanikiwe zaidi, Unahitaji Kuishi Na Watu Hawa.

No comments :
Katika kufikia mafanikikio makubwa unayoyatafuta, ieleweke wazi wapo watu ambao ni lazima sana uwe nao kwa karibu ili uweze kujifunza kwao na hadi kufanikiwa.
Kumbuka, sisi ni matokeo ya watu watano wanaotunzunguka. Kama unazungukwa na watu watano ni maskini, basi ni wazi upo uwezekano hata wewe kuelekea kwenye njia hiyo ya umaskini.
Mpaka hapo unaona upo ulazima wa wewe kuwa na watu sahihi  kila wakati kwenye maisha yako ili ufanikiwe. Usipate shida sana kujiuliza ni watu gani hawa ambao na unatakiwa kuwa nao ili kufanikiwa?
Ili ufanikiwe zaidi, unahitaji kuishi na watu hawa.
1. ‘Mentors’/Washauri.
Kwa chochote kile unachokifanya, wapo watu ambao wamekutangulia na wanakifanya kitu hicho tena kwa mafanikio. Watu hawa, ikiwa utajifunza kwao na kuwafanya wakawa ndio taa yako ya mafanikio, utafanikiwa.
Hawa ndio watu wa kuishi nao karibu kwa kuwafanya kuwa ‘Mentors’ wako au washauri wako wa karibu wa mafanikio. Hiyo iko hivyo kwa sababu njia unayotaka kupita wao tayari wameshaipita. Hivyo ni rahisi sana kukuelekeza.
Inawezekana unakwama kwenye maisha kwa sababu huna ‘mentor’ au hata mlezi mmoja wa mafanikio ambaye unamfuata. Sasa kama unaishi hivyo, sio rahisi sana kufanikiwa. Ni lazima uwe na mtu anayekuongoza kufikia mafanikio yako.
Unaweza ukawa unajiuliza sasa nitawapata wapi? Kama ni watu wenye pesa mbona wako ‘bize’ sana? hilo lisikupe shida,  jifunze kupitia kazi zao wanazotoa kama vile vitabu. Hapo utapata mawazo yao yote na ushauri wao kwa karibu sana.
Pata mshauri wa kukuza kipaji chako.
2. Watu wenye uzoefu kwa kile unachokifanya.
Mara nyingi wengi wetu tunakuwa tunapotea na kukosea sana kwenye maisha kwa sababu ya kuishi au kuzungukwa  na watu ambao si wazoefu sana na kile tunachokifanya.
Kwa mfano utakuta mtu ana duka la vipodozi, lakini ana shauriwa sana na watu ambao muda wote ni wafanyabiashara wa nguo. Hiyo pekee tu ni kosa ambalo  linakufanya kufanikiwa kwako isiwe rahisi.
Ili uweze kutoka kimaisha, jifunze kuwa na watu ambao wana uzoefu na jambo unalolifanya.  Watu hao watakusaidia sana kukuonyesha njia sahihi ya kufikia mafanikio yako kwa haraka. Ili kufanikiwa kwa hili usijifanye mjuaje, kuwa mpole kubali kujifunza.
3. Watu wanaokufanya ufikiri zaidi.
Pia mbali na ‘mentors’ na watu wenye uzoefu, watu wengine ambao unahitaji kukaa nao karibu sana ili wakusaidie kufikia mafanikio ni watu wanaokufikirisha zaidi.
Ni hatari sana kukaa na watu ambao hawakupi changamoto za kimaisha. Ni lazima uishi na watu ambao kila kukicha ni kama wanawasha kichwa chako ‘moto’ kutokana na changamoto wanazokupa.
Unapokuwa na watu hawa watakutia hasira na utafanya kazi kwa mwehu ili kuhakikisha unafanikiwa zaidi na zaidi. Maisha yako kumbuka yanataka changamoto ili yaweze kufanikiwa. Hivyo ni lazima kuwa na watu hawa.
4. Watu wanaosikiliza.
Kuna watu ambao katika maisha ni wabishi karibu kwa kila kitu. Hawa ni watu ambao hata wakielekezwa kitu kidogo wao hukimbilia kwenye kubisha. Ikiwa hutawajua watu hawa watakupotezea muda sana.
Kitu cha kufanya, epuka watu hawa na ishi na watu ambao wanasikiliza. Ishi na watu ambao mnaendana. Ikiwa kila mtu anakuwa ni mbishi jiulize  hayo mafanikio yatapatikana vipi?
Kwa kuhitimisha makala haya, naomba ieleweke hivi, wapo watu ambao unatakiwa uwe nao karibu, unatakiwa uishi nao ili uweze kufanikiwa. Na hao ndio watu unaotakiwa kuishi nao kama tulivyowajadili kwenye makala haya.
Endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku kwa ajili ya kujifunza na kuboresha maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
0713 04 80 35,

No comments :

Post a Comment