google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Oct 1, 2015

Kwa Nini Watu Wengi Hutapeliwa Kirahisi?

No comments :
Kwa kawaida kila jamii ina tabia za jumla kama ilivyo kwa mtu mmoja mmoja. Kila jamii ina tabia na haiba zake, ambazo zinaitofautisha na jamii nyingine. Inaweza kuwa maringo na kiburi, kuchapa kazi kwa bidii, ukarimu na nyingine za aina hiyo.
Watanzania kwa mfano, wanasifiwa kwa ukarimu, ambapo pia kuna wakati ukarimu huo umetafsiriwa kama ni ujinga. Hatuna uhakika, kipi ni kipi kati ya hivyo viwili. Lakini sifa ambayo jamii ya Tanzania ni ya wazi kabisa ni ile ya kutokujiuliza maswali linapokuja suala la fedha mbele yao.
Pamoja na kipato kigumu kwa Watanzania wengi, lakini wakitajiwa kuwekeza na kuvuna kirahisi, kila mtanzania anaweza kupata fedha na bila hata kujua alikozipata na alivyozipata. Ni vigumu siku zote Mtanzania kupata mtaji, hata mdogo tu, na ndicho kilio cha kila Mtanzania kila siku.
Lakini, inapotokea nafasi ya kuwekeza mahali ambapo kuvuna ni kwa haraka na wingi sana Mtanzania hupata mtaji wa kuwekeza hapo. Kama anakopa, ananyang’anya au kudhulumu, hakuna ajuaye, lakini, mara nyingi, fedha anayoitaka ataipata na atawekeza. Mfano ni upatu.
Unapotangazwa upatu wa kuvuna haraka na kwa wingi, akili ya Mtanzania inashindwa kufanya kazi na kuanza kuweweseka kwa kutafuta fedha za kucheza upatu huo. Huwa hajiulizi inakuwaje fedha ije kirahisi kwa kiasi hicho, ilimradi wahusika wana ofisi na wanatoa risiti kwa malipo yanayofanywa, kwao hiyo huhalalisha kila kitu.

Kwa bahati mbaya sana, hata wasomi humizwa kwenye ulaghai huu ambao hupitia kwenye mwavuli wa upatu au mikopo nafuu. Kuna vikundi vingi vya kukopeshana na kucheza upatu, ambavyo hutangaza kwamba, vina vibali vya serikali na vimeandikishwa, ambavyo vimekuwa vikiwaumiza sana watumishi wa serikali na hata sekta binafsi .
Naamini umeshawahi kusikia mmbo kama haya ya kiendelea katika jamii zetu mara kwa mara. Kitu ambacho huwa najiuliza sana, hawa wenzetu wanakuwa wana nini hasa hadi kukubali kuingia katika mkenge wa kudanganyika kirahisi na kupoteza akiba zao hata ndogo walizojiwekea.
Hebu jaribu kuchunguza, utagundua kumekuwa na taarifa nyingi za kiutapeli kwa namna na mtindo uleule, kiasi kwamba, kila kitu kiko wazi kwa kila mtu ni namna gani hawa matapeli wanafanya kazi zao. Lakini, bado unakuta watu wanatapeliwa kila siku, asubuhi na jioni. Ni kama vile, watu hawana kumbukumbu na kile kinachotokea au ni kama vile wanaposikia kupata fedha kirahisi, ufahamu  wao unafyatuka.
Umefika muda ambapo tuna haja ya kujiuliza, ni kwa nini wengi wetu au Watanzania wanatapeliwa kirahisi kiasi hicho?  Bila shaka, Tanzania ni nchi pekee ambapo mtu anaweza kuiba kwa hila kwa njia ileile hata mara kumi, mahali palepale.
Bila shaka, tatizo siyo umaskini, na kama ni umaskini, basi umaskini huo ni wa kufikiri zaidi kuliko wa fedha. Kama ni umaskini wa kufikiri na siyo wa fedha, inabidi watu au jamii ianze kujiuliza, ni kwa namna gani itafikia mahali pa ukomavu? Na ukomavu huo itaupata tu kwa kujifunza kila siku kupitia vitabu na hata semina ili kuondokana na kutapeliwa huko.
Ni wakati wa kuchukua hatua sasa za kubadili maisha yako na kuachana na fikra za kuamini yapo mafanikio rahisi zaidi. Kila mafanikio unayoyataka ni lazima uyalipie. Hicho kitu ndicho unachotakiwa kwa uwazi kabisa ili kujenga mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri katika harakati za kuboresha maisha yako na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
 DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
 Ni wako rafiki katika mafanikio,
 Imani Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.  


 


No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.