Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Tuesday, March 22, 2016

Fursa Anazoweza Kuzitumia Kijana Wa Kitanzania Kufanikiwa.

No comments :
Kimazingira Tanzania, ni moja ya nchi ambayo imejaliwa sana hapa duniani kuwa na fursa nyingi za wazi ambazo ukizitumia ni lazima ufanikiwe. Lakini pamoja na wingi wa fursa hizo ambazo zinaweza kutumiwa na kuleta mafanikio kwa taifa lakini bado kumekuwa na wimbi kubwa la watu ambao hawana ajira.
Kutoka na ukosefu wa ajira vijana wengi wamekuwa wakihaha kutafuta ajira huku na huko bila matumaini. Ni tatizo ambalo limekuwa likisumbua sana si kwa wazazi tu pekee ambao ni wahanga watoto hao, bali hata taifa kwa ujumla. Lakini yote hayo yamekuwa yakitokea na kusahau kwamba tupo kwenye nchi mbayo ina utitiri ama wingi  wa fursa za kutosha.
Kwa kuwa fursa hizi zipo ni matumaini yetu kwamba, badala ya vijana wetu hawa waliomaliza vyuo vikuu kukimbilia ajira ambazo tena kwa sasa ni finyu, ni vyema wakazitumia fursa zinazowazunguka kuwafanikisha. Kwa kusoma makala haya, utajifunza fursa ambazo zinaweza kumsaidia kijana wa kitanzania  popote alipo kujiajiri na kutengeneza mafanikio makubwa kuliko kubweteka peke yake kwa kusubiri ajira.
1. Kilimo cha kisasa kwa kutumia hema.
Hiki ni kilimo kigeni kwa wengi ambacho kinatumia teknolojia ya kisasa ya hema. Lakini pamoja na ugeni wake hiki ni kilimo ambacho pia kinaweza kutatua tatizo la ajira kwa uhakika. Kwa nini iko hivyo? Hiyo ni kwa sababu pato lake linakuwa kubwa na la uhakika ingawa eneo la kulima linakuwa dogo.
Kwa kutumia kilimo hiki kijana anaweza kuchangamkia fursa hii na kuajiri.  Hapa kijana anaweza kujiajiri kwa kujihusisha na kilimo hiki kuliko kukaa na kutegemea ajira peke yake. Kwa mfano, wataalamu wanatuambia katika eneo dogo lenye urefu wa mita kumi na tano na upana wa mita nane lina uwezo wa kutoa tani za nyanya zisizopungua kumi ikiwa litasimamiwa vizuri kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kwa hiyo utaona kwamba kwa kijana ambaye yupo makini na ameamua kuwekeza akitoa nguvu zake nyingi kujihusisha na kilimo hiki basi atakuwa yupo sahihi kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine. Kitu kikubwa cha kuzingatia ni  kuwa tayari kutoa gharama zinazohusika hadi kilimo hiki kikafanikiwa na kuwa chenye manufaa makubwa kwa kila kijana mwenye uthubutu.

MKOMBOZI KWA MKULIMA
2. Ufugaji wa nyuki.
Kati ya miradi ambayo naweza kusema ni rahisi kwa kijana yeyote yule wa kitanzania ni ufugaji wa nyuki. Ni moja ya mradi ambao unaweza ukafanywa katika mazingira tuliyonayo bila kuhusisha gharama kubwa sana na ikawa ni chanzo kimojawapo cha kujiajiri na kuingiza kipato kikubwa. Ufugaji huu hauhitaji gharama kubwa sana mara nyingi unafanywa kulingana na pato alinalo mwenye nia ya kuwekeza.
Tuchukulie kwa mfano kwa kijana ambaye hana mtaji anataka kufuga nyuki ili wamzalishie asali hapa anafanyaje? Kitu ambacho anaweza akafanya si lazima awe na mizinga ya kisasa. Anaweza akatengeneza vibuyu au magome ya miti na kuweka mizinga yake kwa ajili ya ufugaji rasmi. Baada ya kuweka mizinga inatakiwa aweke mazingira rafiki ya kuvutia nyuki kama maji na nta.
Kwa kijana amabaye atafanikiwa kujihusisha na ufugaji huu na akasimamia vizuri, ni ushahidi tosha hata hiyo ajira hatoitaka tena kutokana na pesa atakayoingiza. Hii ni moja ya fursa kubwa sana ambayo inatoa ajira isipokuwa vijana wengi wanakuwa kama wamefungwa macho kwa kushindwa kuona ni nini cha kufanya na kujikuta kukimbilia mjini ambako ajira zenyewe zimekuwa ni kwa uchache.

WEKA MIZINGA BORA.
3. Kilimo cha mazao ya biashara.
Mbali na ufugaji wa nyuki na kilimo cha hema, kijana anaweza kuchangamkia fursa ya kufanya kilimo cha mazao ya biashara. Mazao haya yanaweza yakawa kama karanga,  choroko, kunde, alizeti au hata pamba lakini hiyo yote inategemea sana na eneo ambalo upo urahisi wa kipi kwako cha kufanya.
Kitu kikubwa ni kule kufuta mitazamo hasi kwamba kilimo ni cha watu duni hiyo siyo kweli. Watu wengi wanaoendesha maisha yao vizuri sana kwa kutegemea kilimo hiki cha kisasa. Anza kwa kujifunza kwa wale wakulima waliofanikiwa na kisha changamkia fursa ya kilimo hiki ambacho kinaweza kikawa mwanzo wa ajira kubwa kwako kuliko unavyofikiri.
Kwa kijana ambaye ataingia kwenye kilimo hiki kikamilifu na akasimamia masoko vizuri, njia ya mafanikio itaonekana kwake. Uzuri wa kujihusisha na kilimo hiki cha mazao ya biashara hata soko lake mara nyingi linakuwa kubwa hali ambaye hupelekea kupata faida kubwa kwa mkulima. Hivyo ni wito wetu kuhakikisha vijana wengi wanaolia ajira hakuna kulizingatia hili sana na kuamua kuchukua hatua.

IKILIMWA VIZURI, PATO NI KUBWA.
4.  Ufugaji wa samaki.
Pia ufugaji wa samaki unaweza ukawa ni chanzo kizuri cha kipato kwa vijana wengine ambao hawana kazi hasa katika yale maeneo ambayo ni shida kupatikana kwa samaki. Ufugaji huu unaweza  ukafanywa kwa kuchimba bwawa dogo la samaki na kuanza kutengeneza pesa. Bwawa si lazima liwe kubwa sana linaweza likawa  dogo hata la mita 'square' mia nne.
Uzuri wa kufuga samaki ni kwamba kwanza wanachukua muda mfupi,  pia inachukua miezi minne kukua. Lakini hiyo haitoshi upatikaji wa vifaranga wa samaki pia sio mgumu na vinapatikaana kwa bei rahisi. Lakini uzuri mwingine si kupatikana kwa vifaranga tu,  bali hata pato lake linakuwa ni kubwa kulingana  na kile ulichowekeza kwa muda mfupi.

BWAWA LA KUCHIMBWA LA SAMAKI.
Wataalamu wanatuambia hivi, kwa mfano kama umeweka samaki kwenye bwawa dogo la mita square mia nne. Kwanza bwawa hilo linauwezo wakuchukua samaki elfu nne. Sasa kama eneo hilo linachukua samaki hao na kila samaki akawa na nusu kilogramu, basi kwa bwawa hilo ndani ya miezi minne utapa milioni nane hata kama kilo moja hapo utauza kwa shilingi elfu nne.
Hizi ni baadhi ya fursa chache ambazo kijana wa kitanzania anaweza kuzitumia kufanikiwa. Ingawa hata hivyo kijana anaweza kujihusisha na mambo mengine zaidi ya kumuingizia kipato kama ufugaji wa kuku kwa kisasa au hata kilimo cha matunda.
Chukua hatua kufikia mafanikio makubwa na acha kuendelea kulia eti ajira hakuna, yapo mambo mengi ya kufanya.
Tunakutakia kila la kheri na endelea kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kuweza kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.
Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwau,
Simu; 0713 048035,
E-mail; dirayamafanikio@gmail.com

No comments :

Post a Comment