Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, October 9, 2015

Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuwa Kiongozi Bora Wa Maisha Yako.

No comments :
Sifa kubwa ya viongozi wengi walio duniani ni kutengeneza maisha ya mafanikio iwe kwa jamii waliyomo ama maisha yao binafsi. Kiongozi yoyote yule ambaye hana sifa za kuleta mafanikio huyo mara nyingi huwa hafai  katika jamii husika. Kutokana na hilo viongozi wengi iwe kwa bahati mbaya au kujifunza hujikuta wana sifa za aina fulani ambazo zinawapatia mafanikio.
Lakini unapokuja kuziangalia sifa hizo, si kwa viongozi tu ndiyo zinafanya kazi, hata kwako pia unaweza kuzitumia kukupa mafanikio. Mpaka hapo hiyo yote inaonyesha suala la kuujua uongozi ni la muhimu karibu kwa kila mtu ili kujijengea mafanikio makubwa. Kitu cha kuuliza, ni kwa jinsi gani utakavyoweza kuwa kiongozi bora wa maisha yako na kufikia mafanikio makubwa?
1. Jitoe kikamilifu kwa kile unachokifanya.
Sifa kubwa ya kiongozi ni kujitoa kikamilifu kwa kile anachokifanya. Haya ndiyo maisha waliyonayo viongozi karibu wote duniani. Ni watu wa kujitoa sana kufanikisha maisha ya wengine na yao pia. Sifa hii, ndiyo unayotakiwa kuwa nayo ili kufanikiwa. Unatakiwa kujitoa kikamilifu na kwa nguvu zote mpaka malengo yako yatimie.

2. Jitazame kama mshindi.
Hakuna kiongozi ambaye huwa anaangalia mambo kwa kushindwa. Siku zote viongozi huwa ni watu wa mtazamo chanya. Hiki pia ndicho kitu unatakiwa kukielewa vizuri, ili kikujengee uwezo wa kuwa kiongozi bora wa maisha yako. Siku zote jitazame mshindi kwa kila jambo unalolifanya. Hii ni mbinu nzuri sana ya kukufikisha kwenye mafanikio makubwa.
3. Kuwa na ndoto kubwa.
Hakuna kiongozi mkubwa wa maisha yako zaidi yako. Wewe ndiye kila kitu. Kwa kulitambua hilo, ni muhimu kwako kujiwekea ndoto kubwa za kukufanikisha. Ndoto hizo kubwa unazojiwekea ndizo zinazokufanya unakuwa kiongozi bora zaidi wa maisha yako. Kumbuka, viongozi wote ni watu wa ndoto kubwa.
4. Jijengee uvumilivu wa kutosha.
Safari ya maisha bila uvumilivu ni ngumu sana. Najua kwa kuwa unataka kuwa kiongozi wa maisha yako ni lazima kwako kuwa mvumilivu kwa mambo mengi yanayojitokeza. Kwenye maisha yapo mambo mengi ikiwa pamoja na kukatishwa tamaa na kurudishwa nyuma. Haya yote utayashinda ikiwa utakuwa mvumilivu hadi mwisho.
5. Jijengee tabia ya kujihamasisha.
Inapotokea mambo yako yanakuwa magumu, jiwekee utaratibu wa kujihamasisha. Unaweza ukajihamasisha kupitia vitabu au semina mbalimbali. Lakini hiyo isiishie kwako tu, pia wahamasishe na wengine na kuwasaidia kutimiza malengo yao. Kujihamasisha ni njia pekee itakayokufanya usonge mbele hata pale unapohisi kukata tamaa.
6. Kuwa mtu wa kusikiliza.
Ili uweze kujijengea tabia vizuri ya kuwa kiongozi sahihi wa maisha yako, kuwa msikivu. Acha kuwa mwongeaji sana na kusahau kabisa kuwasilikiliza wengine. Viongozi wote wenye mafanikio makubwa ni watu kusikiliza. Watu wa vitendo na siyo waongeaji sana. Hivyo unachotakiwa kufanya ujue umuhimu wa kusikiliza wengine, hiyo itakusaidia sana.
7. Kuwa na mitazamo chanya.
Mafanikio makubwa ya viongozi wote, mara nyingi yanategemea mitazamo yao. Wengi wao ni watu wa mitazamo chanya sana na mitazamo hiyo huwasaidia kufanikisha mipango na malengo waliyojiwekea. Kwa hiyo unapoamua kuwa kiongozi wa maisha yako, tambua suala la kujijengea mitazamo chanya halikwepeki. Hiyo ndiyo nguzo bora na muhimu itakayokufanya kuwa kiongozi bora wa maisha yako siku zote.
8. Jifunze ubunifu.
Kwa chochote kile unachokifanya, tambua ubunifu ni lazima unahitajika. Siri kubwa ya kufikia mafanikio ni kuwa mbunifu kwa kile unachokifanya. Acha kufanya kwa njia ileile itakukwamisha sana. Ukichunguza kwa makini utatambua viongozi bora walio wengi ni wabunifu. Hivyo, jijengee ubunifu ili kuwa kiongozi bora wa maisha yako na kufikia mafanikio makubwa.
9. Kuwa mtu wa misimamo.
Hautaweza kumudu kuwa kiongozi wa maisha yako kama huna msimamo. Viongozi siku zote ni watu wa misimamo. Siyo rahisi kuyumbishwa hovyo. Ni kitu ambacho unatakiwa kujifunza na kujiwekea misimamo imara ambayo unaiamini. Misimamo hiyo unatakiwa kuiweka katika maeneo mengi ikiwa ni pamoja na mafanikio unayotakiwa kuyasimamia.
10. Jifunze mambo ya uongozi.
Siyo lazima uwe mwanasiasa ili ujifunze suala zima la uongozi. Unaweza ukachukua jukumu la kujifunza uongozi ili kukusaidia wewe binafsi katika maisha yako. Ikumbukwe pia wengi wenye maisha makubwa ya mafanikio, ndani yao wana tabia za uongozi. Kwa kujifunza mambo ya uongozi itakusaidia sana kutumia mambo hayo kwenye maisha yako binafsi na kuwa kiongozi bora wa maisha yako.
Bila shaka umetambua kwamba uongozi ni kitu cha msingi sana kwako na Kila mtu anauwezo wa kuwa kiongozi kwenye maisha yake na kufikia mafanikio makubwa, vinginevyo utaishia kuishi maisha ya hovyo yasiyo na mafanikio ikiwa utakuwa unaishi bila kujiongoza.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea DIRA YAMAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.


No comments :

Post a Comment