google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Oct 16, 2015

Hizi Ndizo Athari Mbovu Za Malezi Kwa Watoto Wetu.

No comments :
Tumekuwa tukishangaa au kama siyo kushangaa, kukerwa na kuachiwa maswali na tabia hii. Inasemekana wasichana wa mijini wanadanganyika kirahisi sana zaidi kwa magari. Utakuta msichana anakubali kuwa na uhusiano na mwanamume kwa sababu amegundua kwamba, ana gari.
Lakini, wengine wanajua kabisa kwamba, gari siyo la huyo mwanamume, lakini hujikuta wakikubali kuwa na uhusiano naye kwa sababu ya gari tu. Ndiyo maana madereva wengi, hasa wale wa teksi wanajisifu kwamba, wanawake wanawapapatikia sana. Kuna ukweli wa aina fulani.
Lakini, je wasichana ni  wote ambao wanawapaptikia madereva au watu wenye magari? Ndilo swali gumu sana kwenye suala hili. Kila kitu kinachohusu uhusiano wa kimapenzi, tunajifunza kutoka kwa wazazi au walezi wetu, labda asilimia 10 tu ndiyo tunajifunza nje ya nyumbani.
Siyo suala la gari peke yake, bali ni suala la karibu kila kitu. Je watoto wetu tunawajengea dhana gani kuhusu kila kitu kwenye maisha? Halafu tunawaambia kitu gani kuhusu kupenda? Siku zote na tulio wengi, tunawaambia watoto wetu uongo mwingi sana.
Uongo huo unatokana na sababu nyingi. Kwanza, nasi tulidanganywa na wazazi wetu. Pili hatujiamini. Tatu, hatuna uhakika sisi ni akina nani na nne, tunadhani uongo huo utawasaidia watoto kuwapa moyo.

Hebu chunguza kwa makini, utagundua kwamba, wasichana wanaobabaikia magari ni wale ambao wamelelewa  kwenye malezi ya uongo mtupu.
Unaweza kudhani wale waliotoka kwenye familia maskini ndiyo ambao wanababaikia magari, hapana. Msichana anaweza kutoka kwenye familia maskini na asibabaikie utajiri wala mali ya mtu. Wako wengi wa aina hiyo.
Kama nyumbani, wazazi wanasifu wenye magari, wanaonesha kwamba, ukiwa na gari ndiyo unakuwa na maana, kwamba, gari ni kiwango cha juu cha mafanikio, unatarajia kitu gani kutoka kwa watoto? Kuna wakati wazazi wanasema, ‘ameshafika mbali siyo mwenzio, yule ana akili bwana. Ana magari mawili na nyumba tatu’
Wakati mwingine inatosha mara moja tu jambo kusemwa na mzazi na mtoto kuamini, kwamba, mwenye gari au magari na nyumba, ndiye aliyekamilika, ndiye mwenye akili.
Kumbuka, mtoto anaingiza akilini mwake maarifa kutoka kwa watu anaowaamini na anaokutana nao maishani. Kwenye suala la uhusiano, wazazi ndiyo wanaoaminika zaidi.
Kwa sababu ya umaskini wetu tulio wengi, gari na nyumba ndiyo tunayoyachukulia kuwa ni malengo ya juu kabisa kuyapata. Kwa hiyo mtoto anakuwa ana akili ya aina hiyo , kigezo chake kuhusiana na mtu kitakuwa ni gari na nyumba au mali kwa ujumla.
Kwake, binadamu, mwenye maana na anayefaa ni yule anayemudu kumiliki vitu hivyo, hii siyo kwa wasichana peke yake, bali hata wanaume, kama mtoto wa kiume alioneshwa thamani ya mtu inatoka kwenye gari, nyumba, na mali, naye bila shaka atakuwa anababaikia vitu hivyo.
Linapokuja suala la uhusiano, anajitahidi kumwonesha msichana kwamba, anavyo vitu hivyo au anao uwezo wa kuvimiliki. Anafanya hivyo, kwa sababu, aliambiwa thamani yake inakuwepo pale anapokuwa na vitu hivyo.
Wazazi wengi wameegemeza thamani zao kwenye vitu, badala ya wao wenyewe. Bila hiari yao wanawafundisha watoto watoto wao kujali na kuthamini vitu, badala ya utu wao. Kwa kadri mfumo wa maisha ulivyokuwa ukiendelea, ukilinganisha na zamani, utagundua binadamu alijitoa thamani na kuiweka kwenye vitu, hasa mali.
Bahati mbaya, wale watoto wa wazazi ambao wana maisha ya kati, ndiyo ambao wanasumbuliwa sana na mali. Kwa nini? Wazazi hao hawajui kama wako juu au chini kimapato.
Katika kujitafuta hufanya mambo na kutoa kauli zenye kuonesha kwamba, maisha ni mali, basi. Wazazi walio chini kabisa, wanaweza nao kuwaathiri vibaya watoto kwa kuzungumza na kutenda kwa njia ambayo watoto wataamini kwamba, umaskini huondoa kabisa thamani ya mtu.
Wale wa juu kabisa, wanaweza wasifikirie kuwa gari au nyumba ni mambo ya maana sana, hata kama wamefundishwa kuhusu mali. Wao watafikiria mali kwa mkabala mkubwa zaidi.
Labda watafikiria kuhusu ndege ya kutembelea, boti ya kifahari na mengine. Lakini, yote ni ileile, kuamini mali ni kubwa kuliko thamani ya binadamu. Mali ambayo unaitengeneza na kuitafuta mwenyewe iwe kubwa kuliko wewe.
Wazazi ambao wanakuchukulia mali kwa ujumla, kama kitu cha kawaida sana, ambacho uwe nacho au usiwe nacho, maana ya maisha haibadiliki, na thamani yako haiondoki, hawa ndiyo ambao watoto wao tunawapenda.
Nikisema tunawapenda, nina maana kwamba, ni watu ambao kwao, kila binadamu ana thamani bila kujali anamiliki au hamiliki kitu gani. Wazazi ni wepesi sana kusema, ‘hawa watoto wetu nao, wakiona mwanamume ana gari, basi wanamkubali tu, bila hata kuchunguza’
Lakini, nyumbani akina mama kauli zao ni hizi; ‘ukiwa na gari na wewe mbele ya watu unasimama ati’ halafu wanatarajia mtoto anayesikia kauli hizo aje ajue kuwa ana thamani kuliko gari. Hizo ni ndoto za mchana.
Ni wazazi hawahawa ambao hawaishi kusema, ‘umefanya kazi miaka yote, hata nyumba wala gari huna, una akili kweli wewe?’ watoto wanasikia, wanaamini kwamba, asiyemiliki nyumba au gari hana akili. Halafu leo watoto wetu wakiyumbishwa na vitu hivi hadi wanakuwa kama vichaa, tunashangaa.
Nakutakia siku njema iwe ya ushindi kwako na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.






No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.