Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Thursday, March 10, 2016

Umuhimu Wa Mahusiano Bora Katika Mafanikio.

No comments :
Katika sekta yoyote ya mafanikio iwe ni biashara, elimu au shughuli za kila siku maofisini. Kipo kitu cha pekee kinachofanya mambo kwenda vizuri au vibaya na bila kuficha ni mawasiliano au mahusiano. Pengine ndio msingi mkubwa wa mafanikio.
Mtu anaweza kuwa na uwezo mkubwa sana ndani yake na nguvu za kufanikiwa lakini asifanikiwe. Naona unashangaa, ndiyo sijakosea unaweza ukawa na uwezo mkubwa wa kufanikiwa lakini usifanikiwe kwa sababu ya kukosa mawasiliano mazuri na wengine
Usiwe na mawazo potofu haujalogwa, wala sio kwamba huna bahati. Lakini swali ni kwamba je, unaishije na watu wanaokuzunguka?Je, unasaidianaje na wale watu unaotaka wakusaidie kufanikiwa? Je, unawazungumziaje watu hao?
Ili kufanikiwa ni lazima kujitengenezea mahusiano bora na wanaokuzunguka. Hata kama ikatokea kuna wakati kutokuelewana, jaribu kujenga mahusiano yawe bora zaidi hata kama unaona huna kosa kwako.
MAHUSIANO BORA NI MUHIMU KATIKA MAFANIKIO.
Mafanikio mara nyingi sana yanajengwa na mahusiano bora Inapotokea pale mmekoseana kwa namna fulani hivi, ni vyema kuvumiliana na kutambua kuweza kuishi na kila mmoja kwa kujua mwenzangu anataka nini na kitu gani ambacho hakipendi ili mweze kwenda pamoja katika safari ya mafanikio.
Siku zote mahusiano bora ndiyo yatakayokuletea furaha na mafanikio ambayo unayataka kila siku. Hakuna mtu anayeweza kukuharibia mafanikio yako zaidi wewe ufanye hivyo kwa kuzidi kuharibu mahusiano yako na ya wengine. Mafanikio yoyote hayajengwi na mtu mmoja. Bali yanajengwa kwa ushirikiano unaotakiwa kuuonyesha kila siku.
Jifunze na furahi kuwa sehemu ya mabadiliko kwa maisha ya watu wengine. Utafanikiwa kwa hili ikiwa utajijengea mahusiano bora na wengine.  Jiulize, je, unataka kuishi maisha ya mafanikio na kutokata tamaa, basi njia rahisi jijengee mazoea ya kuwa na mahusiano bora ya kudumu kila wakati.
Mawasiliano na mahusiano ni nguzo pekee ambayo Mungu alikupa kupata mafanikio kwa urahisi. Kumbuka unaweza kuamua kuwa wa tofauti kwa kuanza wewe kudumisha mahusiano bora na wengine. Hiyo itakusaidia sana kujenga maisha yako na kuwa bora siku zote.
Nikutakie siku njema na endelea kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila wakati.
Makala hii imeandikwa na Noel Ngowi,

No comments :

Post a Comment