Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, February 8, 2016

Siri Katika Kupata PESA Na MAFANIKIO.

No comments :
Katika ulimwengu wa leo hakuna binadamu asiyetambua thamani na umuhimu wa pesa. Pesa inathaminiwa hata na watoto wadogo. Ukimpa mtoto karatasi na pesa halafu ukamwambie tupa zote atatupa karatasi atabaki na pesa.

Kila mtu anahangaika kuitafuta shilingi.  Watu wanahangaika kwa waganga, Usiku na mchana kuitafuta pesa. Pesa inatafutwa kwa njia ya halali na haramu jamani pesa! Pesa ni nini? Mbona viko vingi duniani vizuri lakini pesa inaongoza kutafutwa na kila mtu.

Duuh! pamoja na kutafutwa huku pesa na kila mtu lakini swali la kujiuliza mbona wengi bado wanahangaika na hawaipati pesa? Mbona wengi wana elimu lakini pesa hawana? Mbona wengi wana akili lakini pesa hawana? Nauliza tena kwa nini pesa jamani? 


Katika dunia kuna makundi manne ya watu wanaotafuta pesa ila kundi moja tu ndio lenye mafanikio. Humiliki utajiri na uchumi wa 90% wa dunia. Kundi hili ni la watu wachache sana ila ni watu pekee waliogundua siri ya pesa na mafanikio.

TOA THAMANI, UPATE PESA.
Hawa ni watu wanaoishi ndoto zao na kufuata mbinu za mafanikio ambazo ziko katika siri za pesa na mafanikio. Nimekwambia Leo nataka kukupa SIRI YA KUTAFUTA  PESA NA MAFANIKIO, nataka nikuzindue kutoka kwenye usingizi wa umaskini na leo uanze kukimbia mbio zako mwenyewe.

Unashangaa? Usitoe macho ndio ukweli usiopingika mafanikio ya pesa yana siri yake waliofanikiwa wamezigundua na kuzifanyia kazi siri hizi. Huwezi kuitafuta pesa kama pesa halafu ukategemea kupata pesa abadani asilani. Unaweza kusema  nawe maneno yako ndio nini kusema huwezi kupata pesa kwa kuitafuta pesa kama pesa? Wakati watu wanafanya hivyo. Usiwe mbishi tulia kwanza.

Iko hivi, katika pesa huwezi kupata pesa bila ya kubadilishana na thamani ya kitu. Hizo zilikuwa zama za mawe na ujima sasa tuko katika karne ya 21 ya sayansi na teknolojia. Hivyo mambo yamebadilika. Kisaikolojia na maumbile ya binadamu kamwe huwezi kuwa na pesa nyingi au kumiliki utajiri mpaka uvitumikie viumbe vya mwenye utajiri wa  Mali na dhahabu.


Hapa najua wengi nimewaacha kidogo. Hapa maana yangu ni kuwa huwezi kupata pesa mpaka utatue changamoto na matatizo ya viumbe wa Mwenyezi Mungu (Watu). Hapa nadhani umenipata uzuri. Hii ndio siri ndio siri ya kwanza ya utajiri na pesa. Ni lazima utatue matatizo ya watu ndipo watu hao wakupatie pesa.Haijalishi ni maskini au ni wanyonge kiasi gani watakulipa pesa tu.

Anza na kutoa huduma watatulie changamoto walizonazo watakupa pesa tu watake wasitake. Mfano wa kwanza chimba kisima cha maji watakuletea pesa umekaa, waletee usafiri watakuletea pesa umekaa,Wajengee shule watakuletea pesa umelala, walimie nyanya,mchicha, kitungu na mengineyo mengi watakuletea pesa umelala ndani kwako.

Siri ya kwanza ya utajiri ni kutoa huduma watazame matajiri wote duniani wanatoa huduma, wanatatua matatizo ya watu. Mtazame Bakheresa ameona unahangaika na kukuna nazi akabuni kukuletea nazi ya pakiti ili umpe pesa. Naona sasa mpaka hapo tunaenda sawa na siri ya kwanza ya kupata pesa na mafanikio, subiri nikupe siri zingine bado zinakuja.

Siri ya pili ya pesa na mafanikio ni kuzalisha mali. Hapa ndipo patamu watu wengi leo hii wanatafua eti pesa kwa kuwa mchuuzi wa biashara ndogondogo wanaita mtaani kulangua. Unaenda kwa mzalishaji MKUBWA unanunua kiasi unaenda kuuza ili nawe upate kuwa na pesa na umiliki utajiri.


Mweee hii ni kucheza na nyani shambani utavuna mabua shauri  yako usije sema sikukuambia. Mzee wa nyundo kali napita mie. Mwenye kusikia leo naasikie zalisha mali upate pesa uninunue mali kupata pesa utachelewa sana na pengine ukaishia kupata za kubadilisha mboga tu. Matajiri wakubwa wamegundua siri ya pesa ndio maana wanazalisha mali ili wapate pesa.

Siri ya tatu ya utajiri na pesa ni kuwa na ‘Network’ nzuri ya watu. Watu waliofanikiwa wana marafiki bora katika ushirikiano wao. Hawako tayari kuwa na marafiki wavivu, wakatisha tamaa na wasio na ‘vision’ wala malengo na ndoto katika maisha yao. Huchagua watu wa kwenda nao katika safari ya mafanikio. Naamini tupo pamoja.

Siri ya nne ya utajiri na pesa katika mafanikio ni kujifunza kila siku. Matajiri na watu wenye pesa wanasiri ya kujifunza kila siku na kujiendeleza. Wapenda kujua na kujifunza kila kitu hawana kujifanya wajuaji hata kama  kuna kitu wanajua hujifanya hawajui ili wajifunze zaidi.

Siri ya tano ya pesa na mafanikio ni ubunifu katika kuitafuta pesa ni lazima uwe mbunifu katika kuitafuta pesa. Pesa  haipatikani kirahisi kwa wale wasiotumia ubunifu  ila tu kwa wale wabunifu katika kufikiri na kutenda. Ili upate pesa ni lazima uwe na ubunifu katika kufanya kile unafanya iwe ni kilimo,biashara au ufugaji.

Kwa haya machache naomba kuishia hapa kwa leo tukutane tena katika makala nyingine Mungu akipenda.  Asanteni kwa kunifuatilia  wako katika kusaka mafanikio na utajiri Shariff H. Kisuda.

Ansante kwa kutembelea na kufatilia DIRA YA MAFANIKIO kila wakati. Endelea kuwaalika na wengine wafaidike na makala tunazotoa hapa. 

Tupo pamoja;

Shariff Kisuda aka Mzee wa Nyundo Kali,
Simu; 0715 079 993,
No comments :

Post a Comment