Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, October 26, 2015

Jinsi Unavyoweza Kufanya Jambo Ambalo Hujisikii Kulifanya.

No comments :
Maisha yanakuwa na maana na mazuri kwetu kama tunafanya yale mambo ambayo tunayapenda na kuyatamani. Inapotokea unakuwa unafanya jambo ambalo hulipendi au hujisikii mara nyingi mambo yanakuwa magumu sana. Ni kitu ambacho huwa kinatokea, unakuta tu, hujisikii kufanya jambo fulani ambalo pengine ni muhimu kwako.
Je, inapokutokea unataka kufanya kitu halafu ukawa hujisikii hapo unakuwa unafanyaje? Je, unakuwa unaacha na kuendelea na mambo mengine au kuna hatua unakuwa unachukua? Yapo mambo mengi unayoweza ukawa unajifikiria, lakini ukweli wa mambo ni kwamba, zipo njia unazoweza kuzitumia kufanya jambo ambalo hujisikii kulifanya.
Zifuatazo Ni Njia Ambazo Unaweza Kuzitumia Kufanya Jambo Ambalo Hujisikii Kulifanya.
1. Anza kwa kidogo.
Kama ni jambo ambalo hujisikii kulifanya anza nalo kwa kidogo. Kama wewe ni mwandishi unataka kuandika kitu na unahisi hujisikii, anza na sentensi moja kwanza, hiyo itakupa nguvu ya kuendelea zaidi. Na katika maeneo mengine ya maisha yako unaweza ukatumia mbinu hiyohiyo, kwa kuanza na hatua ndogo katika kila jambo.

ACHA KUKATA TAMAA, ANZA KUFANYA MARA MOJA.
2. Usiruhusu akili yako kuogopa sana.
Kuna wakati ni rahisi kujisikia huwezi kufanya jambo fulani kwa sababu ya woga ambao unakuwa umeujenga kwenye akili yako. Mara nyingi akili inapokuwa na woga wa aina fulani inakuwa siyo rahisi kufanya jambo lolote hata iweje. Ili kufanikiwa katika hili, kwa vyovyote vile usiruhusu akili yako ikawa na woga wa kupitiliza, kwa mfano woga wa kuweza pengine hutaweza kufanikiwa.
3. Jipe muda wa kujifunza.
Inawezekana unashindwa jambo hilo kwa sababu hujalijua vizuri zaidi. Kama ni hivyo jipe muda wa kujifunza na kulielewa jambo hilo kwa undani. Hii itakusaidia kuanza kulifanya huku ukiwa na hamasa kubwa ambayo itakusaidia wewe binafsi kuweza kulifanya jambo lako na kuweza kusonga mbele kimafanikio.
4. Acha kuahirisha.
Pamoja na kuwa upo ugumu fulani wa kutokujisikia kulifanya jambo hilo, dawa pekee ya kuweza kulifanya ni jifunze kutoweza kuliahirisha jambo hilo. Lianze hivyohivyo hata kama ni kwa kidogo, hata kama huku ukiwa unahisi kama mwili  hautaki, lakini kikubwa usiahirishe. Kwa kadri utakavyozidi kufanya bila kuahirisha utajikuta unazidi kuongeza hamasa ya kulifanya zaidi na zaidi.
Kwa kifupi, hizo ndizo njia ambo unaweza ukazitumia kufanya lile jambo ambalo kwako hujisikii kulifanya.
Tunakutakia siku njema na mafanikio makubwa yawe kwako siku zote. Na kumbuka endelea kujifunza kila siku bila kuchoka.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nasi kwa:-
Simu; 0713 048 035,

No comments :

Post a Comment