Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, October 8, 2015

Kama Unatafuta Mafanikio Kwa Njia Hii, Huwezi Kuyafikia.

No comments :
Kitu pekee mbacho huwezi kukifanya kabisa katika maisha yako ni kile kitu ambacho umeamua kutokukifanya. Mafanikio pekee ambayo huwezi kuyapata katika maisha yako ni yale ambayo hujaanza kuchukua hatua ya kuelekea kwenye mafanikio hayo. Kitu kikubwa kinachoturudisha wengi kwenye safari ya mafanikio ni ule uamuzi wa kutoyafuata hayo mafanikio. Hakuna mchawi wa kumlaumu katika hili kama huoni mafanikio, zaidi yako wewe.
Huu ndiyo ukweli halisi wa maisha. Hakuna mtu mwenye uwezo wa kukuzuia wewe kwenye mafanikio yako zaidi yako. Wewe ndiye kinara wa kuzuia mafanikio yako iwe kwa kujua au kutokujua. Haijalishi vizuizi au hali unazopitia  ni za aina gani. Wewe ndiye mwamuzi wa maisha yako. Kitu kikubwa unachotakiwa kukifanya ili uweze kufanikiwa ni kuwa na hamasa ya kufanikiwa na kujitoa. Mambo mengine yote unatakiwa kuachana nayo mara moja.
Umefika wakati wa wewe sasa kuchagua kufanikiwa au kushindwa. Uamuzi wowote utakaouchukua ni wako na utakupa majibu ya unachokitafuta. Kama umeamua kuwa tajiri, hilo linawezekana pia endapo utachukua hatua na kuamua. Chochote utakachoamua kwenye maisha yako hicho ndicho utakachokipata na hakuna mwingine atakayekupinga  kwa hilo.
Kumbuka kama nilivyoanza kwa kusema chochote utakachoamua utakipata na kinawezekana kabisa. Bila shaka ukiangalia maisha yako utagundua kuwa ule wakati ambao wewe mwenyewe ulisema sitaweza kufanikisha ndoto hii ama ile na ni kweli hukufanikisha. Kuna kipindi tena ulidai utafanikisha hili na kweli ulifanikisha.  Hivyo ndivyo maisha yako unavyoyaendesha na yanakupa ukweli halisi.

Sasa unaweza ukatafakari na kujiuliza kama maisha yako mabovu unataka kumlaumu nani kwa sasa? Bila shaka hakuna. Kama chanzo cha kukosa pesa, kuwa na maisha magumu mwanzilishi wake ni wewe hata ujitetee vipi. Imefika wakati inakubidi ukubali ili ujue namna gani unavyoweza kujisaidia na kutoka hapo ulipo na hadi kufikia mafanikio makubwa.
Mambo mengi umeshindwa kuyafanikisha kwa sababu hukutaka kuchukua hatua za lazima kuyafanikisha mambo hayo. Umeshindwa kufikia uhuru wa kifedha kwa sababu hujachukua uthubutu kamili wa kuelekea huko. Umeshindwa kutimiza malengo yako mara kwa mara kwa sababu pia hukujitoa kikamilifu. Ndio maana kama unatafuta mafanikio yako hivi, yaani nusunusu na ukategemea utafanikiwa sana, acha kujidanganya kwa hilo haliwezi kutokea.
Kuanzia sasa kuwa tayari kulipia gharama za mafanikio yako na jitoe kikamilifu kwa kile unachokitaka. Na ukitokea umeona kuna jambo ambalo hujalifanikisha, jaribu kujichunguza utagundua kwamba hujajitoa kikamilifu kufikia huko. Achana na habari za kulaumu wengine ndiyo wanaokukwamisha kwenye mafanikio yako. Kikubwa chukua hatua ambazo zitakupeleka kwenye mafanikio unayoyataka.
Nikutakie ushindi katika safari yako ya mafanikio, ila endelea kuwashirikisha wengine kutembelea mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO kwa ajili ya kujifunza na kuboresha maisha.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.

No comments :

Post a Comment