Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, March 4, 2016

Mambo Matatu (3) Ya Kufanya Pale Unapoona Mipango Yako Haiendi Vizuri.

No comments :
Katika maisha ya kutafuta mafanikio, mara nyingi kila mtu hupenda sana mipango yake imuendee vizuri kila siku. Lakini hata hivyo pamoja na nia hiyo, kiuhalisia bado kuna wakati mambo yanakuwa hayaendi sawa kama inavyotarajiwa. Hapo ndipo changamoto na kuanza kukata tamaa huanza kujitokeza kwa wengine.
Jambo la msingi la kujiuliza je, unapokabiliana na changamoto ama kuona mipango yako haiendi sawa kama ulivyopanga ni hatua zipi ambazo huwa unachukua? Kwa kawaida, ni lazima uchukue hatua za kukusaidia kwenda mbele, na si kukurudisha nyuma. Kwa kusoma makala haya utaelewa hatua za kuchukua pale mipango yako inapokwendea hovyo.
1. Weka nguvu zako nyingi kubadili hali hiyo.
Kuendelea kuishi jana na huku ukiwa ukiwaza sana pale ulipokosea kwenye mipango yako haitakusaidia sana. Kitu cha kufanya sasa ni kuweka nguvu zako zote kwa yale mambo unayoyataka kuyabadilisha. Mambo ya jana au mipango ya jana iliyokuwa inaenda vizuri haipo tena kilichobaki kwako ni historia tu na sasa unatakiwa kuibadili.
Tuchukulie kwa mfano kwenye  biashara yako ulikuwa na wateja wengi sana ambao kwa sasa huna. Kiuhalisia hapa, ili uweze kuwarudisha wateja hao kwako kwanza unatakiwa kujua tatizo ni nini lililosababisha ukose wateja. Baada ya hapo weka nguvu zako nyingi kuibadili hali hiyo. Kama utakuwa una mtafuta mchawi, badala ya kutafuta njia utakuwa unajipotezea muda.

PANGA MIPANGO YAKO UPYA TENA.
2. Panga mipango yako upya tena.
Inapotokea mipango yako haijaenda sawa hiyo isiwe ‘tiketi’ ya kukufanya ukaamua kuacha kila kitu. Hapo sasa ndipo unatakiwa kujipanga upya na kupanga mipango yako upya tena. Kushindwa kwako isiwe hapo ndio mwisho. Kaa chini na fikiri upya juu ya kupanga mipango yako upya tena na tena.
Hata wale watu wenye mafanikio makubwa, hawakufanikiwa mara moja kama unavyofikiri. Walishindwa kwa namna moja au nyingine, lakini kilichowasaidia walijipanga tena hadi kufikia makubwa. Chochote ukifanyacho kama hakiendi sawa, jipange tena kukifanya kwa upya. Hiyo itakuwa ni msaada mkubwa sana kwako.
3. Tafuta msaada wa kukutoa hapo ulipo.
Ni kweli unaweza ukawa kila ukiangalia mipango yako haiendi sawa kama ambavyo unavyotaka iwe. Utakuta umejaribu hili na lile lakini wapi, unaona kama haisadii. Kitu cha kufanya sasa inabidi ukubali na utafute msaada wa kukutoa hapo ulipo. Msaada huu utaupata kwa wengine waliopitia hali kama yako.
Hapo ulipo jaribu kuangalia au kufikiria ni nani unayeweza ukawa unamfahamu aliwahi kupita kwenye wakati mgumu kama wako. Ukimpata mtu wa namna hiyo mfuate akupe mikakati ya kipi cha kufanya. Acha kung’ang’ana mwenyewe sana kutafuta suluhu. Jichanganye na wengine wakupe mawazo mapya ya kukusaidia.
Kwa kifupi, hayo ndiyo mambo matatu unayoweza ukayafanya hasa pale unapohisi kwamba mipango na malengo haiendi sawa.
Nikutakie siku njema na uwe na mafanikio mema.
Ni wako rafiki katika kusaka mafanikio ya kweli,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048035,
E-mail; dirayamafanikio@gmail.com
Blog;  dirayamafanikio.blogspot.com

No comments :

Post a Comment