Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, January 26, 2017

Kama Unayatafuta Mafanikio Kwa Njia Hii, Huwezi Kuyapata.

No comments :
Kuna wakati mwingine binadamu tunakuwa ni viumbe wa ajabu sana kutokana na kutotaka usumbufu hata kwa yale mambo tunayoyahitaji. Inapotokea tunataka kitu cha aina fulani tunakuwa ni watu ambao tumejiweka katika kundi fulani ambalo hatutaki kuweka juhudi sana yaani kwa lugha rahisi tunakuwa kama tunajihuhurumia hivi na kuona kama tutaumia kwa kutafuta vitu hivyo.
Kutokana na hali hiyo hupelekea wengi wetu kuanza kutafuta njia za kupata mafanikio ya haraka na upesi. Kumbe kwa kufuata njia hizo ndiyo tunakuwa tunajidanganya na kupotea kabisa ukizingatia katika maisha hakuna njia ya mkato kuweza kufikia mafanikio. Mafanikio yote yanakuja hatua kwa hatua. Na kama unaona njia hiyo ipo tayari unakuwa unapotea.
Utambue kuwa kila kitu kwenye maisha kinapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii kubwa na maarifa. Hakuna lelemama katika kutafuta mafanikio. Mafanikio ni mfumo wenye hatua zake ambazo ni lazima zifuatwe. Sasa anapokuja mtu anakwambia kwamba ipo njia hii hapa ya mkato kuyapata mafanikio, mmmh huyo ni vyema ukamuogopa sana kwa kuwa atakuwa anakupoteza huku ukiwa unajiona.
Ni vigumu sana kuweza kufanikiwa kama utategemea njia za mkato na bila kuweka juhudi yoyote ile kubwa. Kama utayapata mafanikio hayo kwa njia hiyo ni wazi tu yatakuwa ya muda. Hiyo yote inaonyesha hakuna njia ya mkato kufikia mafanikio yako. Kitu kikubwa unachotakiwa kufanya ni kuweka juhudi zako kubwa mpaka kufanikiwa na siyo vinginevyo.

Hebu jaribu kuangalia watu wote wale ambao wamewahi kushinda bahati nasibu. Watu hawa wengi wao ukija kuwafatilia maisha yao  baada ya miaka michache mbele utakuja kugundua ni watu ambao pesa hizo hawana tena na wafelisika. Kufilisika kwao kumekuja kutokana na walizipata pesa hizo nyingi kwa ghafla na kwa njia ambayo ni ya mkato na sasa zimewakambia.
Kama nilivyosema mafanikio yanakuja hatua kwa hatua. Kuna kujifunza kwingi sana inapotokea umeanzia chini kabisa. Mara nyingi  hiyo inakuwa inakujengea misuli ya kukua kidogo kidogo na mwisho wa siku unajikuta upo kwenye kilele cha mafanikio makubwa. Endesha maisha yako kwa kujiamini na kujua maisha yako ni lazima ufanikiwe hata bila kutegemea njia za mkato ambazo nyingi huwa zina mashimo mengi na isitoshe hazina uhakika wa kufika.
Hiki ni kitu ambacho unatakiwa ukiweke kwenye ubongo wako kuwa unahitaji ujasiri, kujitoa na kuwekeza nguvu zako nyingi kwa kile unachokifanya na siyo kupita njia ya mkato kama unavyofikiri. Kumbuka, ni lazima kujituma kwa bidii tena wakati mwingine katika magumu na vizuizi vya kila aina bila kukata tamaa. Kila kitu kitawezekana na utafika kule unakohitaji kufika katika maisha yako ikiwa utazingatia ukweli huo ninao kwambia sasa.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya maisha yako na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,

No comments :

Post a Comment