Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, March 16, 2016

Jinsi Ya Kutoa Huduma Bora Kwa Mteja Wako.

No comments :
Siku zote biashara ni mteja, bila mteja hakuna biashara yoyote ambayo inaweza ikawepo hapo. Biashara nyingi zinafanywa na kufanikiwa kwa sababu kuna wateja wanayoifanya biashara hiyo iendelee kuwepo. Kwa  maana hiyo kitu cha msingi kabisa katika biashara yoyote inayofanyika ni mteja.

Lakini pamoja na umuhimu huo wa mteja huyo katika biashara, kwa bahati mbaya sana biashara nyingi zimekuwa zikiendeshwa kiholela au kimazoea  sana na kusahau suala zima la utoaji wa huduma bora itakayomfanya mteja  aweze kurudi kwenye biashara yako kwa mara nyingine tena. Kwa sababu hii wengi wamekuwa wakipoteza wateja bila kujijua.

Kwa kusoma makala haya ya leo utajifunza mbinu au njia muhimu utakazoweza kuzitumia ili kuweza kumhudumia mteja wako kwa  ubora hali ya juu. Sasa je, unawezaje kutoa huduma bora itakayomvutia mteja wako wakati wote na kuwa na hamasa ya kuipenda biashara yako? Twende pamoja kujifunza kupitia makala haya.

1. Kuwa na lugha nzuri kwa wateja.

Katika biashara yako ili uweze kuwapata wateja wengi, jijengee mazoea ya kuwa na lugha nzuri kwa wateja wako. Naelewa kuna wakati wateja wanakuwa wanakera sana. Lakini hilo lisikufanye ukamfokea mteji wako na kuanza kumrushia lugha isiyofaa. Mjali mteja wako na kumuonyesha lugha nzuri hata kama amekukera. Hiyo itakuwa ni njia bora ya kutoa huduma bora kwa wateja wako na itakupa sifa wewe na kupelekea kujenga biashara bora.

WAPE HUDUMA BORA WATEJA WAKO.

 2. Ukaribisho mzuri kwa wateja.

Jenga mazoea ya kumkaribisha mteja wako vizuri. Mwonyeshe sura ya tabasamu ambayo hata bila kusema chochote itaashiria kwamba unamkaribisha kwa kumjali. Kuna watu ambao wanafanya biashara lakini utamaduni huu wa kumkaribisha mteja vizuri hawana. Kwa mfano kama una duka na mteja wako amefika na amekukuta unafanya kazi fulani. Achilia hiyo kazi na umsikilize mteja wako kwanza.


3. Kuwa na bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.

Siri kubwa ya kutoa huduma bora kwa mteja wako ni pamoja na kumpa mteja bidhaa zenye viwango vya juu. Kama utakuwa unatoa huduma bora inayoendana na thamani ya pesa ya mteja itasaidia sana kukuza wateja wako. Lakini hiyo haitoshi unapotoa huduma bora ya bidhaa inasaidia ili mteja akinunua bidhaa yoyote kwako anakuwa ana hamasa kubwa ya kurudi kwako tena kununua na hata kuwaambia wengine waje wanunue.

4. Jipe muda wa kuwasikiliza wateja wako.

Katika biashara kuna wakati huwa kuna malalamiko kutoka kwa wateja. Inawezekana kabisa mteja wako akawa hajaridhika na huduma fulani au ubora wa bidhaa unazotoa. Sasa inapotokea hali kama hii na akakwambia jifunze kuwasikiliza wateja wa namna hii na kufanyia mabadiliko mara moja. Ikiwa utamsikiliza na kufanyia kazi kile anachokitaka basi kesho elewa mteja huyo atakuwa wa kwako.

5. Mfanye mteja wako ajione wa thamani sana.

Unapokuwa kwenye biashara ni vyema ukajenga mazingira ya kumfanya mteja akijiona wa thamani. Mteja wako akishatambua hilo kwamba yeye ni wa thamani kwako, basi elewa kesho atakuwa ni wako tu hata iweje. Unaweza ukafanikiwa kwa hili ikiwa utajifunza kusimsikiliza mteja wako kwa makini, kujibu maswali yake vyema, ikiwezekana kwa mifano. Acha kupuuza chochote anachokwambia mteja wako, hata kama kinaonekana ni cha kijinga.

 6. Kuomba msamaha haraka sana kama bidhaa ina mapungufu.

Inapotokea kwenye biashara yako kukawa kuna mapungufu fulani, omba msamaha haraka sana. Tuchulie wewe unafanya biashara ya kuuza chakula halafu ikatokea chakula hicho hakijawa kizuri sana. Ili mteja wako aridhike na huduma yako, njia bora hapo kwako ni kuomba msamaha mara moja. Kama utaomba msamaha na kuahidi kesho utampatia huduma bora zaidi basi atakuelewa na hata kuwa na hasira na wewe tena na atakuwa mteja wako kwa siku nyingine. Kwa kumueleza, hiyo itampelekea kujenga imani kubwa na wewe.


7. Kuokoa muda wa mteja.

Pia huduma bora ni lazima iendane na kuokoa muda wa mteja. Acha kumfanya mteja wako kama mtoto kwa kumgandisha na kumtozea muda wake bila sababu. Mpe huduma mteja wako inayostahili kwa muda mwafaka. Kama unaona kuna eneo utachelewa ni bora ukamwambia ajue kuna kusubiri. Tatizo walilonalo wafanyabiashara wengi ni kuwapotezea wateja wao muda wakati mwingine bila sababu. Ili kuepuka kutokupoteza wateja, okoa muda wa mteja wako kwa kadri unavyoweza.

8 . Toa shukrani kwa mteja wako.

Mteja akishanunua kitu kwako au ukishampatia huduma ambayo wewe unatoa, jifunze kuwa na shukrani kwake. Mwambie tunashukuru kwa kuwa mteja wetu na karibu sana siku nyingine. Pia kwa kuongezea katika hili unaweza ukampa hata na mkono wa kumuaga. Unaweza ukaona ni kitu kidogo katika hili, lakini kitamfanya ajisikie vizuri na kesho atakuwa tayari tena kuweza kuja kwako.

Katika biashara wakati mwingine hauhitaji mtaji mkubwa sana ili kuweza kufanikiwa. Ila kwa kujijengea tabia ya kuwa na huduma bora kwa mteja ni njia nzuri sana ya kukuhakikishia mafanikio makubwa kibiashara. Chukua hatua na kuamua kutoa huduma bora kwa mteja wako kila siku.

Dira ya mafanikio tunakutakia mafanikio mema katika utoaji bora wa huduma kwenye biashara yako.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

Ni wako rafiki,

Imani ngwangwalu,

Simu; 0713048035,No comments :

Post a Comment