Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, January 30, 2017

Mambo Ya Lazima Kuwa Nayo Katika Safari Ya Mafanikio.

No comments :
Katika safari yoyote ya mafanikio huwa ipo misingi na mambo ya lazima ambayo ni lazima uyajue ili kufanikiwa. Kwa kuyajua mambo hayo yatakupa dira na mwelekeo mzuri wa kufikia mafanikio makubwa.
Ni kweli unaweza ukawa una malengo mazuri uliyojiwekea, lakini bila kuyajua mambo hayo na kuyafanyia kazi itakuwa ni ngumu sana kufikia mafanikio yako. Watu wengi wenye mafanikio wanayajua mambo haya na kuyafanyia kazi mara kwa mara. Je, unajua ni mambo gani ambayo ni ya lazima sana katika safari yako ya mafanikio?
 1. Hamasa.
Ili uweze kufanikiwa ni lazima kwanza uwe na hamasa kubwa ya kufikia mafanikio hayo. Wengi huwa wanashindwa kufanikiwa kwa sababu ya kukosa hamasa. Unapokuwa unashindwa kuwa na hamasa inakuwa ni ngumu kufikia mafanikio yoyote kwa sababu karibu kila kitu utakifanya kizembe au kivivu ilimradi ukikamilishe.
Kitu kinachokufanya uongeze juhudi kwa kile unachokifanya sasa ni kwa sababu una hamasa ya kutaka kufanikiwa. Kushindwa kwako kutaanza mara moja ikiwa utaanza kukosa hamasa hiyo. Huu ni ukweli ambao ni lazima uujue ili kuweza kufanikiwa, vinginevyo hakuna utakachoweza kukifanikisha. Kila kitu kitakuwa kigumu kwako.

2. Uzingativu.
Haijalishi una hamasa kubwa kiasi gani lakini ikiwa ndani yako utakosa uzingativu, kuyafikia mafanikio hayo itabaki kuwa ndoto za mchana. Watu wote ambao huwa wanafanikiwa katika mambo yao ni watu wa kuzingatia sana. Huwa ni watu ambao hawana papara, wakianzisha jambo hulifatilia mpaka kulifanikisha.
Mara nyingi unapoweka nguvu ya uzingativu katika jambo moja, huwa zinaleta matokeo makubwa na kuyashangaza. Hakuna kinachoshindikana katika nguvu hizi za uzingativu zinapotumika. Hiki ni kitu ambacho unatakiwa kukiweka kwenye akili yako na kukifanyia kazi. Na hili ni jambo la lazima sana katika safari yako ya mafanikio, bila hivyo huwezi kufanikiwa.
3. Kujiamini.
Msingi mkubwa wa mafanikio upo kwenye kujiamini. Ikiwa wewe utakuwa mtu ambaye unajitilia shaka na hujiamini katika mambo yako ukweli wa mambo uko wazi hata ufanyaje huwezi kufanikiwa. Kama unabisha hebu angalia mambo ambayo hukuwahi kufanikiwa, utagundua mengi hukuweza kujiamini sana.
Kwa hiyo mpaka hapo utagundua kwamba kujiamini ni jambo la lazima sana katika safari ya mafanikio yako. Mafanikio yoyote yale yanahitaji kwanza wewe uanze kujiamini binafsi kuwa utafanikiwa. Kwa kadri unavyozidi kujiamini sana katika maisha yako, ndivyo ambavyo utajikuta ukifanikisha mengi.
4. Kufanya kazi kwa bidii.
Ni kweli unaweza ukawa una hamasa kubwa, una nguvu ya uzingativu na unajiamini vya kutosha, lakini kama hufanyi kazi kwa bidii huwezi kufanikiwa. Kazi ni msingi mkubwa sana wa mafanikio yoyote unayoyahitaji. Ili uweze kufanikiwa ni lazima kujituma na kufanya kazi kwa bidii zote. Hapo ndipo utaanza kuyaona mafanikio yako.
Watu wote wenye mafanikio makubwa ni watu wa kujituma sana. Bila kufanya kazi kwa bidii, elewa kabisa mipango na malengo yako mengi yataishia njiani. Kwa hiyo kama ni kazi weka juhudi zako zote mpaka ikuletee mafanikio. Kwa sababu unakuwa umeweka nguvu zako nyingi, hata ikitokea umeshindwa hutajilaumu sana. 
Kwa mambo hayo manne ni silaha kubwa sana ya mafanikio kwa mtu yeyote mwenye nia ya kufikia mafanikio makubwa. Kitu kikubwa naomba ufanyie kazi mambo hayo ili yaweze kubadili maisha yako na ya wengine wanaokuzunguka. Kila kitu kinawezekana ukiamua, hivyo amua sasa upate kufanikiwa.
Nikutakie kila la kheri katika safari yako ya mafanikio . Kumbuka tupo pamoja.
Endelea kujifunza kupitia dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Kama makala hii imekusaidia na unapenda kujifunza zaidi, karibu kwenye kundi la Whats App ili tuweze kujifunza pamoja tena kwa ukaribu. Kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S, kisha ikifuatia na jina lako kwenda 0713 048035 ili uanganishwe.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YA MAFANIKIO.
Ni wako rafiki,
IMANI NGWANGWALU,

No comments :

Post a Comment