Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Tuesday, October 6, 2015

Kama Unayumbishwa Sana Na Kitu Hiki, Huwezi Kufanikiwa.

No comments :
Habari za leo rafiki na mpenzi msomaji wa mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO bila shaka umzima wa afya. Nakukaribisha katika siku nyingine tena ya kuweza kujifunza na kuboresha maisha yetu. Leo katika makala yetu, nitakusimulia kisa kimoja ambacho kinaelezea habari za mzee mmoja ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kuuza maandazi na nyama pembezoni mwa barabara siku zote.
Kutokana na kukosa elimu ya kusoma na kuandika mzee yule hakuweza kusoma magazeti, na pia kutokana na uhafifu wa macho na masikio yake yake hakuweza kutazama televisheni wala kusikiliza redio. Licha ya haya yote mzee huyu alijitahidi sana katika biashara yake na kujikuta mtaji wake unapanda na kuwa juu hata kufikia hatua ya kuuza maandazi na nyama hizo sehemu mbalimbali.
Mzee huyo akiwa anaendelea na shughuli zake  mtoto wake ambaye alikuwa mhitimu wa chuo kikuu aliamua kuangana na baba yake katika biashara hiyo. Mzee huyo alifurahi kupata msaidizi msomi ambaye aliamini atamsaidia sana katika suala zima la kupandisha  uchumi juu na hatimaye kufikia mafanikio makubwa kuliko yale aliyokuwanayo kwa wakati huo.
Siku moja mtoto huyo alikuja na wazo ambapo alimshauri baba yake akisema huko mbeleni uchumi utashuka kwa kiwango kikubwa kitaifa na kimataifa, hivyo ajihadhari. Yalikuwa ni maneno ambayo kwa baba yake hayakuwa mazuri sana . Kutokana na maneno hayo mzee huyu akaamua kupuuzia biashara yake na kuacha kuuza bidhaa zake sehemu mbalimbali kama mwanzoni.

Kitu pekee kilichopelekea mzee huyu kufanya hivyo ni kuogopa hali ya uchumi ambayo ilikuwa inaenda kubadilika muda siyo mrefu na kuwa mbaya kabisa. Hali hiyo ilisababisha wateja wake wengi kupungua sana na biashara yake ilifika mahali  ikafa na hali mbaya ya kushuka kiuchumi ikaanza kumkabili. Chanzo cha yote hao yalisababishwa na mtoto wake.
Ni kitu gani ambacho umejifunza kupitia simulizi hii? Naamini ni mengi. Lakini ikumbukwe, wengi wetu katika maisha ndivyo tulivyo. Huwa ni watu wa kupokea taarifa sana hata bila ya kuzifanyia uchunguzi huwa tunazifanyia kazi moja kwa moja au kuziamini. Kwa kufanya hivyo hujikuta taarifa hizi zikiua mipango na malengo yetu bila kujijua.
Ili uweze kufanikiwa huhitaji kupokea kila taarifa. Hata kama ikitokea umepokea taarifa hizo unatakiwa kuzifanyia uchunguzi kama ni za kweli kwako au la. Hiyo yote inatuonyesha ni muhimu sana kufikiri kabla ya kutenda na pia tusikate tamaa hata pale inapotokea tunapewa taarifa mbaya za kutukatisha tamaa.
Maisha ni kupanda na kushuka, kwa hiyo tunapoambiwa kuwa kuna mabaya mbeleni yanakuja, tusidharau wala kufa moyo kwa namna yoyote ile zaidi ‘tukazae buti’ ili kuyaepuka mabaya hayo nakufikia mafanikio makubwa tunayoyahitaji. Tusiwe wa kukatishwa tamaa na kukubali kama ilivyokuwa kwa mzee huyu kwenye simulizi yetu.   
Hivyo, kitu cha kuzingatia hapa ni kwamba kuwa makini na kile unachoambiwa. Kwa sababu kinaweza kukusaidia kukufanikisha au kuua ndoto zako kabisa ikiwa utakuwa mtu wa kukurupuka na kufanyia kazi kila jambo. Kuwa na misimamo yako itakayokusaidia kufanikiwa. Ila kama unayumbishwa sana na kitu hiki, huwezi kufanikiwa. Hakikisha taarifa yoyote isikuyumbishe, bali iwe msingi wa kuendelea mbele zaidi.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.No comments :

Post a Comment