Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, October 21, 2015

Mbinu Tano Za Kukuza Biashara Yako.

No comments :
Kwa mapenzi yake Mungu naamini umzima wa afya na unaendelea kujifunza kupitia mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO. Nami bila hiana nakukaribisha tena katika siku nyingine ili uchote maarifa sahihi ya kuweza kukusaidia kubadili maisha yako. Ni maarifa hayahaya yatakayokusaidia kuboresha maisha yako kila siku na kwa nyakati tofauti.
Katika makala yetu ya leo tutaangalia namna unavyoweza kukuza biashara yako na kufikia viwango vya juu. Ikumbukwe kukuza biashara ni hitaji ambalo karibu kila mjasiriamali analitamani kulitimiza. Kama ni hivyo basi, unawezaje kukuza biashara yako? Hapa nimekuwekea mbinu muhimu za kukusaidia kukuza biashara yako hadi kufikia mafanikio makubwa.
1. Toa thamani.
Ili biashara yako iweze kuwa kubwa sana na inayokupa faida, haihitaji mtaji mkubwa sana kama unavyofikiri, inachohitaji ni thamani unayoitoa. Je, thamani unayoitoa inaendana na ile ambayo wateja wako wanaitaka? Kama kweli unatoa thamani halisi, kwa vyovyote vile lazima biashara yako ikue. Haijalishi mtaji ulionao, toa thamani bora utapata matokeo mazuri.
SOMA; Sababu Tano Kwanini Unatakiwa Kumiliki Biashara Yako Sasa?

THAMANI UNAYOTOA ITAKUPA MAFANIKIO MAKUBWA.
2. Kuwa na mahusiano mazuri na wateja wako.
Unaweza ukawa unatoa thamani inayotakiwa, lakini kama huna mahusiano mazuri na wateja biashara yako haitaweza kukua kwa kiwango kikubwa. Wateja ndio kila kitu kwenye biashara yako. Jitahidi hata kama kuna mteja amekukera mwonyeshe kumjali. Kwani hiyo itakujengea jina na kupelekea kuwa na wateja wengi wanaohitaji huduma yako.
3. Kuwa na usimamizi mzuri.
Wapo watu ambao huamua kuanzisha biashara na kuwaachia wengine wasimamie. Linaweza likawa jambo zuri, lakini linahitaji umakini kwa wasimamizi utakaowaweka. Kama watasimamia vibaya uwe na uhakika tayari umeua biashara yako. Hivyo, iwe unasimamia wewe au wengine, inabidi utambue usimamizi mzuri ni kitu ambacho kinahitajika sana ili kukuza biashara.
4. Tengeneza timu sahihi yakukusaidia.
Haiwezekani kila kitu ukafanya wewe kwenye biashara yako. Inabidi ifike mahali ambapo unatakiwa utengeneze timu bora itakayokusaidia kufikia malengo yako. Kipo kipindi ambacho unaweza ukawa unaumwa, au una dharura fulani. Je, katika hiki kipindi unafanyaje? Hapa ndipo unatakiwa uwe na timu au watu wa kukusaidia kukuza biashara yako pale ambapo dharua zinaweza zikajitokeza kwako, ili mambo yaende mbele bila kusimama.
5. Ongeza ukubwa soko lako.
Kama ulikuwa ni mtu wa kuuza bidhaa zako ndani ya mtaa mmoja, ni vyema ukaongeza ukubwa wa soko lako kwa kadri siku zinavyokwenda. Tafuta soko lingine, nje ya eneo ulipo. Utamudu hili lakini ikiwa utawaridhisha wateja wako wa kwanza ambao watakusaidia kukutangazia biashara yako, hali itakayopelekea biashara yako kuzidi kukua siku hadi siku.
Hizo ni baadhi ya mbinu ambazo unaweza ukazitumia ili kuboresha biashara yako na kufikia mafanikio makubwa. Je, una mbinu nyingine ambazo unafikiri zinaweza kutusaidia kukuza biashara na kufikia mafanikio makubwa? Unaweza ukatushirikisha hapo chini kwenye maoni, tukajifunza pamoja.
Dira ya mafanikio inakutakia siku njema na mafanikio makubwa yawe kwako siku zote. Na kumbuka endelea kujifunza kila siku bila kuchoka.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nasi kwa:-
Simu; 0713 048 035,
No comments :

Post a Comment