Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, October 7, 2015

Kila Mtu Ana Saa Mwilini Mwake.

No comments :
Wanasayansi  wamewapa  watu hawa majina  ambayo  yote  ni ya aina ya ndege. Kwanza ni  wale  wanaochelewa  kulala, ambao  wamewaita mabundi (owls) na wale wanaowahi kuamka,  ambao  wamewaita kurumbiza (larks), ambayo ni  aina ya ndege  pia.
Kuna  watu  ambao,  iwe  wana kazi  au hawana ,  huwa  wana kawaida ya  kulala wakiwa  wamechelewa sana. Lakini, kuna  wale ambao hata kama kungekuwa na kitu gani, kuwahi kuamka  ni  kama lazima kwao.
Ni  kama  vile  hawahitaji usingizi kwa muda mrefu. Halafu, kundi kubwa  ni lile  la tulio wengi  ambao tunalala kwa muda wa saa 7  hadi 8 kwa siku.
Ni  watu  wanane kati ya kila kumi  ambao  wako kwenye kundi hili  la  kulala  kwa saa7  hadi 8  kwa siku. Kwa hiyo hawa wanaochelewa kulala  au kuwahi kuamka , ni wawili tu kati ya kila  watu kumi. Hii ina  maana kwamba, ni wachache  katika jamii.
Wanasayansi  wanasema, watu  wanaochelewa  kulala, kama wale  wanaowahi kulala,  wana tabia  ambazo mtu anaweza kuzibaini,  ambazo watu  wengine  hawana. Kwa mfano,  wale  watu wanaowahi  kuamka, huwa ni  wenye kuchangamka sana  wakati wa adhuhuri.
Ni  watu  ambao kama ni kazi huzifanya vizuri sana  kwenye  asubuhi ya saa nne hadi saa tano. Ni  watu  ambao kwa kawaida  wanakuwa   wazungumzaji sana, ni  watu  ambao  wanakuwa na tabia  za kirafiki au  wanaweza kutengeneza urafiki kirahisi na watu  wengine.


Kwenye  saa 3  hadi 4  usiku,  wanakuwa kwenye hali nzuri kihisia na wanaingilika kirahisi  katika muda kama huo.
Wale  wanaochelewa kulala, huwa  wanachangamka sana wakati  wa adhuhuri. Kwa muda  wa asubuhi, mara  nyingi  jioni, hasa kwenye  saa 12. Mtu yeyote  mwenye  tabia ya kuchelewa  kulala, huwa ni mchangamfu jioni zaidi kuliko  muda mwingine.
Kwa nini kuna  watu  wanaochelewa kulala  na wale wanaoamka asubuhi sana? Mtu  anaweza  kuzungumzia  uvivu au “ ushapu” na kingine chochote ,lakini ukweli huenda  hauko hivyo. Kwenye mwili  wa binadamu, kuna  aina ya saa ambayo huratibu  mwenendo wa binadamu katika kila saa zake 24  za  kutwa. Saa hiyo hufahamika kitaalamu kama circadian rhythms.
Saa iliyoko kwenye mwili  wa binadamu huwa  inaratibu mwenendo wa kulala na  kuamka  kwa binadamu. Hufanya hivyo kwa kuratibu joto la mwili na pia homoni kama  zile za melatonin na cortisol.
Kwa kawaida, homoni ya melatonin huongezeka muda mfupi kabla ya mtu kwenda kitandani kulala, na hupungua muda mfupi baada ya mtu kuamka. Homoni ya  cartisol, ambayo hushughulika na sononi, huwa juu muda mfupi kabla   mtu  hajapata fahamu akitokea usingizini.
Kwa hiyo, mtu  anakuwa mchelewa kulala au muwahi kuamka, kutegemea tu kama homoni au mabadiliko haya yanafanyika mapema  zaidi  au kwa kuchelewa sana ukilinganisha na jinsi inavyotakiwa.
Saa ya mwili  wa binadamu  ina tabia ya kufanya  kazi  polepole  au haraka kutegemea umri. Ndiyo maana  kwa wastani,  wale wanaoamka mapema,  wengi huwa ni wazee. Pia kwa sababu hiyo, ndiyo maana wale  wenye umri wa sekondari  na chuo, yaani  wasiozidi  miaka 22, mara nyingi ndiyo  wanaochelewa kulala au ni “ mabundi” kama ambavyo wataalamu wanawaita na hata wanafunzi  wenyewe.
Kwa kiasi  fulani,  tofauti hii ya umri katika kulala au  kuamka, ni ya kibaolojia (homoni) na kijamii. Mabadiliko ya kihomoni yanayojitokeza kwa kadri  mtu anavyokua, huondoa haja ya mtu huyo kulala saa nyingi, kama zile  anazohitaji mtu  wa umri wa chini.
Lakini imebainika kwamba, mwanga nao una athari  yake kwenye  saa hii  ya kuratibu ulalaji na uamkaji kwa binadamu.
Kwa mfano, mtu  anavyozidi kuwa  mzee, ndivyo  ambavyo kudakwa  kwa mwanga  machoni mwake kunavyopungua. Hii huathiri ufanyaji kazi  wa saa  hii.
Kijamii,  nayo huhusu  shughuli  au majukumu, kuliko kitu kingine. Kwa mfano,  watu wa umri wa kati  na hata wanafunzi,  huweza kukabiliana na utaratibu wa saa za miili yao kwa kutengeneza  ratiba  zao za kulala  na kuamka.
Pamoja  na ukweli  kwamba, utaratibu  huwaumiza, hudumu kulazimisha saa za miili yao kukulubaliana  na utaratibu  wao mpya.
Wanafunzi  wa sekondari  na vyuo vikuu kwa mfano, huwa “ mabundi” kwa sababu  ya shinikizo la kazi. Siyo kwamba, saa zao  za mwili ndivyo zinavyofanya kazi, hapana.
Till  Roenneberg  wa Chuo  Kikuu  cha Munich, Ujerumani, aliwahi kufanya utafiti  wa kutosha, akiwahusisha watu  zaidi ya  25,000 wa umri  kati ya miaka  8 na 90 na kupata  matokeo  muhimu  sana  kuhusu usingizi na saa ya mwili  wa   binadamu.
Kwa mfano, aligundua  kwamba, watoto  huwa wanalala sana asubuhi, hadi wanafikia umri wa miaka 20. Hapo katikati  kunakuwa na  mabadiliko ya ghafla na ya mara kwa mara, ambapo kuna  wakati  huwa  wanaamka mapema  kwa muda fulani.
Mabadiliko haya  yanatazamwa na  wataalamu kama  Roenneberg, kuwa  ni  mabadiliko ya kibaolojia ambayo yanatoa taarifa ya mabadiliko ya kimwili. Watoto wa kike wamebainika kuwa katika umri wa kati ya miaka 13 hadi 19 wanachelewa  zaidi kulala ukilinganisha na wale  wa kiume, ambao kuchelewa kulala upande wao, huanza wakati  wakiwa na miaka 21. Tatizo hapa siyo kwa sababu watoto wa kike  wana kazi nyingi usiku, hapana. Ni  suala la saa ya mwilini.
Watoto  wa kike  hupevuka haraka na hivyo, homoni husika  nazo hufanya mabadiliko  mapema.
Kwa ujumla, watoto  wa umri wa miaka 13 hadi 20 ambao huchelewa  kulala ,hawana  tatizo, bali mara nyingi, saa za miili yao ndivyo zinavyotaka.
Nchini Marekani  kwa mfano, kumekuwa na midahalo yenye kuhusu kama muda wa kuanza  masomo usogezwa kidogo, ili kuwapa watoto muda  wa kulala zaidi  au la.
Hii inatokana na ukweli kwamba, hivi sasa watu wengi wameanza kukubali kwamba, mwili wa binadamu una saa inayorataribu kulala  na kuamka, ambayo siyo  vizuri kuiingilia.
Kwa kawaida, jamii nyingi hutazama kuchelewa  kuamka  kama udhaifu na kuchelewa  kulala kama sifa ya aina  fulani. Kuna  wanaoamini  kwamba, kuamka mapema  humfanya  mtu  kufanya kazi kubwa  zaidi  kwa siku au humfanya mtu  kuvuna  zaidi katika kipato. Inategemea  tu, lakini hakuna ushahidi  unaotilia nguvu  jambo  hilo.
Ushahidi mpya   wa hivi karibuni unaonesha kwamba, kulala mapema au kuchelewa  kuamka, ni suala la chembe urithi (DNA), badala  ya utashi  wa mtu. Kama mtu anafanya mazoezi na kumudu kubadili mtindo wake  wa kulala, anaweza,  lakini kama amerithi  kulala au kuamka mapema, hali inaweza kuwa mbaya kwa upande wa mtu huyo.
Kumbuka kwamba,  watu  wanaopenda  kulala usiku sana, iwe  wana shughuli au hawana, bali wanapenda  tu, huwa hawapatishwi tabu na hali hiyo ya kukosa usingizi, kama ambavyo wale wanaolala saa  mbaya  wale  wanaolala saa  mbaya kwa sababu maalumu, huumizwa  na hali hiyo. Hii ni kwa sababu, jambo hilo liko  ndani mwao. Mtu ambaye yuko hivyo, kujaribu kumlazimisha, ni kupoteza muda  na kumuumiza bure.
Carolyn Schur,  ambaye ni mtaalamu  wa masuala ya usingizi na mtunzi wa kitabu chenye kuchambua sana  kuhusu  wanaolala usiku  sana na wanaoamka mapema sana  cha Birds of a Different Feather, anasema, kuna watu ambao pia ni kama  wagonjwa kuhusiana na usingizi.
Watu hawa ambao wanaelezewa kitaalamu kwamba,  wana tatizo linalofahamika kama Delayed Sleep Phase Syndrome au DSPS,   huwa  hawawezi kulala  chini ya saa 8 usiku na huchelewa  kuamka asubuhi.
Hawa huwezi kuwabadili na kuwafanya  kulala mapema kabla ya saa 8 usiku  na kuwalazimisha kuamka mapema. Kama  utadumu  au  wao  watadumu, kuna uwezekano wa kuingia  kwenye  matatizo.
Kila  mmoja  wetu  ana saa  zinazomtosha  katika  kulala  pia.  Wengine wakilala kwa saa tano. Wakati  wa usiku  inawatosha,  wengine saa 7 ndizo zinazowatosha na  wengine saa 8 au zaidi.
Ni kwa namna gani  tunaweza  kuheshimu na  kupata saa zinazotutosha kwa usingizi ni jambo muhimu sana.
Lakini kujua  kuwa  tuna saa miilini  mwetu ambazo hutupangia tuwe watu  wa kulala kwa namna gani, ni jambo lingine muhimu.
Kuna wakati  tunaweza  kuwalalamikia wenzetu, yaani waume au wake zetu kwamba, wanachelewa sana kuingia kitandani au kwamba wanawahi au kuchelea sana kuamka. Kwa sehemu kubwa suala linaweza kuwa saa ya mwilini na siyo utashi wa  mtu.
Nakutakia kila la kheri katika harakati za kuboresha maisha yako na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
 DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
 Ni wako rafiki katika mafanikio,
 IMANI NGWANGWALU,
Kama una maoni, ushauri au changamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio yako wasiliana nami kwa email dirayamafanikio@gmail.com au simu 0713 048035 kwa ushauri na msaada wa haraka.  No comments :

Post a Comment