Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, January 5, 2017

Fanyia Kazi Utajiri Wa Mabonde Haya Ukusaidie Kujikwamua Kiuchumi.

No comments :
Ni majira ya saa tisa alasiri ambapo nimekaa kandokando ya ufukwe wa bahari huku nikitazama viumbe mbalimbali ambao wapo mahali hapa,  mara ghafla akili yangu inahama na kuzama katika dibwi la mawazo, naanza kutafakari ukuu wa Mwenyezi Mungu na uwepo wake katika dunia hii. 

Mawazo yangu yanazidi kuwa makubwa zaidi nagundua ya kwamba Mungu wetu anatupenda sana kwani ameweza kuviumba vitu mbalimbali kwa ajili ya matumizi yetu wanadamu. Na vitu hivi ndivyo vinavyotufanya tuendelee kuishi. Asante Mungu.

Nayatazama maji ambayo kiukweli yanavutia kwa macho kwani ya rangi ya kupendeza. Naendelea  kuyatazama maji kwa mbali naona kuna vitu ambavyo ndani kuna watu,  najaribu kuvichunguza kwa umakini nagundua ni mashua, mitubwi na natazama mbele naona kuna meli kubwa za mizigo na abiria.

Wakati naendelea kutazama unakuja ule usemi usemao "shilingi yazama meli yaelea" hapa napata majibu ya kwamba mwenyezi Mungu ana makusudio yake katika ulimwengu huu hasa kwa sisi waja wake. Kwani wavuvi hupata pesa kupitia bahari hii, mizigo mbalimbali husafirishwa kupitia bahari hii na mambo mengi hufanywa kupitia bahari hii.


 Nautazama udongo ambapo mi nimekaa juu yake,  kwa macho unavutia sana halikadhalika na upepo uliopo mahali hapa unasahaulisha matatizo kwa muda.  Kweli Tanzania nchi yangu ni nzuri sana,  nilalapo nakuwaza wewe.

Kwani umejaliwa kila aina ya rasilimali ambazo kiukweli hata sehemu nyingine rasilimali hizi hazipo. Mmmh kweli jamani najivunia kuwepo katika nchi hii. Pamoja  kila aina ya rasilimali tulizonazo najiuliza mbona hutajafanikiwa sana, ikiwa rasimali ambazo tunazo ni mtaji tosha? Kwa kweli nakosa majibu sahihi.

Akili yangu inazidi kuwaza huku nikifikiria zaidi kuhusu rasilimali za nchi yangu ya Tanzania. Nawaza kuhusu rasilimali ardhi ambayo viumbe vyenye uhai na visivyo na uhai vipo juu yake.

Tanzania yangu imejaaliwa kuwa ardhi tosha ambayo inafaa kwa matumizi mengi sana ikiwa ni pamoja na

1. Makazi
2. Kilimo
3. Majani kwa ajili ya malisho
4. Ardhi kwa ajili ya kujenga huduma  za jamii. 
5. Ardhi kwa ajili ya kutengeneza miundo mbinu kama barabara.
Pamoja na matumizi mengineyo.

Pamoja na matumizi mbalimbali ya ardhi tuliyonayo, kwa kuwa nchi yetu idadi kubwa ya watu wake huishi kijijini na idadi kubwa ya watu hao hutegemea zaidi kilimo na ufugaji kama shughuli za kiuchumi. Pamoja na yote hayo mbona  tunalalamika umaskini, pamoja na  njaa.  Hivi tunakwama wapi wakati hakuna foleni na rasimali ardhi ipo ya kutosha?

Lakini pamoja na hayo kiukweli ni lazima tuweze kuitumia vyema rasimali ardhi ili tuweze kukua kiuchumi kupitia kilimo.

Zipo pia pamoja na sera mbalimbali zinazoeleza kuhusu kilimo tangu kipindi cha miaka ya nyuma mpaka hivi sasa hii ikiwa ni pamoja na " sera ya kilimo cha siasa,  kilimo cha kufa na kupona,  kilimo ni uti wa mgongo pamoja na sera ya kilimo kwanza.

Sera hizo zote zimekuwa zikifanya kazi katika kuhakikisha watanzania waamini katika kilimo, hasa katika ukuaji huu wa kiuchumi. Nazidi kuwaza na kuwazua kuhusu kilimo cha Tanzania nakosa majibu sahihi.

Kwani ikiwa tunasema kilimo kwanza ni jitihada gani ambazo zimekuwa zikifanywa kuweza kukuza kilimo hiki? Kwani tangu miaka ya nyuma tunatumia jembe la mkono pamoja na mvua.

Pamoja na kuendelea kuisubiria mvua hii kuna wakati mvua zinagoma kunyesha huku njaa ikiendelea kumtawala . Wapo wale ambao wanaona mvua hazinyeshi wanadiliki kusema hata mvua zipo kwenye uhakiki. Mmmh sijui ni kweli mvua zinahakikiwa nazo?

Mawazo yangu yanakuja na jibu mvua hazihakikiwi ila kutoka tumezoea kufanya kilimo kwa mazoea kwa kutegemea mvua, pale ambapo mvua hizi kutoka na mabadiliko ya tabia ya nchi zinashindwa kunyesha tunajikuta tunashindwa kuendana na mazingira.

Mwisho wa siku tunajikuta tunatangaza njaa. Mmmh jamani!  Ni kweli kutokunyesha kwa mvua kunasababisha njaa?  Kwa majibu ya haraka utasema ni ndio. Lakini ukweli ni kwamba pamoja na kuwepo kwa uwepo ya vijito,  mito mabwawa na visima hivi kweli tumeshindwa kufanya kilimo cha umwagiliaji? Usinipe jibu

Bila shaka naamini tunaweza kufanya kilimo cha umwagiliaji kwani tanzania yetu imebarikiwa kuwa na mito mingi lakini haina faida kwa wananchi wake kwa asilimia kubwa. Ifike mahali Serikali ijenge miundombinu ya mabomba ya umwagiliaji ikiwapelekea wananchi kwenye mashamba na wao watalima bila kutegemea mvua. 

Kwani hapa Tanzania yapo mabonde yaliyopo huko Kilombero Malindi,, mvumero, Kilosa mbarali, Isimani,  songea, rukwa,  Tanga na sehemu nyinginezo ambazo kilimo kama hiki kinaweza kufanywa na watu tukaneemeka kwa kilimo hiki bila kutegemea mvua. Jiulize, utajiro wote ulioko kwenye mabonde haya tunaufanyia nini? 

Kipo pia kilimo cha matone ambacho hakihitaji uwepo wa mvua. Kama ndivyo hivyo ni kwanini  tutangaze njaa? Bila shaka majibu ya kutangaza njaa kwa mkoa wowote ule ni kwamba tumezoea kuishi kimezoea. Nafikiri wizara husika ikishirikiana wakuu wa mikoa, wilaya pamoja na wataalamu wa kilimo waweze kuona umuhimu juu ya hili.  Ilikuwa kufikia malengo ya kilimo ya mwaka 2025.

Kama endapo tutashindwa kushirikiana kwa pamoja juu ya mbinu mbadala kwa ajili ya ukuzaji wa kilimo katika nchi yetu tutaendendelea kuishi katika maisha yale yale kila wakati.  Najua mapinduzi ya kilimo yanawekana. Tanzania pamoja na rasimali ardhi tuliyonayo tunauwezo mkubwa sana wa kuweza kuwasaidia mataifa mengine. Kwa kuuza mazao ya biashara ambayo tutayazalisha mahali hapa.

Mawazo yangu kwa leo naomba yaishie hapa, ila kila mmoja wetu kwa hayo niliyoyaeleza yakamguse huku tukitegemea yakaleta "mapinduzi makubwa ya kilimo". Kwani najua kila kitu kinawezekana tena kwa asilimia mia moja.  Kizazi kijacho matumizi ya mvua pekee na jembe la mkono libakia historia kama matumizi ya zana za mawe. 

"kabla jua halijazama natumaini ya kwamba tutaleta mapinduzi ya kilimo" kila mmoja afikirie juu kufanya mapinduzi ya kilimo

MUNGU IBARIKI TANZANIA WABARIKI NA WATU WAKE. 

Ni wako mkeleketwa wa maendeleo na mafanikio Afisa Mipango Benson chonya,

No comments :

Post a Comment