Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, October 14, 2015

Kabla Hujakata Tamaa, Jiulize Kwanza Maswali Haya.

No comments :
Kuna wakati katika maisha yetu mambo huwa magumu, hayaendi na kila tunachokifanya kinakuwa hakileti mafanikio kama tunayoyatarajia. Ni kipindi ambacho wengi kinakuwa kigumu sana na kinatupa mawazo ya kukata tamaa. Wengi wetu bila shaka tumewahi kupatwa na hali kama hii kwa namna moja au nyingine.
Kitu kikubwa cha kujiuliza unapokutana na hali hii ya kukatisha tamaa unafanyaje? Je, ni kweli unaamua kuachana na kitu hicho ambacho ulikuwa unakifanya au kuna njia mbadala utatumia kufanya kitu hicho kwa namna tofauti na kikakuletea mafanikio? Wengi mara nyingi inapotokea wakashindwa jibu la kwanza kwao huwa ni kukata tamaa.
Lakini pamoja na kukata tamaa huko, watu hao huchukua kitu kingine na kukianza kukifanya tena, lakini pia wanapokatishwa tamaa kidogo hujikuta wakiacha tena kitu hicho. Hivyo hujikuta wao ni watu wa kuanza na kuacha na mwisho wake hakuna mafanikio makubwa wanayoyapata. Hiyo yote ni kwa sababu hakuna mafanikio yanayokuja kwa kutaa tamaa kirahisi.Ili uweze kufanikiwa kwa vyovyote vile ni lazima uwe na roho ya ukakamavu ambayo itkufanya ushikilie mipango na malengo yako mpaka ifanikiwe. Chochote kile unachokitafuta huwezi kukipata kwa urahisi ni lazima ukilipie jasho vya kutosha. Kwa lugha nyingine hakuna mafanikio rahisi kama ulikuwa hujui hili. Na ndiyo maana kabla hujakata tamaa, anza kwanza kujiuliza maswali haya:-
1. Kitu gani kinachotaka kukufanya ukate tamaa?
Ni vizuri ukaelewa ni jambo gani linalokufanya utake kukata tamaa kwa sasa. Je, ni wasiwasi, woga, uzoefu au umekosa ujuzi fulani ambao kama ungekuwa nao usingeweza kukata tamaa. Ukishajua kinachokufanya ukate tamaa unaweza ukatafuta njia ya kuweza kukabiliana nacho ili kuondokana na hali hiyo inayokukatisha tamaa.
SOMA; Huna Haja Ya Kukata Tamaa, Mafanikio Yako Yanaanza Na Kitu Hiki.

2. Kitu gani kilichokufanya uanze jambo hilo?
Pia ni lazima kwako kujiuliza swali hili, wakati unaanza jambo hilo ni kipi hasa kilichokusukuma hadi ukalianza. Kwa mfano kama ni biashara ulikuwa unafanya lengo lako kubwa la kwanza lilikuwa ni nini? Kama lilikuwa ni kutengeneza faida na kuwasaidia watu, basi tumia msukumo uleule wa kwanza kusonga mbele badala ya kukaa chini na kukata tamaa.
3. Je, kukata tamaa ni majibu ya kila kitu?
Unaweza ukafikiri ukikata tamaa utakuwa umepata suluhisho la kile unachokiacha lakini sio kweli. Inawezekana kabisa kukata kwako tamaa kukakupelekea wewe kukosa kujifunza mengi likiwemo pamoja na uvumilivu. Kama kukata tamaa siyo jibu la kila kitu ni vyema ukaendelea na kile unachokifanya.
SOMA; Kama Unataka Mafanikio Makubwa Mwaka 2015, Acha Kukata Tamaa Tena katika Mambo Haya.


4. Je, unataka kukata tamaa kwa sababu nzuri au mbaya?
Kuna wanaokata tamaa kwa sababu ya maneno ya watu ambayo yamewavunja moyo, hawa sababu yao ni mbaya.  Pia kuna wanaokata tamaa kwa sababu kile wanachokifanya hakileti matokeo chanya, hawa sababu yao ni nzuri. Hivyo, ni muhimu kujiuliza unakata tamaa kwa sababu ipi? Kwa sababu za kijinga tu au sababu ipi hasa? Ukigundua kama ni sababu ya kijinga endelea kusonga mbele.
Kukata tamaa ni moja ya jambo ambalo linapeleea malengo ya wengi kutokufanikiwa. Kabla hujakata tamaa ni vizuri ukajiuliza maswali mengi zaidi ambayo yatakusaidia kuifikirisha akili yako, ikiwezekana uachane na mawazo hayo. Ukijiridhisha na ukagundua kweli kitu hicho hakifai kwako, basi unaweza ukaachana nacho kuliko ukajimiminia msingi wa zege kwenye maisha yako ambao unaweza ukakupoteza.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea DIRA YAMAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.
No comments :

Post a Comment